TUACHE MASLAHI BINAFSI TUTAFUTE KATIBA YA NCHI
Na Prudence Karugendo
MCHAKATO wa kuandika Katiba mpya ya taifa letu umefika
mahali pagumu. Ni pagumu kwa vile mwenendo wa Bunge Maalumu la Katiba
hauonyeshi kutoa kile ambacho wananchi wanakisubiri kwa hamu sana.
Bunge hili
ambalo ni hatua ya mwisho ya mchakato wa kuipata Katiba mpya kabla ya wananchi
kuamua kama inawafaa kwa kuiridhia au kuikataa, linaonekana limejaa watu wenye
malengo na matamanio yanayotofautiana sana, kama vile wametoka nchi mbalimbali
tofauti, ila wote wakijiita Watanzania!
Sio kwamba
tofauti ninazoziona na kuzisema zinatokana na kile kilicholiunda Bunge hilo,
yaani makundi ya wanasiasa, ikiwa ni wa upande wa chama tawala na wa upinzani,
Wazanzibari na Watanganyika pamoja na wa makundi mengine kulingana na
ilivyomfurahisha rais katika uteuzi wake wa wajumbe wa Bunge hilo. Ninachokiona
ni kitu tofauti kabisa.
Utofauti
wake uko hivi; wamo wanasiasa walio katika pande mbili hasimu, yaaniwa upinzani
na wa chama tawala, ila uhasimu wao unafanana kwa namna moja au nyingine,
maslahi binafsi. Wale wa CCM wanaonekana kuutetea u CCM wao ambao inajionyesha
wazi kuwa hawautetei kwa kukipenda sana chama chao ila kwa maslahi yao binafsi
waliyoyawekeza kwenye chama hicho. Vilevile kwa upande wa upinzani nako wapo
wanaoonekana kuutetea upande huo wakionekana kuyasaka maslahi binafsi
wanayoyaona huko.
Wote hao, wa
upinzani na wa chama tawala, hakuna wanaosukumwa na uzalendo kwa nchi yao
kuyatetea wanayoyaona yanafaa kwa nchi yao na watu wake.
Ila pia wapo
wanaoonyesha uzalendo wa kweli wakionekana kukipigania kilicho bora kwa nchi
yao, hata kama hakitawanufaisha wao kwa
wakati huu, ila wakiangalia mbele wanaona kuwa kuna vizazi vijavyo.
Kitu cha
kwanza kilichonishtua na kunifanya nijiulize inakuwaje, ni pale mwenyekiti wa
Bunge hilo alipokuwa anatoa shukurani baada ya kuchaguliwa. Furaha
aliyoionyesha ilionekana kumvua uzalendo wake, sababu hakuonekana kama
kakabidhiwa jukumu la umma bali jukumu binafsi!
Furaha
aliyoipata ilimfanya awashukuru hata ambao hawakuhusika kumchagua! Maana
tukimuacha mke wake, ambaye naye ni mjumbe wa Bunge hilo Maalumu, pia
aliwashukuru watoto wake, majirani zake, waumini anaosali nao kanisa moja
nakadhalika!
Furaha hiyo
ya mwenyekiti, kusema ukweli, ilininyima
amani. Sikuuona uzalendo wowote katika furaha hiyo. Ile ilikuwa ni furaha
binafsi ikionyesha mafanikio binafsi, haikuonyesha mafanikio ya umma yanayoweza
kuashiria uzalendo wa mtu kwa nchi na watu wake.
Katika
kudhihirisha ninachokisema, tulimuona mwenyekiti wa Bunge Maalumu akibadilisha
au kukiuka kanuni za Bunge hilo mara tu alipokalia kiti chake. Alibadilisha
kanuni ili Jaji Warioba aanze kuwasilisha Rasimu hata kabla ya Bunge
kuzinduliwa.
Mbali na
mwenyekiti pia tulimsikia mbunge mmoja akidiriki kumwaga machozi akikataa mambo
yasiende kinyume na matakwa ya chama chake. Ni wazi mbunge huyo hakuwa
anaililia nchi yake wala chama chake, isipokuwa maslahi yake binafsi
aliyoyawekeza kwenye chama chake.
Baada ya
kujiridhisha kuwa limo tatizo la ubinafsi katika mchakato huu wa uandikaji wa
Katiba mpya ya nchi yetu, wananchi sote kwa pamoja, kama wazalendo, tunachotakiwa
kuwashauri wajumbe waliomo katika Bunge hilo maalumu ni kitu gani wanapaswa
kukifanya ili tuweze kukipata kile tunachokitarajia.
Na ushauri
wenyewe ni wa kwamba wayaweke pembeni maslahi binafsi kwanza, wawe kitu kimoja
wakiongozwa na uzalendo kwa nchi yao, tuipate Katiba ya nchi kwanza na mengine
yaendelee baadaye.
Ni kwa
sababu Katiba ya nchi haipaswi kuwa kitu cha wananchi kukitumia kukomoana,
badala yake Katiba ndio muongozo wa wananchi kufikia maelewano na hatimaye
makubaliano.
Maana
ikiandikwa Katiba inayoonekana kukibana chama kilicho madarakani kwa sasa huku
ikitoa unafuu kwa upinzani na kuuwezesha kushika madaraka kirahisi, tutakuwa
tumerudi kulekule tunakotoka. Tutakuwa tumetengeneza mchezo wa mzunguko ambao
Waingereza wanauita “marry go round”.
Sababu
inaaminika kwamba Katiba iliyopo inatumiwa vibaya na chama tawala, CCM, kwa
manufaa yake. Itawezekanaje hiyo mpya itakayoandikwa ionekane inawapendelea
wapinzani kiasi cha kuwaingiza madarakaini kirahisi nao wasiweze kuitumia
vibaya kwa manufaa yao dhidi ya wale ambao hawako madarakani? Je, na hao ambao
watakuwa hawako madarakani watakosaje kudai Katiba nyingine mpya? Si utakuwa
mchezo wa kuandika Katiba kila chama kinapoondolewa madarakani?
Kwa upande
wa CCM ni kwamba hawatakubali itengenezwe Katiba itakayowanyang’anya tonge
mdomoni. Ndiyo maana tunaona kwamba huu mchakato wa Katiba mpya umegubikwa na
makada wa chama hicho.
Mbali na
chama hicho kuwa na wabunge wengi, ambao ni kama robo tatu ya wabunge wote,
bado kuna makada wa chama hicho walioingizwa kwenye Bunge Maalumu kupitia
kwenye makundi ya vijana, wafugaji, wavuvi, waganga wa kienyeji nakadhalika.
Sio kwamba
makada hao wa CCM wamekuwa kwenye makundi hayo kwa bahati mbaya tu, la hasha,
ni wazi kwamba huo ni mpango mahususi wa chama hicho kuyalinda maslahi binafsi
ya makada wake ya wakati uliopo, kukiwa hakuna fikra ya kwamba kuna wakati ujao
na vizazi vijavyo huko mbele katika nchi hii!
Inawezekanaje
chama ambacho hakikuwa na wazo la Katiba mpya, kikiwa na imani kwamba Katiba
hii iliyovaa matambara yenye viraka vinavyopachikwa kulingana na matamanio ya
wakati, ndiyo inayofaa kudumu muda wote, leo hii kiwajaze makada wake kwenye mchakato
wa kuandika Katiba mpya? Nani anayeweza kuamini kuwa kuna nia njema katika
wingi huo wa wajumbe walio makada wa CCM?
Kwahiyo
tunapoiangalia hivyo CCM, kwamba haina nia njema na Katiba mpya, hatunabudi
kujivua umakundi na kuuvaa uzalendo ili CCM ipate fundisho. Ni uzalendo pekee
utakaowezesha Katiba mpya ipatikane.
Lakini
tukiendelea kuinyoonyea tu kidole CCM huku tukiwa tumejibanza kwenye u Chadema,
u NCCR, u CUF nakadhalika, hatuna namna yoyote tunayoweza kuwashawishi CCM
wajiondoe kwenye u CCM wao. Tutabaki kila mtu na kikundi chake tukicheza mchezo
wa mwenye kupata apate na mwenye kukosa akose.
Nilishasema,
na sasa narudia, kwamba Katiba ya nchi ya Marekani, taifa kubwa na lenye nguvu
za kila aina karibu kupita mataifa yote duniani, ilitengenezwa na watu 10 tu!
Watu hao hawakuwa na mlolongo wa mambo ya kupoteza muda bure kama hawa wa kwetu
zaidi ya 600.
Wale ni watu
waliouvaa uzalendo wa nchi yao wakiwa hawana ukada wowote wala umakundi wa aina
yoyote.
Walichokifanya
bado kinaheshimika hata baada ya miaka 226!
Je, hawa wa
kwetu zaidi ya 600, ambao wanachokifanya hawawezi hata kukiheshimu wao wenyewe,
kitaweza kuheshimika kwa wananchi hata kwa miaka 2 ijayo?
Sababu
kinachoonekana ni kila mjumbe kulipigania kundi lake. Mpaka tumeanza kushuhudia
matusi ya nguoni yakiwatoka baadhi ya wajumbe. Hivi kweli katika kutengeneza
Katiba ya nchi, kwa manufaa ya watu wote waliopo nchini kwa sasa na vizazi
vijavyo, yanaweza yakamtoka mtu matusi ya nguoni?
Je, naye
huyo tumuite mzalendo au ni mtu tu anayesukumwa na tumbo lake kuyatetea maslahi
anayoyaona kwa sasa bila kujua kama kuna kesho?
Wakati Jaji
Warioba anawasilisha Rasimu kwa kitu
ambacho kilikuwa hakijawa Bunge Maalumu, kwa vile lilikuwa bado
halijazinduliwa, alishauri Katiba mpya itambue serikali tatu katika Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Baada ya
hapo ndipo Rais Kikwete akaja kuzindua Bunge. Kabla ya kuzindua akaanza kuijibu
minong’ono aliyoikuta ya serikali tatu. Naita minong’ono sababu rais aliikuta
kabla ya kulizindua Bunge Maalumu. Kitu chochote kilichokuwepo kabla ya hapo
hakikuwa rasmi sababu Bunge halikuwepo. Yaliyokuwepo ni maandalizi tu.
Kwa maelezo
yaliyokuwepo ni kwamba Bunge Maalumu lingeanza kuitwa Bunge baada ya
kuzinduliwa na rais.
Katika
majibu yake kwa minong’ono iliyokuwepo ya serikali tatu rais alionekana wazi
kutetea serikali mbili. Sikumshangaa rais kutokana na mambo mawili. Kwanza yeye
alikula kiapo cha kulinda nchi yenye serikali mbili. Kwa maana hiyo ni lazima
akitetee kiapo chake. Nadhani nje ya hapo ingemwia vigumu kuendelea kujitambua
kama rais, rais wa nchi gani?
Kitu cha
pili ni kwamba, unapotaja serikali tatu maana yake ni kwamba Tanzania haipo
tena, na Muungano ndiyo basi. Kwahiyo
Katiba inayoandikwa ni ya nchi gani? Si bora ingesemwa kwamba inatafutwa Katiba
ya Tanganyika kwa vile Zanzibar tayari inayo Katiba ya kwake? Kusema ukweli kwa
hilo rais nilimuelewa.
Nimalizie
kwa kusema kwamba vyama 15 vya siasa visivyokuwa na wabunge, vinavyounda Baraza
la Vyama vya Siasa, vinajiwakilisha
vyenyewe na si wananchi. Walau vingekuwa na mbunge mmoja mmoja ningeamini
kwamba vinawawakilisha hao walioviwezesha vikapata mbunge mmoja mmoja.
Mwisho, ni
kwamba ingekuwa vema CCM nayo ikajiunga na Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA,
kama kweli chama hicho kinaitafuta Katiba ya wananchi. Kitendo cha kuwa nje ya
UKAWA kinadhihirisha kuwa CCM haitafuti Katiba ya wananchi bali inachokifanya
inakijua yenyewe!
0784 989 512