KAMA TUNAUTETEA NA KUULINDA MUUNGANO TUSIUCHOKONOE
Kama tunautetea na kuulinda Muungano
tusiuchokonoe
Na Prudence Karugendo
MNYUKANO unaoendelea kwa sasa katika Bunge Maalumu la
Katiba ni wa muundo wa Muungano wa Tanzania. Ni katika mjadala wa serikali
mbili dhidi ya serikali tatu kama zilivyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba
Mpya.
Mnyukano huo
umefikia kuwafanya UKAWA, Umoja wa Katiba ya Wananchi, kususia vikao vya Bunge
Maalumu. Hilo tuliache kwanza, tuangalie mjadala unavyoendelea.
Baadhi ya
wajumbe wanaonekana kuijadili Rasimu ya Katiba Mpya wakiwa wameiweka pembeni
kabisa dhima iliyopewa tume ya Mabadiliko ya Katiba, wakionekana kutoelewa
sababu yoyote iliyosukuma mpaka Tume hiyo ikaundwa na rais. Wanachokizingatia
ni kwamba wao ni wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba basi. Wanajifanya kutokuwa
na uelewa wowote wa kwamba Bunge hilo ni matokeo ya uwepo wa Tume hiyo
wanayoikashfu!
Wajumbe hao,
ambao wengi wanadai wanawasemea wananchi
ilhali wakielewa kwamba hawajachaguliwa na wananchi kwa ajili ya kazi hiyo,
wanaonekana kulazimisha mawazo yao ndiyo yaingizwe kwenye Katiba ya nchi yetu,
hasa muundo wa serikali mbili, kitu ambacho hakimo kweye Rasimu, tena kikiwa ndicho moja ya sababu kubwa za
kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Wajumbe hao
wanaotetea muundo wa serikali mbili katika Muungano wa Tanzania wanadai lengo
lao ni kuulinda Muungano huo. Sina hakika na madai yao hayo. Kinachonikosesha
uhakika huo ni hoja wanazozitoa zilizojaa mapengo.
Mapengo
katika hoja zao nayaona kupitia katika misimamo yao wanayoionyesha kwamba ni ya
kuulinda Muungano huku kauli zao zikionekana sumu kali kwa Muungano huo.
Ni kwamba
Tanganyika na Zanzibar zilipoungana mwaka 1964, baadaye kidogo lilibuniwa jina
linalofaa kwa muungano huo, jina hilo ni Tanzania, ikawa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, yakiwa yameunganishwa majina ya Tanganyika na Zanzibar.
Baada ya
hapo yakaja majina mawili ya Bara na Visiwani ili kutofautisha ni sehemu gani
ya muungano inayolengwa. Hiyo ni kwa sababu kutajwa Tanganyika kulionekana ni
kuuchokonoa Muungano kama ilivyokuwa kwa kuitaja Zanzibar.
Lakini
baadaye ikaanza kutajwa Zanzibar na Tanzania Bara, kitu ambacho ni kosa kubwa
kwa ustawi wa Muungano wa Tanzania. Sababu ukishataja Zanzibar kinachobaki ni
Tanganyika wala sio Tanzania Bara. Tukumbuke kwamba hakukuwepo kitu kinachoitwa
Tanzania Bara kabla ya Muungano. Hakikuwahi kuwepo na hakina maana yoyote nje
ya Muungano.
Mazoea hayo
ya kuuchokonoa Muungano yameendelea mpaka leo, hata wanaodai wanautetea
Muungano wanaitumia njia hiyohiyo ya kuuchokonoa, eti Tanzania Bara na
Zanzibar! Kana kwamba huku Tanganyika nako kulikuwepo na sehemu inayoitwa
Zanzibar. Hiyo ni sumu kubwa katika Muungano huo.
Kwa
kulishadidia hilo la kuungana, hebu tuzitazame mila za Kiafrika. Katika
tamaduni za Kiafrika mwanamke anayeolewa akang’ang’ania kutumia jina lake la
ukoo ni lazima aonekane hana nia njema na ndoa yake. Hiyo ni kwa sababu mahari
inayotolewa na upande wa mume, pamoja na mambo mengine, ni gharama ya
kubadilisha ubini wa anayeolewa.
Hata kwa
wazungu iko hivyohivyo, anayeolewa anaitwa Mrs. fulani, ubini wa alikoolewa.
Kwahiyo
mwanamke aliyeolewa kwa kutolewa mahari kuendelea kung’ang’ania ubini wake ni
kuitia ndoa yake kwenye misukosuko isiyo ya lazima. Tofauti iko kwenye tamaduni
za Kiarabu ambako mahari inaliwa na anayeolewa.
Mfano, hapa
kwetu mama mmoja aliolewa akaachana na jina la ubini wake, akaanza kutumia jina
la ukoo wa alikoolewa. Hata baada ya kuachana na mumewe bado anaendelea kutumia
jina la ukoo wa alikoolewa.
Ni mtu
aliyejiendeleza kibiashara na kupata umaarufu mkubwa kitaifa na kimataifa, akiwa
analitumia jina hilo kama alama ya biashara (Trade mark).
Kwa maana
hiyo, ni kwamba jina lina maana kubwa, iwe katika kuungana au kibiashara. Kulichokonoachokonoa
ni kuingiza mitafaruko kwenye muungano au kwenye biashara husika.
Ndiyo maana
nawashangaa wanaodai wanaulinda na kuutetea Muungano kuona hawalioni kosa hilo.
Wao wamekomalia Tanzania Bara na Zanzibar bila kujali kwamba tayari majina hayo
yanauvunja Muungano. Ni lazima walio makini waulize maana ya neno Tanzania
wanapoiona Zanzibar ikiwa pembeni.
Utasemaje
unakilinda kitu unachokichokonoa makusudi kuona kama kitaanguka au kubaki
kimesimama?
Katika
uchangiaji kuhusu muundo wa Muungano, katika Bunge Maalumu, wapo wachangiaji wanaojidhihirisha wazi kwamba
hawakielewi wanachokifanya. Mfano mtu anapewa dakika 10 za kuchangia, anatumia
dakika 8 au 9 kuwasakama wapinzani na kuitukana Chadema matusi ya nguoni.
Dakika 1 au 2 anamalizia kwa kusema sera ya CCM ni serikali 2, kamaliza!
Kweli tutegemee
kupata Katiba bora kwa michango ya mawazo ya aina hiyo?
Mwingine
anadai serikali 2 ni mhimu kwa vile watu wa Zanzibar na Tanzania Bara
wamezoeana na wanaoleana kwa muda mrefu! Huyo anachokiona katika serikali mbili
ni hicho!
Mwingine
atasema watu wa Zanzibar na Tanzania Bara wamezoea kufanya biashara pamoja. Hata
rais alisema kitu cha aina hiyo, kwamba alikwenda mahali, mkoa mmojawapo wa
Bara, akaambiwa mashamba anayoyaona ya vitunguu ni ya Wapemba!
Nasema
baadhi ya wajumbe, hasa walio makada wa chama tawala, wanaonekana hawakielewi
wanachokifanya. Maana wanashindwa kutofautisha Bunge Maalumu la Katiba na kikao
maalumu cha chama chao! Mawazo yao yanajionyesha yanavyorudi nyuma zaidi ya
miaka 25 iliyopita wakati chama chao kilipokuwa kimeshika hatamu za kila kitu
kikiipeleka nchi kama farasi asiyejua anakoelekea, kibaya zaidi kikishindwa
kumpa farasi huyo walau dakika moja ya
kunywa maji!
Wajumbe wa
aina hiyo hawakumbuki kuwa chama chao kinao wanachama wasiofikia hata milioni
5, wakati wanachama hai, kwa maana ya wanaofuata kanuni zote za chama, hawazidi
laki 5, wakati suala linaloshughulikiwa ndani ya Bunge Maalumu likiwa
linawahusu wananchi wote wa Tanzania wanaokaribia milioni 50!
Kwahiyo
kutojivua ukada wa chama wakati wa kuandika Katiba ya nchi ni tatizo kubwa
sana. Ni tatizo linalotishia upatikanaji wa Katiba yenyewe pamoja na
mustakabali wa nchi kwa ujumla. Ni suala la vizazi vilivyopo kutovitendea haki
vizazi vijavyo.
Mambo ya
kuzoeana na kuoleana kati ya Wazanzibari na Watanzania Bara, kama yanavyoelezwa
na baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu, yanaingilianaje na suala la Katiba ya
nchi? Au tuseme serikali tatu zinawezaje kuliondoa jambo hilo?
Hata kama ni
nje ya Muungano kitu hicho kinawezaje kutoweka? Mbona Watanzania wanazoeana na
hata kuoleana na Wakenya, Waganda, Warundi na hata Wanyarwanda? Ina maana wote
hao wanashawishiwa na muundo wa muungano wa serikali 2 wa Tanzania?
Ieleweke
kwamba Watanzania, kibinafsi, wamezoeana na hata kuoleana na watu wa mataifa ya
mbali katika mabala kama Ulaya, Marekani, Asia na kwingineko, bila kuathiriwa
na muundo wa serikali yao. Kwahiyo wanaotaka kuliingiza hilo katika muundo wa
serikali linapokuja suala la Muungano wa
Tanzania waelewe wana yao mambo, kwa kulielewa jambo hilo au kwa kuburuzwa tu.
Wengine
wanajenga hoja kwamba serikali tatu zitaongeza gharama za uendeshaji wa
serikali hizo. Hao wanajifanya wanayajali sana matumizi ya serikali! Lakini
wakichunguzwa vizuri si ajabu watu hao wakakutwa ndio haohao waliokuwa wanadai
kwamba shilingi laki tatu kutwa kwa kila mjumbe wa Bunge Maalumu ni kidogo
sana!
Sasa
wanaposema gharama za uendeshaji wa serikali tatu zitakuwa kubwa sana ni kweli
wanakimaanisha wanachokisema?
Kuhusu
Wapemba kuwa na biashara Bara kunaingilianaje na serikali 3? Kwani wapo watu wa
mataifa mangapi waliowekeza hapa kwetu Tanzania? Je, hao nao wanavutiwa na
muundo wa serikali 2 katika Muungano wa Tanzania?
Mwisho
kabisa yatubidi tuelewe kwamba taifa kubwa, lenye nguvu kubwa sana na uchumi
imara sana dunaini, Marekani au “United States of America”, lina Muungano wa
serikali 51.
Nchi, ambazo
kwa sasa yanaitwa majimbo, 50 ziliungana, na kila jimbo likiwa na uchumi ulio
imara kuzidi uchumi wa Tanzania kwa mbali. Juu ya serikali hizo 50 kuna
serikali kuu inayoifanya idadi ya serikali za nchi hiyo kuwa 51.
Ni kitu gani
kimeishaharibika kutokana na muundo wa muungano huo ulio na umri wa zaidi ya
miaka 200? Kwa nini sisi tunapoangalia upya muundo wa muungano wetu tusivutiwe
na muundo huo wa Muungano wa Marekani?
Kwa nini
tuvutiwe tu na utajiri wa muundo huo huku tukijijengea uhalali wa kwenda kila
mara kuomba misaada, tukijifanya vipofu bila kuangalia na kujifunza mbinu
walizozitumia wenzetu kuwa imara kiuchumi kama hivi walivyo?
Marekani
wanazo serikali 51 na ni matajiri kupindukia, katika Tanzania wapo wanaodai
kwamba serikali 3 zitakuwa mzigo,
hatuziwezi! Je, hao wajumbe wenye madai ya aina hiyo wanakielewa
wanachokifanya?
0784 989 512