MUUNGANO WA SERIKALI MBILI NI ENDELEVU KISHERIA NA KISIASA
Ndugu zangu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba na Maoni ya
Wananchi
Rasimu ya
Katiba imeandikwa kwa kuzingatia na kuongozwa na maoni ya wananchi, ambayo
yamechambuliwa na kupewa tafsiri kwa makubaliano ya pamoja ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba. Naamini kwamba, hadi Tume inafikia makubaliano ya nini kiwekwe
kwenye Rasimu ya Katiba na nini kiachwe, ulikuwepo mchuano mkali wa
kubishanisha fikra ndani Tume. Hivyo basi, Tume ya Mabadiliko ya Katiba
inastahili kila aina ya pongezi kwa kufanikisha kazi hii kubwa, nzuri na ya
maana sana kwa Tanzania yetu. Mwenyezi Mungu akulipeni kheri na baraka. Pia
nitumie fursa hii kumpongeza Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa busara wa
kuiunda Tume hii.
Kila Kazi Ina Mapungufu
Hakuna kazi
isiyokuwa na mapungufu isipokuwa kazi za Mwenyezi Mungu tu. Katika kujadili
mapungufu au mazuri katika ya kazi za wenzetu tujadili hoja katika kazi hizo na
tujiepushe kabisa kuwajadili watu wanaohusika, kwa namna moja ama nyingine,
katika mchakato wa kuziandaa kazi hizo. Kuwajadili watu hawa ni kuupeleka
mjadala ndiko siko; ni ukosefu wa hoja ya kujibu hoja iliyoko mbele yako. Na
matokeo yake ni kejeli, matusi na kutunishiana misuli.
Rasimu ya
Katiba si msahafu kutoka kwa Mola Mwenyezi kwamba ni haramu kubadilishwa hata
herufi moja. Rasimu ya Katiba, kama kazi nyinginezo za wanadamu, inayo
mapungufu yake, kwa mfano, INAUZIKA UJAMAA. Lakini pia inayo mambo mengi mazuri
sana, kwa mfano, MIIKO YA UONGOZI. Mapungufu haya ni lazima yajadiliwe. Kuzuia
kuyadili mapungufu yaliyoko katika Rasimu ya Katiba si jambo la hekima.
Misingi ya Mjadala-shirikishi na
Endelevu
Ili mjadala
wowote ufanikiwe katika mawasiliano shirikishi, washiriki ni lazima wafuate
misingi ya KUHESHIMIANA, KUSIKILIZANA, KUSTAHIMILIANA na ADABU zake. Kwamba
kila mchangiaji katika mjadala bila kujali itikadi, dini, rangi, jinsia, umri
n.k anayo nafasi ya kutoa maoni yake bila woga, akasikilizwa, na hoja yake
ikakoselewa kwa hoja na si kwa kumrushia matusi ya nguoni mtoa hoja; au hoja
ikaungwa mkono na kupongezwa kwa amani. Mjadala unaofuata misingi hii siku zote
huzaa matunda mema kwa washiriki.
Katika
kulijadili jambo, ingawa kila mshiriki anakuwa na mtizamo wake, washiriki
huanza kwa kuiangalia hoja inayowaunganisha wote -- kwa maana wote
wanakubaliana au wana mtizamo sawa katika hoja hiyo. Kuanzia hapo hoja nyingine
hujengwa juu ya hoja hiyo tena kwa mchuano mkali na hatimaye washiriki hufikia
makubaliano -- kwa maana ya KUKUBALI-KUKUBALIANA, mkasonga mbele na kufikia
muafaka-endelevu; au KUKUBALI-KUTOKUKUBALIANA, mkatofautina na mkabaki mlipo au
hata kurudi nyuma zaidi kwa kuibua tofauti nyingi na kuwekeana kila aina ya
vipingamizi.
Mjadala wa Serikali Moja/Mbili/Tatu/Mkataba
Katika
kuijadili Rasimu ya Katiba kuhusu suala la serikali moja au mbili au tatu
tuanzie na hoja inayokubalika kwa wote: Kwamba tunaupenda Muungano wetu na
tutaudumisha. Kwamba Tanzania ni nchi moja yenye serikali mbili ambazo ni
matokeo ya kuungana kwa nchi mbili huru (kwa maana ya dola huru) za Tanganyika
na Zanzibar kwa hiari. Kwamba Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar katika nchi ya
Tanzania zina mipaka yake inayojulikana. Kwamba sababu walizozitoa waasisi wa
Muungano huu za kuwa na muundo wa serikali mbili katika Muungano ili kuepuka
kuimeza Zanzibar na pia kupunguza gharama za uendeshaji kuwa kubwa hasa kwa
Tanzania Bara (Rejea Hotuba ya Mwalimu Nyerere katika kitabu cha Nyufa), sababu
hizi bado zina mashiko na ni mwongozo mwema katika mjadala wetu wa sasa; kwa
hiyo ni jambo la busara sababu hizi zikafuatwa. Hapa ndipo pa kuanzia.
Kukubali-kukubaliana katika hoja hizi hakumaanishi kwamba wale wanaotetea
serikali mbili wameshinda, na wale watetezi wa serikali moja/tatu au muungano
wa mkataba wameshindwa. La hasha! Bali ni kukubaliana na hali halisi ilivyo.
Kwa mfano, suala la kila sehemu ya Muungano kuwa na mipaka yake inayojulikana
si jambo baya ila tatizo linaibuka unaposema, ‘Zanzibar ni nchi yenye dola huru,’
kwa kutumia kigezo cha kuwa na mipaka yake. Zanzibar itakuwaje NCHI YENYE DOLA HURU,
KWA MAANA HALISI YA NENO SOVERIGN STATE, ili hali iliishajivua hadhi hiyo na
kuwa sehemu ya NCHI YENYE DOLA HURU ya TANZANIA kama Tanganyika ilivyofanya?
Mipaka inayojulikana kimataifa ni ya Tanzania na si ya Tanganyika au Zanzibar.
Katika hili la mipaka utaiona faida ya Muungano kwa wepesi kwani ni rahisi
kwetu kuwa na mpaka mmoja wa kimataifa katika Bahari ya Hindi kuliko nje ya
Muungano. Pia jiografia inaufanya Muungano wetu kuwa ni wa asili kwani ni
rahisi kwa mkazi wa Pemba kusafiri kwenda Tanga kuliko kwenda Unguja. Vivyo
hivyo kwa Unguja na Bagamoyo. Kama busara itatumika, hoja iko wazi kwamba
Zanzibar ni sehemu ya Tanzania yenye mamlaka yake ya ndani kwa maana ya NCHI
NDANI YA NCHI (AUTONOMOUS REGION) – kwa mujibu wa Katiba ya Muungano na si
vinginevyo. Na Muungano upi huo MKATABA? Kwani huu Muungano uliopo si wa
mkataba? Kwani Hati ya Muungano si MKATABA (au Hati hii ilitokana na nini)?
Mkataba upi mnaoutaka? Mkataba wa Zanzibar kama dola huru? Kama msimamo
utashikiriwa wa Zanzibar ni NCHI KAMILI YENYE DOLA HURU kwa sababu na maslahi
ya watu binafsi na si kwa maslahi nchi ya Tanzania basi tujue wazi kabisa
kwamba Katiba mpya haitapatikana mpaka Tanganyika nayo imekuwa nchi kama Tume
ya Mabadiliko ya Katiba ilivyopendekeza. Na kwa kuirejesha Tanganyika kama nchi
yenye dola huru tutakuwa tunarudi kabla ya tarehe 26 Aprili 1964. Na hapo
HAKUNA Muungano! Nitafafanua.
SERIKALI TATU NCHI TATU NI JAMBO AMBALO
LINAWEZEKANA KISHERIA LAKINI SI JAMBO ENDELEVU KISIASA.
Kwa kuwa
jambo hili si endelevu kisiasa basi halitufai. Kisheria utakuwa na Marais
watatu wenye mamlaka juu vyombo vya dola. Marais watu wenye majeshi na wakiwa
na mamlaka ya kutangaza hali ya hatari. Kisheria jambo la Rais nchi ya
Tanganyika au Zanzibar kuwa amri jeshi mkuu wa nchi yake ndani ya Muungano
linaonekana kuwa liko sawa lakini kisiasa halifai. Hebu fikiria itakuwa vipi
Rais wa Tanganyika akaamua kujitangazia hali ya hatari na yule wa Muungano na
wa Zanzibar wakataa? Na hapa ikumbukwe kuwa Marais hawa watatu wanaweza kuwa
wanatokea vyama tofauti vya siasa vyenye misimamo tofauti kabisa – hawapikiki
chungu kimoja. Au wawili wao wakiwa wanatoka chama kimoja cha siasa na
wakajenga genge la kumtenga Rais mwenzao. Iko hatari kubwa sana hapa.
Tutajikuta tuko chini ya wababe wa kivita. Serikali ya Muungano katika mfumo
huu itakuwa haina vyanzo vya mapato. Na huwezi kutoa suluhisho la tatizo la
mapato kwa kuesema kwamba ‘kodi ya bandari inatosha kuendesha serikali ya Muungano.’
Haya ni mapungufu makubwa sana katika utoaji hoja kwani mapato ya bandari
yanaweza kuwa pungufu katika mwaka fulani na kuiach serikali ya Muungano ikiwa
na naksi. Nani ataipatia pesa ya kujiendesha? Na kama kuna tofauti za kisiasa
kati ya marais watatu bila shaka itakuwa vigumu sana kwa serikali ya Muungano
kupata mapato ya uhakika. Matokeo yake itashindwa kujiendesha na ofisi za
Muungano zitafungwa na Muungano utavunjika. Tuwe makini sana. Tusifuate hisia
na haja binafsi bali tuongozwe na uhalisia wa mambo na ukweli wa hoja iliyo
wazi kwamba nchi (dola huru) ni Tanzania yenye serikali mbili -- Serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Mgogoro wa
Kikatiba uliopo sasa kwamba Baraza la Wawakilishi linaweza kuiikataa sheria ya
Bunge la Muungano ni mfano mdogo tu wa utata mkubwa wa kisheria na kisiasa
utakaoibuka baada ya kuwa serikali tatu na nchi tatu.
Katika muundo
wa serikali tatu, wenye serikali za Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya
Tanganyika, zenye dola huru na mamlaka kamili kama taifa-nchi, hakuna Jamhuri
ya Muungano hapo kwa maana ya taifa-nchi moja ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, bali kutakuwa na Shirikisho la Jamhuri za Tanzania au Jumuiya ya
Jamhuri za Tanzania zenye mkataba wa kushirikiana kisiasa, kiuchumi, kiulinzi na
kijamii pale inapobidi. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja ili hali tuna utambulisho
tofauti kimatiafa -- kila mmoja akiwa na kiti chake Umoja wa Mataifa, Umoja wa
Afrika na kwingineko. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja ili hali kila mmoja ana
mahusiano yake kimataifa na sera zake za nje. Hatuwezi kuwa taifa-nchi moja
Tanganyika na Zanzibar zina marais wasiowajibika kwa Rais wa Muungano kwani
watakuwa wanaongoza mataifa-nchi yenye dola kamili. Hatuwezi kuwa taifa-nchi
moja kwa kuanzisha, kurasimisha na kuhalalisha, tena kwa makusidi kabisa
ukabila na ubaguzi katika Katiba. Kwamba “wao watanganyika, sisi wazanzibari.”
Kwa kufuata muundo wa serikali tatu tutakuwa temeanzisha rasmi mchakato wa
kuiuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ambavyo Rasimu ya Katiba inavyouzika
Ujamaa.
Zanzibar na OIC
Inasikitisha
kusikia kwamba miongoni mwa hoja za kuwa na muundo wa serikali tatu ni kuipa
Zanzibar uhuru wa kujiunga na OIC kwamba itaneemeka. Hoja hii haina mashiko.
Hakuna uhusiano wala ushahidi wowote kati ya nchi fulani kuneemeka eti kwa kuwa
ni mwanachama wa OIC. Somalia ingekuwa ya kwanza kupatiwa misaada ya kila hali
na mali kuondoa vita na umaskini lakini nani katika OIC kaisaidia Somalia?
Mpaka leo wanapigana na kuuwana. Nchi wanachama wa OIC nyingi ni tajiri sana na
ni pua na mdomo na Somalia lakini hazijawahi kuwa mstari wa mbele kuisaidia
Somalia ipate amani. Kumbe kuwa OIC si suluhisho la matatizo ya kiuchumi,
kijamii na kisiasa kwa nchi wananchama. Pia tukumbuke kwamba katika nchi hizi
OIC za mashariki ya kati moto unawaka. Kila uchao watu wanachinjana. Je,
watakuja kuisaidia ya Zanzibar ili kwao kunabomoka? Na hali hii ya ukosefu wa
amani na utulivu katika nchi hizi kwa jinsi mambo yalivyo haishi leo wala
kesho. Kwa hiyo suluhisho la umasikini wa watu wa Zanzibar ni watu wenyewe,
uongozi bora na siasa safi na kuzitumia raslimali zilizopo kuondoa umasikini na
si kutegemea kwamba OIC itakuja kuuondoa. Fikira hizi za kutegemea misaada
hazijengi. Ni fikira za kudumaza ustawi na kudumisha utegemezi na ukoloni.
Mtegemea cha nduguye hufa ili hali masikini, wahenga walisema. Na hata kama
Zanzibar itapata misaada ya OIC na Tanzania Bara je, hakuna waislamu? Wapo.
Pili Zanzibar inaweza kupata misaada kutoka nchi za OIC bila kuwa mwanachama.
Hili linaweza kufanywa na kufanikiwa ikiwa viongozi watafanya jitihada za
kuitafuta misaada hiyo na kuifikisha kwa walengwa.
Muundo Upi wa Muungano Unafaa?
Rejea Historia
Busara
itumike sana katika kuangalia muundo wa Muungano. Ni muundo upi unatufaa kama
Tanzania? Tukirejea katika historia tunazikuta sababu nzuri ya kuwa serikali
mbili ambazo zinamashiko mpaka leo hii (kama nilivyosema hapo juu). Mojawapo ni
kutokumezwa kwa Zanzibar. Naamini hali ingekuwa ngumu sana sasa kama Muungano
wetu ungekuwa serikali moja. Wale wanaosema Zanzibar ni koloni kwa hakika hoja
yao ingekuwa moto wa kuotea mbali. Serikali tatu jibu lake ni hakuna Muungano
bali Jumuiya tu. Katika kuimarisha Muungano tulikuwa na Rais wa Muungano
akisimamia shughuli zote za Muungano na Tanzania Bara (Tanganyika). Pia tulikuwa
na Makamu wa Rais wawili -- Rais wa Tanzania Zanzibar na Waziri Mkuu katika
serikali ya Muungano na Tanzania Bara. Ulikuwa ni muundo mzuri kabisa. Rais wa
Muungano alikuwa na mamlaka juu ya Rais wa Zanzibar kwani huyu alikuwa ni
Makamu wake wa Kwanza au wa Pili. Pili Rais wa Zanzibar alikuwa na hadhi yake
kamili katika Muungano. Tatu Waziri Mkuu alikuwa na hadhi yake kama Makamu wa
Rais Muungano huko Tanzania Zanzibar. Ni kweli kuna wakati fulani Rais wa
Zanzibar ndiye alikuwa Makamu Rais pekee yake lakini hili halikumuondolea hadhi
Waziri Mkuu huko Zanzibar (Rejea wakati Aboud Jumbe akiwa Makamu wa Rais). Muungano ulikuwa imara. Ni kutokana na uimara
huu ndio maana Muungano hakuvunjika mwaka 1984. Pia ulikuwepo wakati Makamu wa
Rais na Waziri Mkuu wote walitokea Zanzibar (Rejea wakati Alli Hassan Mwinyi
akiwa Rais wa Zanzibar na Dr. Salim Ahmed Salim akiwa Waziri Mkuu). Utaifa huu
umeishia wapi?
Madhara ya G55 kwa Muundo wa Uongozi wa
Muungano
Katika muundo
wa sasa wa uongozi wa serikali ya Muungano uliojitokeza baada ya vuguvugu la
G55 la kuidai Tanganyika, Zanzibar kutaka kujiunga na OIC na kuelekea kwenye
uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi wa 1995, Rais wa Zanzibar si Makamu wa Rais
katika serikali ya Muungano, hivyo basi hana sauti katika serikali ya Muungano.
Pia Waziri Mkuu wa Tanzania hana sauti yeyote Zanzibar. Matokeo yake hadhi ya
viongozi hao ipo tu kwa sababu ni watu wanaotoka chama kimoja na si vinginevyo.
Matokeo yake Rais wa Zanzibar hawajibiki kwa Rais wa Muungano. Atawajibika
kwake kama nani? Siyo Makamu wake. Ndiyo maana hata utaratibu wa kuteuliwa
wakuu mikoa ya Zanzibar kwa Rais wa Zanzibar kushauriana na Rais wa Muungano
unafutwa na Katiba ya Katiba ya Zanzibar ingawa hii ni kinyume na Katiba ya
Muungano. Kumbe ikitokea ‘Kuchafuka kwa Hali ya Hewa Zanzibar’ kama ilivyokuwa
mwaka 1984 hakuna mwenye mamlaka ya kumzuia Rais wa Zanzibar kuuvunjwa
Muungano. Hayupo. Labda kupitia vikao vya vyama vya siasa ambavyo haivitakuwa
na nguvu tena hali hiyo ikijitokeza. Pia kwa Makamu wa Rais wa Muungano na
Waziri Mkuu wa Muungano ukiuliza wana mamlaka gani kule Zanzibar ni vigumu
kupata jibu. Hawana sauti. Wanaheshimika tu kiungwana. Kumbe katika kumdhibiti
Rais wa Zanzibar mwaka 1994, G55 ilituachia muundo wa kiuongozi wa serikali ya
Muungano unaoendeshwa kiungwana tu. Jambo hili ni kikwazo kikubwa sana kwa uhai
wa Muungano wa serikali mbili nchi moja. Huu ndiyo ukweli na
tulisahihishe.
Mabadiliko ya Katiba Zanzibar 2010
Mabadiliko ya
Katiba Zanzibar ya 2010 ambayo yanasema Zanzibar ni nchi (dola huru), ingawa
yanaonekana ni ukombozi wa kuipa Zanzibar hadhi ya nchi, lakini yako kinyume
kabisa na Katiba ya Muungano. Ni kinyume na tamko kwamba nchi za Tanganyika na
Zanzibar ziliungana kuunda nchi moja iitwayo Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kimsingi kwa mabadiliko haya Katiba ya Zanzibar iko juu ya Katiba ya Muungano.
Kwamba sheria zikitungwa na Bunge la Muungano ambalo lina wabunge kutoka
Zanzibar lazima ziidhinishwe na Baraza la Wawakilishi ili ziweze kutumika
Zanzibar. Iko wapi nchi moja hapo ya Tanzania? Au Baraza la Wawakilishi ni
Bunge la Seneti la Muungano? La kusikitisha wakati mabadiliko haya yanafanyika
hakuna aliyeyakemea. Matokeo yake sasa ni hiki kizungumkuti kilichopo.
Kwa kuwa
yalifanyika makosa haya basi tusiyatumie pamoja na kero zilizopo kuhusu
Muungano kujenga hoja za kuleta muundo wa serikali tatu ambao kimsingi utakuwa
mbovu zaidi ya ubovu uliopo katika muundo huu wa sasa. Kazi iliyoko mbele yetu
ni kusahihisha makosa yote haya kwa maridhiano ya kukubali kukubaliana.
Dhana Potofu Kuhusu Muungano
Katika
kujadili muundo wa Muungano tusisahau kwamba katika miaka 50 ya Muungano
yamekuwepo makosa mengi yaliyofanywa
ambayo yamesababisha chuki dhidi ya Muungano. Yamefanyika mabadiliko
mbalimbali ya Katiba na sheria ili kukidhi haja binafsi za baadhi ya viongozi.
Makosa haya yasitumike kupandikiza mbegu ya kuuvunja Muungano kwa kuchochea
muundo wa serikali tatu. Pia Muungano umezushiwa dhana nyingi potofu
zinazolenga kuuvunja. Ipo dhana kwamba Muungano ni matokeo ya kazi za kijasusi
za wamarekani kwa kumtumia Mwalimu kuimeza Zanzibar; kwamba mchakato wa
kuanzishwa Muungano ulikwenda haraka mno tena bila ya ushauri na hivyo basi
Muungano si halali. Ufe. Uzikwe. Usahaulike. Dhana nyingine inasema kama
Nyerere angelikuwa kweli anaupenda Muungano wa Afrika basi angemshauri rafiki
yake Kenneth Kahunda ili Zambia nayo iingie kwenye Muungano wetu. Dhana hii
nayo inahitimisha kwa kushadidia kwamba hatima ya Muungano wa Tanzania ni
kuvunjika kama ulivyovunjika muungano wa Ghana na Guinea, au ule Senegal na
Gambia. Hata Muungano wa Uingereza nao uko kwenye hati hati ya kuvujika kwani
Uskoti (Scotland) inataka kujietenga. Pia ipo dhana kwamba madhumuni ya waasisi
wa Muungano yalikuwa ni serikali tatu. Kwa hiyo serikali tatu zinarudi kwenye
mzizi wa madhumuni ya Muungano. Dhana hizi zote msingi wake mkubwa ni
kupandikiza chuki dhidi ya Muungano. Na hoja zake hazilengi kuijenga Tanzania
imara bali zinalenga kuiangamiza kwa kuuvunja Muungano wetu.
Kero za Muungano
Kero za
Muungano zimekuwa zikitajwa kama mapungufu katika Muungano. ‘Kero za Muungano’
zisiwe chachu ya kukimbilia muundo wa serikali ya mkataba au tatu kwa kuanzisha
serikali na nchi ya Tanganyika bali ziwe ni nyenzo za kutusaidia kutafuta dawa
mujarabu ya kero hizo. Tusahihishe. Tuboreshe. Tusivunje. Kero zote
zinazungumzika na zina dawa mujarabu kama nia ya dhati ya kuulinda Muungano
ipo. Kiimsingi kuundwa kwa serikali tatu, kutokana na utata unaozunguka
mapendekezo hayo tena kwa mujibu wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, kutauvunja
Muungano. Na matokeo yake ni kero kubwa zaidi ya “sisi na wao.”
Mjadala Bungeni Ulenge Kujenga na Si
Kubomoa
Katika kuamua
ni muundo upi Muungano tuufuate, Bunge la Katiba, lifikirie kwa busara na
mapana sana, tena kwa maslahi ya nchi yetu Tanzania na si kwa maslahi ya vyama
vya siasa au kundi la watu fulani. Kama maamuzi yatachuliwa ya kulinda maslahi
binafsi baadala ya maslahi ya Tanzania tutajikuta tunauvunja Muungano. Kwa
hiyo, umefika wa wakati sasa wananchi, vyama vya siasa na asasi za makundi
mbalimbali na wabunge wa bunge la Katiba kukubali kukubaliana kwamba muundo
muafaka utakaodumisha Muungano ni muundo wa serikali mbili. Nje ya serikali
mbili au ndani ya serikali tatu kuna “sisi ni watanganyika wao ni wazanzibari.”
Tutakapoanza kuitana “sisi na wao” hakuna Muungano hapo. Kikatiba na kisheria
mtajiita Watanganyika na Wazanzibari lakini kisiasa mtakuwa mmevunja UTANZANIA
NA UDUGU UTOKANAO NA UTANZANIA HUO. Ubaguzi huu hautaishia hapo, utaitafuna
Tanganyika na Zanzibar milele. Hatutasalimika. Utaifa utakufa na ukabila
utatawala – “Wazanzibari na Wazanzibara”. (Rejea Hotuba ya Mwalimu Nyerere ya
Nyufa).
Sasa nini kifanyike ili kuleta
makubaliano ya kukubali-kukubaliana katika mjadala wa Bunge la Katiba kuhusu
muundo Muungano wa serikali mbili ?
1. Heshima na kuthamini utu ni vitu adhimu
sana hivyo basi uwepo wa nidhamu, hekima, busara na umakini katika kujadili
Rasimu ya Katiba katika Bunge utaliwezesha Bunge kufikia makubaliano. Uzalendo
na nia ya dhati ya kupata Katiba nzuri viwe muongozo mkuu. Kwamba wabunge wajiepushe
na kutumia lugha chafu ya matusi, kejeli na vitisho kwani kwa kufanya hivyo
mtakuwa mnaubomoa upendo, umoja na udugu wetu na mnajenga hasira, chuki na
uhasama. Katiba bora haitapatika kupitia hali ya uhasama na kutokuaminiana
iliyopo kwa sasa katika Bunge. Wabunge wawe na ustarabu wa kusikiliza,
kushauriana, kusahihishana, kukosoana na hata kurekebishana kwa kusikilizana na
si kwa kupayukiana na kutukanana na hata kutunishiana misuli kama
tunavyoendelea kuona. Jazba au kupayuka si ishara ya uzalendo.
2. Mjadala wa Rasimu ya Katiba usigeuzwe
kuwa mjadala wa kujadili watu. Mtakuwa mnapoteza mwelekeo, muda na pesa za
wananchi kwa kuwajadili watu. Katika kuwajadili mnaweza kujikuta mnateleza
ulimi au hata kwa makusidi na kuwatukana mnaowajadili kutokana na jazba na
hatimaye mkaonekana ni wachache wa adabu. Pia yako mambo mengi muhimu sana ya kujadiliwa,
likiwemo suala la ITIKADI YA UJAMAA, na si muundo wa Muungano peke yake ingawa
Muungano ndiyo nchi yenyewe -- Tanzania.
3. Tanzania Zanzibar ikubali kubadilisha
Katiba yake ili isipingane na Katiba ya Muungano. Tukumbuke kwamba waasisi wa
Muungano waliweka MUUNDO WA NCHI MOJA, TANZANIA, YENYE SERIKALI MBILI.
4. Kiongezewe kifungu katika Rasimu ya
Katiba kwamba Tanzania iwe na Makamu wa Rais watatu. Cheo cha Makamu wa Rais
anayetokana na nafasi ya Mgombea Mweza kiendelee kuwepo ili kuondoa utata wa
nani atakuwa Rais endapo nafasi ya Rais itakuwa wazi kwa mujibu wa Katiba na
hasa pale Makamu wa pili na watatu wa Rais wakiwa wanatokea vyama vya siasa
tofauti na Rais (hili linaweza kutokea). Makamu wa Rais atokanaye na mgombea
mwenza atajulikana kama Makamu wa Kwanza wa Rais.
5. Waziri Mkuu wa Muungano na Rais wa
Zanzibar wawe ni Makamu wa Rais kwa nafasi zao – Makamu wa Pili na Makamu wa
Tatu. Tukifanya hivi tutakuwa tumewapa viongozi hawa hadhi yao katika serikali
ya Muungano. Ukosefu wa hadhi ya viongozi hawa katika Muungano ni kikwazo
kikubwa kwa Muungano imara. Pili Rais wa Jamhuri ya Muungano atakuwa na mamlaka
kwa Rais wa Zanzibar kwani atakuwa ni miongoni mwa Makamu wake.
6. Kwa kuwa hofu kuu inaweza kuwa juu ya
utata iwapo nafasi ya Rais na nafasi ya Makamu wa Rais ziinaweza kuwa wazi kwa
pamoja kwa wakati mmoja kwa mujibu wa Katiba (jambo ambalo ni nadra sana
kutokea ingawa linaweza kutokea) basi Katiba iweke wazi kwamba Jaji Mkuu au
Spika wa Bunge atashika madaraka ya Rais katika kipindi hicho cha mpito na si
Makamu pili au Makamu tatu ambao huenda wakawa wanatoka vyama tofauti na chama
cha Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais walioacha nafasi zao wazi ili kuondoa
utata huo. Hii ni kwa sababu ridhaa ya wapiga kura ni kwa hao watakaokuwa
wameacha nafasi.
Mapendekezo
namba 4-6 yatatupa wepesi sana ikiwa tutaka kuunda serikali ya umoja wa kitaifa
iliyo imara kwa maslahi ya Tanzania pale serikali zetu mbili zikuwa zikiongozwa
na marais kutoka vyama tofauti vya siasa.
Hitimisho
Nitumie
fursa hii kutoa angalizo kwamba ukipima uzito wa sababu za kuwa na nchi tatu na
serikali moja/tatu na faida zake na hasara zake au muungano wa mkataba
ukalinganisha muundo wa nchi moja na serikali mbili na faida zake na hasara
zake unaona kwamba Muungano wa nchi moja serikali mbili unafaa na ni
endelevu kisheria na kisiasa.
Nimalizie kwa
kulikumbusha tena Bunge la Katiba umuhimu wa kufuata misingi ya kuheshimiana,
kusikilizana, kustahimiliana na adabu na kuepuka matusi na kutunishiana misuli
katika kuijadili Rasimu ya Katiba. Kinyume chake mtapitisha Katiba mbovu
inayotoa leseni ya kuuwa Muungano. Na wananchi wataikataa. Endelezeni umakini
wenu wa kujadili kila kipengele kwa kina na msikubali kushinikizwa na yeyote
yule. Fanyeni kazi hii kwa maslahi ya Tanzania na watanzania.
Panapo uhai na
uzima nitaandika kuhusu Rasimu ya Katiba kuuzika Ujamaa na athari zake kwa
Tanzania, Uraia wa Nchi mbili na athari zake, na upotoshaji kuhusu maendeleo ya
Tanzania ikilinganishwa na Malaysia au Korea.
Nakutakieni
kila lenye kheri katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano wetu.
Mungu Ibariki
Tanzania
Dumisha Uhuru
na Umoja
Dumisha
Muungano wa Tanzania
Ndugu yenu
Dkt Amani
Millanga
06/04/2014
London
"No Choice, No Sacrifice; No Sacrifice, No Access;
No Access, No Success.The Choice Should be Guided by the 6Cs of a Good
Character: Conscience, Compassion, Consideration, Courage, Control &
Confidence."by Amani Millanga
NAAMINI KUWA
NAFSI IKITAWALIWA NA TAMAA HATA KAMA INA ELIMU KUBWA NA UTAJIRI KIASI
GANI, ELIMU NA UTAJIRI HUO HAVIFANYI KAZI KWA MANUFAA YA WATU.