NASAHA ZA NYERERE UGHAIBUNI
Katiba mpya, Nyerere
anapotumika kuwakwamua majirani wakati
sisi tumekwama!
Na Prudence Karugendo
NAPENDA misemo ya wahenga kwa vile mara zote huonekana imelenga mbali. Wahenga wa Kihaya walisema
kwamba “ente ya ahai telya bunyasi bwaho”. Maana ya usemi huo ni kwamba ng’ombe
hali nyasi zilizo karibu na anakoishi. Kawaida ng’ombe huwa anapelekwa mbali
kwa ajili ya malisho akiziacha nyasi zilizo karibu na anakoishi zije kuliwa na ng’ombe wengine
kutoka mbali na hapo.
Hebu tuuangalie mfano wa usemi huo wa wahenga wa Kihaya
ndani ya jamii yetu. Watanzania tumekuwa tukijivunia jina la Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere, hili ni jina la mtu ambaye kwa mapenzi yetu kwake na mapenzi
ambayo yeye mwenyewe alikuwa nayo kwa nchi yake na watu wake, tumeamua
kumtunukia hadhi ya Baba wa Taifa.
Busara na hekima za Nyerere katika kutetea usawa na usahihi
wa kila jambo ziliwafanya watu wa mataifa ya mbali kutamani kwamba bora mtu
huyo angekuwa anatoka katika mataifa yao.
Mfano, Rais Joachim Chisano wa Msumbiji, wakati wa kuuaga mwili wa Mwalimu pale
Uwanja wa Taifa, kwa majonzi makubwa alitamka kwamba “Watanzania na wananchi wa
Msumbiji sote tunalia kwa sababu Baba wa Taifa wa Tanzania ni Baba wa Taifa wa
Msumbiji”.
Kauli hiyo ya Chisano ilikuwa na maana ndefu zaidi ya ilivyofikiriwa
kuwa pengine ililenga katika urafiki na udugu kati ya Tanzania na Msumbiji. Hiyo ni
kutokana na kwamba Chisano alitamka na tukamsikia tukiwa tumemuelewa katika
mazoea ya urafiki na udugu wa nchi hizi mbili. Lakini kuna watu ambao
hawakuwahi kulitamka hilo pamoja na kwamba
walilitamani sana,
au wengine walitamka na hatukulisikia kutokana na kutokuwa nao karibu.
Katika gazeti moja la nchini Marekani iliwahi kuandikwa
tahariri kwamba Nyerere alipaswa kuzaliwa katika nchi kama Marekani lakini bahati
mbaya akazaliwa Tanzania!
Hiyo yote ni katika kuonyesha thamani aliyokuwa nayo kiongozi huyo muasisi wa
taifa letu, thamani ambayo sisi Watanzania naona tunashindwa kuifanyia kazi
zaidi ya kubaki tunaimba tu “Baba wa Taifa Baba wa Taifa” huku tukifanya mambo
yasiyo na uwiano hata kidogo na thamani ya jina la mtu huyo tunayemtumia
kuringa kuwa ni Baba wa Taifa bila jitihada zozote za kuhakikisha tunanufaika
na uadhimu wake.
Wahaya wanasema “ente ya ahai telya bunyasi bwaho”. Wakati
Watanzania tunashindwa kulitumia jina la muasisi huyo wa taifa letu kujikwamua
katika mambo mbalimbali walau hata kujaribu kuzitumia nasaha zake kutatua
baadhi ya mambo yanayotuelemea, wenzetu wa nje wanazitumia sanaha zake kupata
ufumbuzi wa matatizo yao.
Kwa sasa nchini mwetu kuna mahitaji ya Katiba mpya. Haya ni
mahitaji yanayoonekana hata kwa kipofu. Mambo yetu yanaenda ndivyo sivyo huku
baadhi ya watu, hususan waliomo katika mfumo wetu wa utawala, wakijinufaisha na
katiba iliyopitwa na wakati. Katiba iliyoandikwa wakati wa udikteta wa chama
kimoja cha siasa, lakini inaendelea
kufanya kazi hata wakati ambapo
tunajidai tumo kwenye demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa!
Nchi nyingi katika bara letu, hususan katika ukanda wetu huu
wa Afrika Mashariki, zimepitia katika udikteta wa chama kimoja cha siasa ingawa
karibu zote kwa sasa zimo katika kinachoitwa mfumo wa kidemokrasia ya vyama
vingi vya siasa. Nasema hivyo kutokana na mfumo huo kutopewa nafasi ya kufanya
kazi ipasavyo. Kama
tunavyoelewa mfumo huu umekuja kwa shinikizo wakati watawala wengi walikuwa
bado hawajajiweka sawa kuupokea. Zipo sababu zilizokuwa zinawafanya
watawala wasiufurahie mfumo huo wa
kidemokrasia na hivyo kulazimika kuupokea shingo upande, mfumo ukarasmishwa
kimaneno huku katiba za nchi zikiendelea kubaki zilezile zinazotambua udikteta
wa chama kimoja cha siasa. Kimaneno Katiba inasema vyama vingi vya siasa lakini
kimatendo ni kama Katiba inavilaani vyama
hivyo na kubaki inakitambua chama kimoja pekee kilichohusika kuiandika.
Nchi nyingi zimepigana kufa na kupona kuhakikisha katiba za
nchi hizo zinabadilika kulingana na matakwa ya wakati. Moja ya nchi ambazo
zimefanikiwa kuandika katiba mpya, siyo kubadili kwa kuchomeka viraka kama
ilivyo hapa kwetu, ni Kenya.
Zilifanyika kampeni za kuwaelimisha wananchi wa Kenya juu ya mahitaji ya kuandika katiba mpya nchini
mwao. Wapo waliokuwa wanaona katiba yao
ya zamani inafaa kwa wakati huu na hivyo
kutoona umuhimu wa kuandika katiba nyingine. Kwa maana hiyo ikabidi ifanyike
kura ya maoni kuona ni upande upi unakuwa na nguvu kati ya ule unaoona umuhimu
wa kuandika katiba mpya na ule unaosema iendelee ileile ya zamani.
Ni katika kampeni hizo za kuwashawishi wananchi kukubali
kuandikwa kwa katiba mpya ambapo kulijitokeza kitu ambacho ndilo lengo langu la
makala hii. Katika sehemu maarufu kwa mikusanyiko ya hadhara, Uhuru Park,
Jijini Nairobi, Makamu wa Rais wa sasa, Kalonzo Musyoka, katika jitihada
zake za kuinadi katiba mpya alitumia nasaha za Baba wa Taifa la Tanzania,
Mwalimu Julius K. Nyerere, kuwashawishi Wakenya kukubali kuandikwa kwa katiba
mpya ya nchi yao
na Wakenya wakamuelewa bila tatizo lolote.
Kalonzo Musyoka aliwauliza wananchi waliokuwa wanasikiliza
kampeni hizo, kama walikuwa wanamkumbuka
Mwalimu Julius Nyerere, wote wakasema
wanamkumbuka, akawauliza tena ni nani? Kwa pamoja wananchi wakasema Baba wa
Taifa wa Tanzania.
Akasema sawa, yule alikuwa ni mwalimu, akasema Mwalimu Nyerere aliwahi
kufundisha juu ya katiba ya nchi, maana yake na umuhimu wake kulingana na
wakati inapohitajika.
Kusema ukweli, nikiri kwamba somo alilokuwa analiongelea
Kalonzo Musyoka kutoka kwa Nyerere nilikuwa sijawahi kulisikia. Musyoka
akawaeleza wananchi kuwa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba katiba ya nchi
ni kama mtoto. Mtoto anapozaliwa anafurahiwa
na wazazi wake, wanamnunulia nguo za utotoni. Lakini kadri mtoto anavyokua ni
lazima wazazi waendelee kumnunulia mtoto nguo nyingine kwa vile zile za awali
atakuwa tayari kaishazizidi. Kwahiyo eti wazazi wanaompenda mtoto wao hawawezi
kuzing’ang’ania zile nguo za uchanga za mtoto wao kuwa ndizo zinazomfaa bila
kununua nyingine. Kwahiyo kwa nasaha hizo za Mwalimu Kalonzo Musyoka akawa
amewashawishi Wakenya kuunga mkono kuandikwa kwa katiba mpya. Wakenya wakawa
wamenufaika na nasaha za Baba wa Taifa wa Tanzania.
Wakati Kenya
wanafurahia Katiba mpya ya nchi yao
waliyoizindua kwa mbwembwe kana kwamba ndipo wanapata uhuru wao, sisi Tanzania
bado tunaendelea kuing’ang’ania katiba iliyochakaa ikiwa imepachikwa viraka
kila sehemu. Tunapaswa tujiulize, Watanzania tuna tatizo gani? Ina maana Kenya
wanatuzidi akili kwa kiasi hicho cha
kutamani kitu kipya wakati sisi tunaona kilichochakaa ndicho kinachotufaa?
Inawezekana Kenya
nako walikuwepo ving’ang’anizi ambao walikuwa hawapendi mabadiliko ya
katiba yao, lakini wakaja kulainishwa na nasaha za Baba wa taifa
wa Tanzania, sasa inakuwaje
ving’ang’anizi wa Tanzania
washindwe kulainishwa na nasaha za Baba wa Taifa lao ambazo alikuwa
anazitoa
kila kukicha mpaka mwisho wa uhai wake? Hapa ndipo ninapokubaliana na
wahenga
wa Kihaya kuwa “ente ya ahai telya bunyasi bwaho”, ng’ombe hali nyasi za karibu na anakoishi.
Yapo mambo mengi ambayo Mwalimu alikuwa anatuhasa
kutoyafuata ili kulinda maadili yetu na heshima yetu. Lakini mambo hayo kwa
sasa ama yanafuatwa au kukiukwa kulingana na mahitaji ya kila kundi katika
jamii yetu. Cha ajabu hata yaliyo machafu yanaweza yakafanyika kwa madai ya
kwamba wakati uliopo unakinzana na wakati ule ambao baadhi ya mambo
yaliharamishwa. Lakini linapokuja suala la katiba ya nchi wakati ule wa zamani
ilipoandikwa katiba tuliyo nayo unakuwa sawasawa kabisa na wakati tulionao kwa
sasa! Ndipo yanapojitokeza madai ya kwamba kwani katiba tuliyo nayo ina
matatizo gani?
Tuliona jinsi Azimio la Arusha, kwa mfano, azimio ambalo
Mwalimu amekufa nalo mfukoni mwake akiamini kwamba ni azimio la utu,
lilivyozikwa kirahisi kule Zanzibar.
Hapakuwepo na kura ya maoni au kuwashawishi wananchi kwa namna yoyote kulikataa
azimio hilo
kwanza ndipo yafanyike mabadiliko.
Viongozi peke yao walikaa Zanzibar
na kuamua kulifuta kinyemela baada ya
kuona linakinzana na maslahi yao.
Kwahiyo kitu ambacho kinakinzana na maslahi ya viongozi,
hata kama kwa wananchi ni muhimu na kizuri
kiasi gani, ni rahisi kubadilishwa. Lakini kitu ambacho ni muhimu kwa wananchi
na kwa mustakabali wa nchi, kama kinaonekana
hakitaleta manufaa kwa watawala kinakuwa kigumu kubadilika. Kitaendelea
kuchomekwa viraka kulingana na matakwa ya watawala mpaka wakati usioeleweka.
Lengo langu katika makala hii ni kuonyesha jinsi Watanzania
tunavyoshindwa kujinufaisha na mambo tuliyojaaliwa kuwa nayo zikiwemo nasaha za
Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kama ilivyo kwa raslimali zote
tulizo nazo ambazo zinawanufaisha watu wa nje, hata nasaha za Mwalimu
zinaonekana kuwanufaisha wageni sisi tukibaki tumetumbua macho kama viziwi. Haya, Kenya
wameandika katiba mpya wakizitumia nasaha za Mwalimu kama
mwongozo wa kufikia mafanikio hayo, sisi tunalia na katiba iliyojaa viraka.
Tunashindwa kuzitumia nasaha za Mwalimu kupata katiba mpya wakati Mwalimu
alikuwa ni wetu na Baba wa Taifa!
Hata kama nchi yetu si ya kishirikina lakini kwa hili ni
lazima tumtafute mchawi, maana hii si bure. Wenzetu kunufaika kwa kitu ambacho
sisi tumekikalia huku pengine tukihitaji msaada kwao utakaotoka na kitu
kilekile tulichokikalia si jambo la kawaida. Kama
ni usingizi basi huu umepita kiasi, tusipojihimu si ajabu tukapitiliza na huo
kuwa mwisho wetu.
0784 989 512