Bukobawadau

KAULI YA KOMBA KWENDA MSITUNI:Mchelea mwana kulia hulia mwenyewe!

Na Prudence Karugendo
NIANZE  kwa kutaja maslahi yangu kwamba mimi nilikuwa mpenzi mkubwa wa Kapteni John komba. Nyimbo zake, hasa zile za mwanzo akiwa kiongozi wa kikundi cha kwaya cha JWTZ cha Lugalo, zilikuwa zinanikosha roho kupita kiasi na kunifanya nizione rangi zote za utukufu wa nchi yangu, huku yeye nikiwa nimemweka katika daraja la kwanza la wazalendo wa nchi hii.
 Lakini Waswahili walisema kwamba “kua uyaone”! Niliyedhani kwamba yuko kwenye kundi namba moja la wazalendo wa nchi yangu leo hii anatishia kuwa wakati wowote anaweza akawa adui namba moja wa nchi hii iwapo matakwa yake hayatazingatiwa! Anaamini kwamba yeye ndiye mzalendo peke yake, wengine wote wahamiaji sijui!
Komba katamka kwenye Bunge Maalumu la Katiba kwamba iwapo maoni ya wananchi ya muundo wa serikali tatu katika Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, yatayazidi nguvu matakwa ya chama chake kinachopendelea muundo wa ajabu wa serikali mbili, basi yeye ataongoza njia kwenda msituni!
Sidhani kama Komba anatamani kwenda msituni  ili akaishi na ngedere baada ya kuwachoka binadamu wenye mawazo tofauti na ya kwake, hapana, ni lazima huo ni mpango wake wa kuanzisha vurugu zenye lengo la kuwakomoa na kuwakomesha wananchi wasiokubaliana na mtazamo wake. Hiyo maana yake ni vita na mauaji ya wananchi.
Mpaka hapo, kwangu mimi, uzalendo wa Komba umeyoyoma kwa kasi kubwa. Hayo ndiyo yaliyosemwa kwenye usemi wa wahenga wa kua uyaone.
Mzalendo wa kweli ni yule aliye tayari kuilinda nchi yake pamoja na wananchi wenzake. Wawe wamehitilafiana au kukosana undugu unabaki palepale, kulindana na kuwekeana kinga dhidi ya mabaya toka nje yao.
Lakini anayetamani kuingia msituni ili akawadhuru wananchi  wenzake eti kwa vile wametofautiana na mawazo yake, siwezi kuamini kwamba anao uzalendo wa aina yoyote. Uzalendo kwa lipi?
Sababu nchi ni ya wananchi wote. Uzalendo unatakiwa uyaheshimu matakwa ya wananchi walio wengi. Uko ndiko kuilinda nchi na watu wake, ikiwa ni pamoja na kuyalinda matakwa yao. Vinginevyo uzalendo hakuna.
Kauli hiyo ya hatari ya Komba haikukemewa na yeyote kwa upande wa chama chake, CCM, imechukuliwa tu kama kauli ya kuwakomoa wapinzani na yeye kubaki akionekana ni kipenzi kwa chama chake hicho!
Kauli hiyo ya Komba imenikumbusha jinsi Ossama bin Laden alivyokuwa kipenzi mkubwa wa Marekani pale nchi hiyo ilipokuwa ikimtumia kuyalinda maslahi yake na kuwakomoa wale ambao haikuwataka.
Lakini baada ya Bin Laden kuhitilafiana na Marekani akageuka adui namba moja wa nchi hiyo. Ikabidi nchi hiyo itumie gharama kubwa sana,  tena kwa muda mrefu, kumtafuta na kumuangamiza mtu huyo, huku yenyewe ikiwa imebaki na majeraha makubwa ambayo haitakaa iyasahau. Mchelea mwana kulia hulia mwenyewe.
Komba hakuchukuliwa hatua wala kukemewa kwa aina yoyote na walio madarakani, hususan chama chake cha CCM, kwa tamko lake hilo la hatari. Ni kwa sababu tamko lake hilo kwa sasa linaonekana halina madhara kwao, ila limelenga kuwatisha na kuwanyamazisha wapinzani wanaotamani kuiona nchi yao ikipita mwenye mstari ulionyooka.
Isipokuwa kauli hiyo ingekuwa mbaya sana kama ingekuwa imetolewa na mtu wa upande wa upinzani. Lazima kwa sasa hivi mtu huyo angekuwa anaijutia kauli hiyo.
Kwa uzoefu tulio nao kwa sasa, hasa kwa upande wa Bara letu la Afrika, Watanzania hatukupaswa kuichukulia kauli hiyo ya Komba kiurahisi na kuipuuza kiasi hicho. Sababu anacholenga kwenda kukifanya kule msituni hakitambui nani yuko upande wake, nani yuko upande wa pili na ni nani hahusiki. Ni machafuko kwa kwenda mbele, sababu ilishasemwa kwamba vita haina macho.
Nchini Uganda, kwa mfano, alijitokeza mama mmoja, Alice Auma Lakwena, akadai kwamba anataka kuendesha nchi kwa kufuata Amri Kumi za Mungu. Akapuuzwa. Sikujua alikoishia. Lakini akaja kurithiwa na Joseph Kony ambaye naye mwanzoni alionekana kupuuzwa na serikali ya Uganda.
Baada ya Kony kuanza kutoa cheche ndipo serikali ya Rais Museven ilipoanza kuhangaika ikitafuta kumdhibiti bila mafanikio. Wakati huo Kony na kikundi chake wakizidisha madhara kwa nchi na maafa kwa wananchi.
Tuseme kikundi hicho kilikuwa na ugomvi na serikali, lakini waliodhurika zaidi ni wananchi. Wananchi ndio wanaovamiwa na hao walio msituni,  kutekwa na kuuawa wakati serikali ya Rais Museven ikiwa bado iko palepale.
Inavyoonekana lengo la kikundi hicho cha Kony ni kuwaua wananchi na wala sio kuiondoa serikali ya Museven madarakani.
Nakumbuka kuna wakati Museven aliwahi kumuahidi mwanahabari mmoja wa Uganda, aliyeuliza swali juu ya Kony, shilingi milioni sita za Kiganda endapo Kony angefika wakati fulani kabla hajauawa na serikali, zaidi ya miaka kumi iliyopita. Museven alitimiza ahadi yake, maana mpaka sasa Kony bado “anadunda”.
Kosa kubwa lililofanywa na serikali ya Uganda ni la kushindwa kumdhibiti Kony mapema, kwa kumchukulia kwamba yeye na kundi lake ni watu wepesi ambao wangemalizwa mapema bila madhara yoyote.
Ninapoyaangalia hayo ndipo nashawishika kuilaani tena na tena kauli ya Komba ya kwamba ataenda msituni iwapo matakwa ya chama chake ya muundo wa serikali mbili hayatakubaliwa.
Najiuliza kwa mshangao, kama maoni ya wananchi yanasema muundo wa muungano wa nchi yetu uwe wa serikali tatu, hizo serikali mbili zinazotaka kumpeleka Komba msituni ni kwa manufaa ya nani?
Kwa nini Komba atamani kuingia msituni kwa lengo la kuziteketeza roho za wananchi wenzake kisa eti anataka serikali mbili dhidi ya matakwa ya wananchi? Serikali mbili bila wananchi zina maana gani?
Imeishasemwa mara kadhaa kwamba Katiba ni maridhiano, bila hivyo Katiba itabaki kuwa kielelezo cha manyanyaso. Kwa nini Komba anaona maridhiano hayafai na hivyo apange kukifanikisha anachokitamani kupitia msituni?
Nakumbuka Mwalimu Nyerere aliwahi kukusudia kuwashitaki wakoloni kwa Mungu, iwapo njia zote za kuwataka watuachie uhuru wetu zingeshindikana. Baadaye alifafanua kwamba kuwashitaki kwa Mungu alikokusema kulimaanisha kushika silaha na kuudai uhuru wetu kwa nguvu, uhuru wa wananchi wote.
Sasa anayetaka kuingia msituni baada ya maoni ya wananchi walio wengi kupingana na matakwa yake anataka afanye hivyo kwa faida ya nani? Bilashaka kama sio kwa maslahi ya kikundi kidogo anachokipenda yeye ni kwa maslahi yake binafsi. Ndiyo maana nasema kwamba tunatakiwa kumlaani Komba kwa nguvu zote kwa mpango wake huo mchafu.
Kwa nini Komba asichukuliwe hatua kwa wakati huu na kudhibitiwa kabla hajaamua kukifanya anachokikusudia kama alivyotamka yeye mwenyewe? Naamini kwamba gharama ya kumdhibiti kwa sasa ni ndogo na nyepesi kuliko kumsubiri akaingia msituni.
Tukiichezea kauli yake kwa kujiridhisha kwamba aliyoyasema ni maneno tu, na hivyo kumwachia ili kwanza ayaweke maneno yake kwenye vitendo, inabidi tuelewe kwamba tutakuwa tumeviweka rehani, nchi yetu na roho zetu.
Sababu ikishakuwa hivyo gharama ya kumpata itakuwa kubwa sana kiasi ambacho pengine hatutakiweza, muda wa mateso utakuwa mkubwa sana wakati thamani ya roho za wananchi itakuwa imeshuka kukaribia na sifuri. Maana kwenye hali hiyo mtu kuuawa haina tofauti na mjusi kuuawa.
Waswahili wanasema kwamba asiyejua kufa muonyeshe kaburi. Nataka niwaonyeshe Watanzania wenzangu waiangalie Nigeria ilivyo kwa sasa. Mohammed Yusufu, aliyekuwa kiongozi wa kikundi cha kijambazi cha Boko Haram kule Bauchi, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria, kabla ya kuuawa na kurithiwa na Abubakari Shekahu, alitamka maneno kama ya Komba.
Wanigeria kwa mbwembwe zao wakadharau wakimuona si lolote si chochote.Lakini sasa hivi walikofikia wanaichukulia Boko Haram kama kiama! Wapende wasipende wanaiheshimu.
Tumeona jinsi Jeshi la Nigeria lilivyoshindwa kukidhibiti kikundi hicho ambacho mwanzoni kilidhaniwa ni “tisha toto” tu. Sasa imebidi Marekani, Uingereza na Israeli waingilie kati kujaribu kukisaka kikundi hicho.
Jambo la kusikitisha zaidi ni kwamba wanaoathirika sana na unyama wa kikundi hicho ni wananchi wasio na hatia yoyote, wananchi wasiojua wafanye nini ili kutuliza mzuka wa majambazi hayo ya Boko Haram.
Kwa sasa dunia nzima, kila mtu anamuomba Mungu kivyake ili watoto wa kike zaidi ya 200 waliotekwa na kikundi hicho toka shuleni kwao wapatikane wakiwa salama.
Tujiulize, mabinti hao wamekifanyia kosa gani kikundi hicho? Kwani wao ndio serikali ambayo kikundi hicho kinadai kuna mambo ambayo hakikubaliani nayo. Bilashaka hapana.
Hapo ndipo tunapaswa tuelewe kwamba wazo la kuingia msituni linasukumwa zaidi na “umimi”, mtu kujifikiria yeye binafsi bila kuyajari mahangaiko yanayowapata wengine wala kujali zahama atakazowasababishia. Kwa ufupi huo ndio unaoitwa ujambazi.
Jambazi anajali yeye kupata, hajali kwamba anachotaka kukipata ni cha mwingine na anataka akipate kwa mabavu hata kufikia kuitoa roho ya yule anayekimiliki kihalali!
Laiti serikali ya Nigeria ingeliona hilo mapema na kumkamata kiongozi wa kikundi hicho, marehemu, mwanzoni kabisa kabla hajaanza kuyatekeleza aliyokuwa anayakusudia, maafa yote haya yanayoikumba nchi hiyo yasingekuwepo. Haya sasa ni matokeo ya kuudharau mwiba ambapo sasa guu lote limevimba tende!
Hakuna mtu mwenye kuitakia mema nchi yake, akiipenda na kuwapenda watu wake, halafu akatamani kuifanyia uasi au ugaidi nchi ileile.
Ndiyo maana wapinzani hapa nchini wanafanyiwa vituko vya kila aina, kunyanyaswa, kuonewa, kutukanwa, kudhulumiwa nakadhalika, lakini hakuna mpinzani aliyewahi kuwa na wazo kama la Komba. Ni kwa sababu wanaoitwa wapinzani wanaipenda nchi yao. Iweje sasa tuseme Komba anaipenda nchi yake kwa wazo lake hilo la kutaka kuiangamiza?
Nimalizie kwa kusema kwamba tunapaswa tuilaani kwa pamoja kauli ya John Komba ya kwamba ataenda msituni, na tuiombe serikali yetu imshughulikie kwa kuwa hiyo ni kauli ya kijambazi. Sababu mchelea mwana kulia hulia mwenyewe. Tusiwe kama Nigeria inayolia kwa sasa.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau