Bukobawadau

MBUNGE AOMBA KURA KATIKA MAAFA MULEBA

Na Ashura Jumapili | Kagera
ATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), ametoa mpya kwa kuomba kura za ubunge 2015 kwa wananchi waliopigwa na kimbunga kwenye Kijiji cha Bulembo.

Vile vile, Mwijage ameshambulia vyombo vya habari na kutaka vyombo vya dola viwatie mbaroni waandishi waliopiga picha za maafa yaliyokikumba kijiji hicho na kuziweka kwenye mitandao na magazeti.

Akihutubia wanakijiji hao Jumanne wiki hii katika viwanja vya Shule ya Msingi Rugongo iliyo kijijini hapo, Mwijage alisema picha hizo zimemtia aibu kwa watu wanaomheshimu, kwani zimeonyesha nyumba mbovu mbovu zilizobomolewa na kimbunga, na kuwafanya wanakijiji wa Bulembo waonekane ni watu masikini.

Mwijage, ambaye hakuonekana kijijini hapo kwa zaidi ya siku 30 tangu wanakijiji hao walipopigwa na kimbunga hicho, alimshutumu hadharani Ansbert Ngurumo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vox Media, ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Free Media, aliyechapisha makala na picha ya Yasinta Godfrey, na kuwaombea msaada kwa serikali na wasamaria wema kupitia safu ya Maswali Magumu Jumapili Aprili 13, mwaka huu.

Katika makala hiyo, Ngurumo aliitaka serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kitengo cha Maafa, kupeleka msaada Bulembo haraka ili kunusuru maisha ya wananchi hao.

Miongoni mwa waliokwishapeleka msaada Bulembo ni pamoja na Shirika la Kolping, Kanisa la Kilutheri, Parokia ya Rutabo, Halmashauri ya Wilaya Muleba na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera.

Watu binafsi waliopeleka misaada ni Mbunge wa Muleba Kusini, Prof. Anna Tibaijuka (kilo 1,250 za maharage), Mbunge wa Viti Maalumu CHADEMA, Conchesta Rwamulaza (kilo 1,100 za mchele) na Ngurumo mwenyewe (kilo 1,100 za mchele).

Mwijage, ambaye amefika eneo la tukio baada ya siku 30 kupita akitoka bungeni Dodoma, hajapeleka msaada wowote, bali amefika kutangazia wananchi kwamba serikali itatoa msaada wa chakula siku chache zijazo.

Katika mkutano huo, alijitangaza kuwa yeye ni miongoni mwa wabunge matajiri, hivyo hawezi kupeleka kilo mbili mbili kama waliomtangulia.

Alitumia fursa hiyo kuomba kura za mwaka 2015 kwa maelezo kuwa yeye ni mpenda maendeleo.

Hata hivyo, kabla hajaondoka Bulembo alimuita Yasinta na kumkabidhi pesa taslimu sh 100,000 kama mchango wake.

Akizungumza na gazeti hili jana, Yasinta alishukuru wote waliomsaidia hadi sasa, hasa vyombo vya habari ambavyo vimesaidia kujulisha umma matatizo aliyonayo.

“Kwa namna ya pekee, namshukuru sana Ngurumo. Kupitia kwake nimepata msaada mkubwa, sasa hivi kuna mtu amejitolea kunipa makazi ya muda mimi na mtoto wangu. Hata mbunge amenijua baada ya magazeti kuandika,” alisema Yasinta.

Alipuuza kauli za mbunge kuwa picha hizo zimemdhalilisha yeye na mumewe. Hata baadhi ya wanakijiji waliokuwa kwenye mkutano wa hadhara wa Mwijage walisema walikerwa na tambo zake na matusi kwa watu ambao walinusuru maisha yao kwa misaada midogo midogo wakati yeye yuko bungeni.

“Hivi kama wasingejitokeza akina Ngurumo na Tibaijuka yeye angetukuta tuna hali gani? Na bado amekuja mikono mitupu, anatudanganya eti ndiye analeta msaada wa serikali, wakati tunasoma magazeti na tunajua kinachoendelea,” alisema mwananchi mmoja ambaye alikataa kutaja jina, kwa maelezo kuwa anaogopa visasi.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kama mbunge anajinasibu kwa utajiri, na anadharau wengine, alipaswa kuwa wa kwanza kutoa msaada kutoka mfukoni mwake, kama walivyofanya wengine.

Alisema wananchi wanajua kutofautisha mchango wa mbunge na msaada wa serikali.

Mwanakijiji mwingine, Pastory Steven, alisema mbunge amepewa dhamana na wananchi, na kwamba kitendo cha kuwabeza waliotoa misaada, kimempunguzia heshima, kwani misaada hiyo ndiyo imesaidia wananchi hadi akawakuta hawajafa kwa njaa, kwani yeye mwenyewe ameonekana jimboni baada ya mwezi mzima tangu walipopigwa na kimbunga.

Alisema anamshangaa mbunge kwa kushindwa kuthamini uhai wa wapigakura wake wakati wa shida, halafu akajitokeza kutukana watu, na kuomba kura katika mazingira ya maafa, na kabla hajapitishwa na chama chake, na kabla ya wakati wa kampeni.
Next Post Previous Post
Bukobawadau