Bukobawadau

BUNGE LETU NA DHARAU ISIYOPIMIKA

SIJAELEWA  kwa nini shughuli za Bunge letu zinaendelea kuonyeshwa moja kwa moja “live” kwenye luninga. Kuonyeshwa kwenye luninga ni kulivua Bunge letu ufaragha ambao pengine ungeendelea kuwapa wananchi imani na Bunge lao wakiamini kuwa wawakilishi wao wako kazini wakiyafanya waliyowatuma wayafanye.
Sipingani na teknolojia ya sasa,  wala kutaka wabunge wetu wafanye mambo kwa faragha kwa kuwaficha wananchi wanachokifanya mle Bungeni, hapana, nataka uwazi ila uwazi usiokuwa wa aibu. Nitajieleza.
Lengo la matangazo ya luninga, kwa teknolojia ya sasa, sio mbwembwe tu za kuonyesha kuwa na sisi tunaweza, isipokuwa kuonyesha kilicho cha kweli na kutafuta namna ya kukiboresha kwa maana ya kusonga mbele tukiwa imara zaidi.
Hivyo ndivyo tunavyoweza kujivunia aina hii ya teknolojia tukiwa tunaonyesha namna tunavyonufaika nayo. Siamini hata kidogo kama teknolojia hii inapaswa iwepo kama mapambo ya kuonyeshana mikogo isiyo na tija yoyote.
Lakini kwa sasa sikioni tunachoweza kusema kuwa tunajivunia katika teknolojia hii ya kuangalia shughuli za Bunge letu moja kwa moja kupitia kwenye luninga. Maana kwa sasa tunaishia kuliangalia Bunge na kuviona viroja ambavyo sidhani kama kuna mwanachi yeyote anayevifurahia. Kiroja kimojawapo kikubwa ni cha watazamaji wa shughuli za Bunge kuishia kuviona viti vitupu ndani ya ukumbi wa Bunge huku Bunge hilo likiwa linaendelea na shughuli zake bila kujali kwa mtindo wa bora liende.
Picha inayopatikana katika mazingira ya sasa ndani ya ukumbi wa Bunge ni kwamba viti ndivyo vinavyoendesha shughuli zote ndani ya ukumbi huo! Kwa sababu muda wote ndivyo vinavyoonekana vikiwa makini bila kuhama kwenda kokote.
Swali ni kwa nini kitu hiki tunaacha kiendelee bila kukikemea? Kama wabunge ni wawakilishi wetu tuliowachagua na kuwatuma kule wakafanye kazi ya uwakilishi, sababu haiwezekani Watanzania wote tukajazana mle kwa ajili ya kila mmoja wetu kukitaja anachokita katika uendeshaji wa nchi yetu, tena tukiwa tunawalipa pesa yetu nyingi kwa ajili ya kazi hiyo, kwa nini tunawaacha wajifanyie mambo kadri wanavyotaka wao?
Hii haina maana nyingine zaidi ya wabunge wetu kuonyesha dharau kwa wananchi waliowachagua na kuwaweka kwenye nafasi hizo adhimu ambazo wao, wabunge, wanapendelea wazitumie kuitana, au kuitwa na waliowachagua, waheshimiwa!
Kwa mtindo huo, najiuliza kwa nini wabunge wetu wanaipendelea sifa hiyo ya kuitwa waheshimiwa wakati wao wakionyesha mambo yasiyoendana na heshima wanayopewa?
Ieleweke kwamba heshima ya upande mmoja kamwe hainogi, heshima ni ya kuheshimiana, kuheshimiwa na kuheshimu,  hapo ndipo heshima inapokamilika. Ya upande mmoja siyo heshima ni vitisho. Kwa nini wabunge wetu hawalioni hilo?
Haiwezekani wabunge wetu wawaheshimu wananchi halafu waliache Bunge tupu huku vikao vikiendelea, tena wakijua kuwa wananchi wanaangalia, halafu waseme wanawaheshimu. Haiwezekani.
Mfanyakazi anayemheshimu mwajiri wake, kwa maana ya kuitaka kazi yake, hawezi kuonyesha utovu wa nidhamu wa kuiacha kazi na kufanya mambo mengine mbele ya bosi wake, vinginevyo huyo atakuwa haipendi kazi.
Wananchi wanaliheshimu Bunge lao na wabunge wao, hivyo ilipaswa wabunge nao waliheshimu Bunge na wananchi wanaowawakilisha. Kuwaheshimu wapiga kura wao wabunge wanapaswa wawe kwenye nafasi zao ili kuonyesha kuwa wanakitimiza walichotumwa kukifanya.
Hata wale wabunge wanaoteuliwa na rais, sidhani kama wanamtendea haki kuviacha wazi viti vyao kwenda kujifanyia mambo yao mengine nje ya Bunge. Hiyo siyo heshima kwa aliyewateua kuingia Bungeni, na ikizingatiwa mtu mwenyewe ni rais wa nchi. 
Kuwa katika nafasi zao hakuwalazimishi wabunge kuongea kama mtu hana la kuongea, kusinzia ni rukhsa, maana ilishasemwa kwamba wabunge kusinzia Bungeni si kosa ilmradi wasikorome. Lakini tuwaone kwenye nafasi zao.
Inaeleweka kuwa Bunge letu limevamiwa na wafanyabiashara, lazima tuwafanye watu hao waelewe kwamba Bunge ni mali ya wananchi. Hivyo anayejitoa kuwawakilisha wananchi katika chombo hicho anatakiwa awaheshimu wananchi kwa kukifanya kile alichowaahidi, uwakilishi, vinginevyo aachie ngazi. Maana Kristo alisema kuwa huwezi kuwatumikia mabwana wawili.
Sasahivi kila unakoenda nchini unawakuta wananchi wakikilalamikia kitendo cha Bunge lao kuendesha shughuli zake likiwa tupu. Wanajiuliza wabunge wao wanaenda wapi? Hiyo ni kwa sababu wanakiona moja kwa moja kinachoendelea mle ndani ya Bunge.
Ingekuwa wanasikiliza tu bila kuangalia bilashaka maswali hayo yasingekuwepo. Miaka ya nyuma ilikuwa hivyo, tulikuwa tunasikiliza tu kinachoendelea Bungeni kupitia kwenye redio. Lakini sasa tunaona na wabunge wenyewe wanaelewa kwamba wapiga kura wao wanakiona kinachoendelea.
Kwahiyo kitendo cha kuziacha wazi nafasi zao wakati vikao vya Bunge vinaendelea hakina maana nyingine  zaidi ya kuonyesha dharau kwa wananchi.
Mimi nahisi kwamba dharau hiyo inayoonyeshwa na wabunge wetu inatokana na ukweli wa kwamba wanaona wananchi hawana cha kuwafanya zaidi ya kubaki wakinung’unika na kushangaa kuwa Bunge lao linaendeshwa na viti badala ya wabunge, wakati waheshimiwa wakiwa wanajifanyia mambo yao mengine nje ya Bunge.
Laiti wananchi wangekuwa wamekolea elimu ya uraia kiasi cha kuwawajibisha wabunge watoro, sidhani kama mchezo huu wa kuvikacha vikao vya Bunge ungedumu.
Tofauti na Bunge letu, kila ninapoviangalia vikao vya mabunge ya wenzetu, kuanzia nchi za  Afrika Mashariki mpaka Ulaya na Marekani na hata Asia, naona jinsi wabunge walivyobanana katika kumbi za mabunge yao kwa shauku ya kutimiza uwakilishi wao.
Lakini kwetu sisi kinachotiliwa maanani ni uheshimiwa, ukiangalia Bungeni unawahesabu watu wawili watatu na upande mwingine ukumbi ukiwa mtupu.
Labda mahali panapoonekana pamejaa ni kwenye sehemu za wageni wanaokwenda kuangalia shughuli za Bunge, wakiishia kuwaona tu Spika, Naibu Spika au Wenyeviti wa Bunge, ambao sio kawaida yao kukwepa vikao.
Pamoja na kuyasema hayo, sinabudi kuwapongeza baadhi ya wabunge ambao ni nadra sana kuwaona hawapo kwenye nafasi zao Bungeni. Mheshimiwa Chritopher ole Sendeka si kawaida yake kutoroka vikao vya Bunge, pia wapo Mhe. John Mnyika, Tundu Lissu, Chritowaja Mtinda, Halima Mdee, Mchungaji Msigwa, Mchungaji Natse,  bila kumsahau Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Mhe. F. Mbowe. Nawapongeza sana.
Nimalizie kwa kusema kwamba, kama mambo ndiyo hayo ya kukwepa vikao vya Bunge,  tuna sababu gani ya kuendelea kuwa na wabunge? Kwa nini tusiachane nao ili tuendelee kuwakilishwa na wabunge wa Wingereza na Marekani wasiokwepa vikao vya Bunge? Maana wawakilishi hao wanatuwakilisha na sisi vilevile kwa misaada wanayoipitisha katika vikao vyao kuja kwetu.
Vinginevyo wabunge wetu wanapaswa kujirudi.

Na Prudence Karugendo 
prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau