Bukobawadau

NI SHIDAAA WANAFUNZI WAKOSA MASOMO HUKO RUSHENYE BUGORORA!!

Wananchi wakisafiri kwa mitumbwi kutoka kitongoji cha Lushenye kijiji Gaburanga,kata Kassambya kwenda kijiji Bugorora kata Bugorora kufuata huduma.
 Mmoja wa wazee wa kitongoji cha Lushenye anayekadiriwa kuwa na miaka zaidi ya 90 aliyejulikana kwa jina moja la Katabazi akieleza juu ya masahibu ya kitongoji chao
WANAFUNZI wanaosoma katika shule ya msingi Bugorora  iliyopo kijiji Bugorora,kata ya Bugorora wakitokea kitongoji cha Lushenye,kijiji Gaburanga kata ya Kassambya hawapati masomo yao inavyostahili kutokana na mazingira magumu ya kuvuka mto Kagera kwa mtumbwi kwenda
shuleni na kurejea makwao.

Kilio hicho kimetolewa hivi karibuni na baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Lushenye ambao eneo lao ni kama kisiwa kwani ili ufike makao makuu ya kijiji chao cha Gaburanga ambako kuna shule na huduma nyingine huna budi kutembea umbali wa km 18.
Hivyo,hulazimika wanafunzi kuvuka mto Kagera kwenda kwenye kijiji cha  Bugorora  kilicho ng’ambo  kufuata masomo.

 Kijana mdogo anayesoma shule ya msingi Bugorora akiwa amewavusha abiria kwa mtumbwi baada ya 'mtu mwenye zamu' kutoonekana kwenye shughuli hiyo.
 Mkazi mmoja wa kitongoji cha Lushenye,Athman Mutehilungu alisema mwishoni mwa wiki kuwa watoto wao wanapata adha kubwa kuvuka mto kila siku na kuwa sasa wanaambiwa kuwa mwakani watoto wa darasa la kwanza hawatasajiliwa shuleni hapo kwani eti si shule ya kijiji chao.

Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugorora,Yasini Mwanga akizungumzia suala hilo alisema ni kweli matakwa ya wazazi wa shule hiyo ni kutotaka kuwasajili watoto wa kitongoji hicho kutokana na matatizo mbalimbali wanayokumbana nayo.

Aliitaja mifano ya matatizo hayo kama utoro kwa wanafunzi hasa majira ya mvua na kuna wakati kiboko hutishia usalama wa mitumbwi hivyo wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo.Wanafunzi zaidi ya 30 huvuka mto kwenda shule hiyo.
Alisema mwaka uliopita ilimlazimu kupanda mtumbwi kwenda kuwatafuta baadhi ya wanafunzi waliokuwa darasa la saba wakati wa mchakato wa usajili kwa ajili ya mtihani wa kuhitimu darasa la saba.
Aidha alisema wazazi wanakerwa na tabia ya wazazi wenzao waLushenye kutohudhuria mikutano na kutoa michango iliyoidhinishwa na hivyo baadhi yao kutaka uongozi wa shule usiwasajili watoto kutoka kitongoji hicho.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Lushenye ,Hamza Sadiki amekiri kuwapo na ulegevu katika mahudhurio na michango ya shule lakini akasema hiyo inatokana na mazingira magumu ya kijiografia waliyo nayo na kuiomba halmashauri ya wilaya kuwajengea miundo mbinu muhimu.

Alisema kuwa wanakitongoji kwa kushirikiana na mwalimu mkuu wa shule ya msingi Bugorora wameanzisha darasa la awali,kitongojini hapo ili kuwanusuru watoto wadogo kuvuka mto.
Akizungumzia matatizo  ya wananchi hao diwani wa kata ya Kassambya Safura Banobi amekiri kuyafahamu matatizo yao kwa kuwa tangu uchaguzi mkuu uliopita amekwenda kitongojini hapo safari mbili kwa kuvuka mto kwa  mtumbwi na kukutana na wananchi.

Alisema kuwa tayari kilio chao kuhusu barabara ammekwisha kiwasilisha kwenye baraza la madiwani lakini tatizo ni ufinyu wa bajeti.Hata hivyo alionesha wasiwasi wa kujengwa miundombinu kwenye sehemu hiyo hasa shule na kliniki akisema sehemu hiyo ni ardhi chepechepe mno na
inayojaa maji sana nyakati za mvua.

Alisema Halmashauri ya wilaya iliwashauri uongozi wa kijiji Bugorora kuendelea kuwapa huduma zote zinazotolewa kwa wanakijiji kwa kuwa hawawezi kuhudumiwa na kijiji chao cha Gaburanga ambako ni mbali mno.
Diwani huyo alikuwa na matarajio kuwa kadri siku zinavyokwenda,basi siku moja huko mbeleni,na kutokana na ongezeko la watu basi kitongoji hicho kitajikuta kimepata huduma muhimu.

NA MUTAYOBA ARBOGAST,Missenyi
Next Post Previous Post
Bukobawadau