Bukobawadau

WANANCHI WACHARUKA MULEBA

Jeshi la Polisi mkoani Kagera linawashikilia watu 30 wakazi wa Wilaya ya Muleba kwa tuhuma za vurugu na uharibifu wa mali uliotokea wilayani humo, ikiwemo kuvunja chumba cha kuhifadhia maiti katika Kituo cha Afya Kaigara na kuchoma nyumba moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, George Mayunga, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa chanzo cha uharibifu huo ni kifo cha Asera Triphone (16) kilichotokea Juni 12, mwaka huu katika Hospitali ya Mount Meru mkoani Arusha.
Alisema kuwa baada ya kufariki kwa mtoto huyo, mwajiri wake, Valentina Maxmilian, alichukua jukumu la kusafirisha mwili wa marehemu kwenda kwa wazazi wake wilayani Muleba kwa ajili ya mazishi.
Alisema wakati mwili unafikishwa nyumbani kwa baba wa marehemu, Triphone Joseph, alikuwa na taarifa kuwa mwanae ameuawa kwa mateso, ikiwa ni pamoja na kuondolewa baadhi ya viungo vyake vya mwili, zikiwemo sehemu za siri.
Alisema wazazi hao walitoa taarifa kituo cha polisi wakiomba mwili wa marehemu upelekwe kituo cha afya cha Kaigara kwa ajili ya uchunguzi wa kidaktari ombi lililopingwa na polisi ambao walitaka mwili huo ukafanyiwe uchunguzi katika Hospitali ya Mkoa wa Kagera.
Alisema kutokana na msimamo wa polisi, kundi la wananchi lilihamasishwa na kuamua kubeba jeneza la marehemu kutoka Kijiji cha Bukono na kulipeleka Muleba kisha kulitelekeza barabarani, lakini mwili huo ulichukuliwa ukahifadhiwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo cha Kaigara ili kusubiri utaratibu wa kufanya uchunguzi.
Kwa mujibu wa kamanda, wazazi wa mtoto bado walikuwa wakishinikiza uchunguzi wa kidaktari ufanyike kubaini chanzo cha kifo cha binti yao.
Alisema kabla ya utafiti huo kufanyika, wananchi wakaamua kuvunja mlango wa chumba cha kuhifadhia maiti cha kituo hicho ambapo polisi waliingilia kati na kutumia nguvu kuwadhibiti.
Alisema wazazi wa marehemu walikubali kuchukua mwili wa mtoto wao kwa ajili ya taratibu za mazishi huko kijijini kwao Bukono na kuwa tayari wameshazika.
Aliongeza kuwa ilipofika usiku saa mbili, uhamasishaji uliendelea, likatoka kundi la watu na kwenda nyumbani kwa Veronica Maxmilian, mama wa mwajiri wa marehemu katika Kijiji cha Buyango, na kuchoma moto nyumba mbili.
Alisema hatua za kisheria zimechukuliwa kwa kuwakamata waliohusika na uvunjaji wa kituo cha afya, kutelekeza maiti barabarani na uchomaji wa nyumba mbili za familia ya mwajiri wa msichana huyo.
Alisema watu 30 wanashikiliwa kwa lengo la kuwahoji ili kuwabaini vinara wa vurugu hizo na kuwa ukamataji huo ulifanyika baada ya kupata taarifa mbalimbali zilizolifikia jeshi hilo.
Hata hivyo, alisema mwajiri wa marehemu anashikiliwa na jeshi hilo kwa ajili ya upelelezi wa kina ambao utafanyika hapa Kagera na mkoani Arusha pamoja na jirani wanaomzunguka.
Next Post Previous Post
Bukobawadau