Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AENDELEZA VITA YA KUTOKOMEZA UGONJWA WA UNYANJANO UNAOTISHIA KUANGAMIZA ZAO LA NDIZI

Vita dhidi ya ugonjwa wa migomba ujulikanao kama  unyanjano  imeingia katika hatua nyingine mkoani Kagera baada ya Mkuu wa Mkoa  kutangaza kuwa kipindi cha kutoa elimu, na wananchi kung’oa migomba iliyoathirika kwa hiari kimeisha Juni 30, 2014.
Katika kipindi cha kuanzia Januari  hadi  Juni 2014  Elimu ilitolewa bure kwa wananchi kuhusu kung’oa kwa hiari migomba iliyoshambuliwa na ugonjwa huo . Katika mkoa mzima maeneo yote yaliyokuwa yameathirika na  ugonjwa wa unyanjano umetokomezwa kwa asilimia 60 hadi sasa.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian  Massawe anasema asilimia 40 ya maeneo yaliyobaki na ungonjwa wa unyanjano  itamalizwa na operesheni ambayo inaanza rasmi Julai 1, 2014 kwa kuhusisha viongozi wa ngazi mbalimbali wa serikali na wananchi wenyewe.
 Akitoa ratiba ya utekelezaji wa operesheni hiyo Mkuu wa Mkoa alisema kuanzia wiki ya kwanza mpaka wiki ya nne mwezi Julai 2014 watendaji wa vijiji na vitongoji watapita kwenye maeneo yao kila shamba kung’oa migomba iliyoathirika kwa lazima kwa kila mkulima katika Wilaya husika.
Mwezi Agosti  2014 itakuwa zamu ya Madiwani kutembelea kata zao kuhakikisha ugonjwa huo umemalizika. Wiki ya kwanza na ya pili mwezi Agosti 2014 ni wiki ya Afisa Tarafa kutembelea eneo lake na wiki ya tatu na nne ni wataalam wa Halmashauri kukagua maeneo yao kama ugonjwa umekoma .
Aidha katika mwezi Octoba 2014 wiki ya kwanza na ya pili Wakuu wa Wilaya na Wabunge watahusika katika kukagua mashamba ya wakulima na kuhakikisha hakuna ugonjwa wa unyanjano.
Mkuu wa Mkoa na Kamati yake ya Ulinzi na Usalaama  atazunguka mkoa mzima katika wiki ya tatu na nne mwezi Octoba kuhakikisha kuwa ugonjwa wa unyanjano umekoma katika mkoa wa Kagera na unakuwa historia.
Operesheni hiyo itaambatana na utekelezaji wa sheria ndogo za serikali za Mitaa kwa wananchi ambao wamekaidi kung’oa migomba iliyoathirika katika mashamba .  Sheria hizo ni pamoja na kifungo cha miezi sita jela au faini ya shilingi 100,000/= (laki moja) au vyote kwa pamoja.
Aidha Mkuu wa mkoa ametoa maagizo kwa Wilaya zote kuunda vikosi kazi vya kutekeleza operesheni hiyo. Pili watendaji wote watakaohusika na operesheni hiyo kutoa taarifa kila mara zoezi hilo litakavyokuwa linaendelea kutekelezwa, na tathmini itafanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba 2014.
Kwa wazee  na wasiojiweza hawatatozwa faini  bali vikosi kazi vitang’oa migomba iliyoathirika bure kwasababu ni makundi maalum. Pia msaada wa chakula kwa kaya ambazo zitakuwa zimeathirika kwa kiasi kikubwa kitatolewa kwani serikali tayari imetenga tani 200,000 za chakula kwa mkoa wa Kagera.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI

RS-KAGERA@2014
Next Post Previous Post
Bukobawadau