Bukobawadau

KWA NINI UKAWA NA SI TANZANIA KWANZA?

NA PRUDENCE KARUGENDO
 
WAKATI  mchakato wa Katiba Mpya ukiendelea na safari yake kupitia kwenye vikwazo vinavyowekwa makusudi na wenye hila, ambao hatahivyo hawawezi kufafanua sababu za kufanya hivyo wakaeleweka, wapo wananchi wanaojiuliza maswali mbalimbali kuhusu yanayojiri katika mchakato huu.
 
Kuna watu wanajiuliza nini maana ya makundi mawili, Ukawa na Tanzania Kwanza, yaliyojitokeza ndani ya Bunge Maalumu la Katiba huku kila moja likidai ndilo linaloujali sana musitakabali wa nchi yetu.
 
Kwa leo, kama nilivyoshauriwa sana na baadhi ya wasomaji wangu, nimeona bora nijaribu kuyatazama makundi haya mawili, Ukawa na Tanzania Kwanza.
 
Nianze na UKAWA; Kama jina linavyojieleza lenyewe, Umoja wa Katiba ya Wananchi, naweza kusema umoja huo umekuwepo nchini kwa muda mrefu hata kama ulikuwa haujajitambulisha hivyo. Msukumo na shinikizo la kuitaka Katiba Mpya ya nchi yetu havijaanza wakati huu, na shikizo hilo hatuwezi kulipambanua na hiki kinachojionyesha kama Ukawa kwa sasa,  kwa vile kinachopiganiwa ni kilekile kilichokuwa kikidaiwa miaka nendarudi, Katiba bora ya wananchi iliyotokana na matakwa yao.
 
Kwahiyo mpaka Rais Kikwete kuiona mantiki ya madai hayo na kukubali kuanzisha Mchakato wa Katiba Mpya ni wazi kwamba alikuwa amekubaliana na mtazamo wa Ukawa. Wasioliona hilo ni lazima wana lao jambo.
 
Kwahiyo baada ya kujitokeza sintofahamu ndani ya Bunge Maalumu la Katiba, ambapo baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo wanaonekana wazi kutanguliza maslahi binafsi, hasa posho zinazoonekana ni za kufuru, bila kujali hatma ya nchi yao na wananchi wenzao itakuwaje, wakitaka maoni ya wananchi yaliyorasimishwa ili itengenezwe Katiba bora yachakachuliwe kusudi ipatikane Katiba inayokithi maslahi ya baadhi ya wananchi, hususan vigogo, pasipo kuwajali walalahoi, ndipo watetezi wa kweli wa Katiba ya nchi wakaona ni bora waunde umoja wao ndani ya Bunge Maalumu na kujiita UKAWA.
 
Lengo la Ukawa ni kujitofautisha na wajumbe wengine waliomo kwenye Bunge hilo, ili wananchi wasije wakachukulia kwamba wote waliomo ndani ya Bunge hilo ni “Maziganyanza”, kama alivyowahi kusema Baba wa Taifa, MwalimuNyerere,  akiwa na maana ya wote ndio hao, wasaka maslahi binafsi.
 
Ikumbukwe kwamba sio wajumbe wote wa Bunge hilo wanaoipenda Katiba Mpya kwa sasa. Kuna wasioona matatizo yoyote na hii Katiba iliyopo kwa kutotilia maanani ubaya na uzuri wake,  na wapo wanaotaka Katiba iliyopo iendelee pamoja na kuyaelewa mapungufu mengi iliyo nayo.
 
Ila si kwamba wanaopenda iendelee jinsi ilivyo wanafanya hivyo kwa kuiona ni bora, hapana, ni kwamba wanaipenda kutokana na yale inayowapatia kwa wakati uliopo. Pindi mambo wanayonufaika nayo kwa mujibu wa Katiba hiyo yakisitishwa si ajabu watu hao wakageuka na kuwa Ukawa wakali sana kuliko hata hawa tunaowaona kwa sasa.
 
Hilo ndilo tatizo kubwa linalowasumbua baadhi ya wananchi, kupofushwa na maslahi binafsi bila kujali kuwa kuna wananchi wengine!
 
Nitoe mfano mmoja, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),  Jaji Frederick Mwita Werema, aliwahi kutamka kwamba Katiba iliyopo haina tatizo lolote. Kwake madai ya Katiba Mpya ulikuwa ni msukumo tu wa wananchi wakorofi! Vivyohivyo kwa aliyekuwa Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani.
 
Sasa la kuzingatia ni kwamba watu hao wote wawili ni sehemu ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba. Je, ni nini tunaweza kukitarajia kutoka kwao? Hivi tunaweza kusema kweli  watu hao wamedhamiria kukitimiza wanachokifanya? Watu hao ambao wametamka hadharani kwamba hakuna umuhimu wa kuandika Katiba Mpya, wanaweza wakatutengenezea Katiba Mpya kweli?
 
Huo ni mfano mmoja,  lakini wajumbe wa aina hiyo ndani ya Bunge Maalumu la Katiba wako wengi. Wao wanajali Katiba iliyopo imewakaliaje kwa sasa bila ya kujali kama kuna kesho.
 
Kwa upande wangu naamini kwamba huo ni mtazamo batili, kuangalia tu manufaa ya leo,  tena yaliyo binafsi,  katika suala linalohusu umma. Kitu kama Katiba ya nchi kinapaswa kiunufaishe umma wote kwa wakati uliopo na wakati ujao. Kuiandaa Katiba ya nchi kwa mtazamo wa wakati uliopo tu hakuitendei haki nchi wala wananchi hata kidogo.
 
Juma lililopita kuna mtu alinitumia ujumbe mfupi wa maandishi katika simu yangu kufuatia makala yangu iliyopita, akidai kwamba najikweza sana kwa kuwaunga mkono Ukawa! Sikuelewa najikweza kivipi,  kwa mtazamo wake!
 
Kwakuwa alichokisema namini  alikisoma kwenye makala yangu, hivyo na mimi ningependa kumjibu kwa njia hii ya makala.
 
Napenda nimfahamishe mtu huyo kwamba mimi siishabikii Ukawa kwa vile nimeiona wakati huu, hii Ukawa ya sasa ina muda mfupi sana tangu ijulikane. Mimi nilianza kuipigania Katiba ya Wananchi miaka 37 iliyopita.
 
Mwalimu wangu wa somo la Elimu ya Siasa, Elizabeth Rweyemamu, anaweza kuwa shuhuda wa hili nilisemalo kwa sasa, maana mwaka 1977 alinitoa darasani na kunipa adhabu ya kukata nyasi siku nzima kutokana na mimi kulalamikia kitendo cha watu wasiozidi 20, Tume ya Sheikh Thabith Kombo,  kujifungia ndani eti wanaandika Katiba ya nchi ya watu wasiopungua milioni 17 bila kuwahusisha wananchi wenyewe.
 
Kwahiyo nataka ionekane kwamba Ukawa ya sasa ambayo haina hata umri wa miezi 3 imenikuta tayari ninao mtazamo kama ilio nao lakini wa kwangu ukiwa unakaribia miaka 40 sasa! Hivyo huyo anayedai najikweza kwa Ukawa atawezaje kujiona yuko sahihi?
 
Lakini hatahivyo, japo kitendo kile nilikilaani kwa wakati huo, ni kwamba kilikuwa kimejaa uzalendo ndani yake tofauti na sasa ambapo zaidi ya watu 600, bila kujali gharama inayotumika ambayo ni pesa ya walipakodi, wanataka watumie wingi wao kukibariki kitendo kilichofanywa na watu wasiozidi 20 mwaka 1977! Ni ufujaji usio na uzalendo hata kidogo.
 
Wakati ule mambo yangeweza kufanyika, hata kwa kulazimisha, lakini gharama ikiwa imezingatiwa, kwamba kama mambo ni ya kulazimisha hakuna haja ya kuharibu pesa ya walipakodi kwa kuingia gharama inayowahusisha watu wengi bila sababu wakati hata wachache wangeweza kufanya maamuzi yanayotakiwa na mamlaka husika bila kupingwa na yeyote.
 
Kwahiyo katika mchakato wa sasa, baada ya baadhi ya wajumbe wa BMK kuona wenzao wamedhamiria kuwapa wananchi Katiba Mpya iliyo ya kweli, kwa kutumia umoja wao waliouita Ukawa, nao wakaanzisha umoja mwingine waliouita Tanzania Kwanza!
Lengo la Tanzania Kwanza silielewi vizuri, ila naona ni kama linapingana na Ukawa. Sababu unaweza kujiuliza Tanzania Kwanza kwa maana gani? Mtu anayepingana na maoni ya wananchi kuhusu uendeshaji wa nchi yao anawezaje kusema anawajali wananchi hao kiasi cha kujiona anaitanguliza nchi yao kwa kuujali sana musitakabali wake kama ilivyo kwa neno hilo, Tanzania Kwanza?
 
Watu wasiojali ufujaji wa rasilmali za nchi, wakifanya mambo ambayo hayaonyeshi tija kwa nchi, au tuseme kwa Watanzania, wanawezaje kuwa na ujasiri wa kujiita Tanzania Kwanza? Au tuseme wao wanalifurahia tu neno Tanzania bila kuhitaji kujihusisha na nchi inayolibeba jina hilo pamoja na wananchi waliomo?
 
Kila nikiangalia kwa makini naona kwamba wengi wanaojiita Tanzania Kwanza ni wale wanaotoka kwenye vyama vinavyojiita navyo ni vya upinzani,  lakini kila nikijaribu kuwapata wanachama wake siwaoni! Ila pamoja na kujiita vyama vya upinzani vinaonekana vikifanya mambo yake kwa ukaribu sana na chama tawala, CCM, vikiwa vingi havina hata mbunge mmoja!
 
Lakini kwa upande wa Ukawa utakuta wengi wanaounda umoja huo wanatoka kwenye vyama vikuu vya upinzani. Wanao wabunge wanaounda kambi ya upinzani Bungeni. Hao wanapojiita Umoja wa Katiba ya Wananchi walau nakielewa wanachokimaanisha. Kwanza wamekuwa wakiidai Katiba Mpya kwa muda mrefu, ndio walioshinikiza mpaka mchakato huu ukaanzishwa,  pili wanao wananchi nyuma yao. Wanao wabunge waliochaguliwa na wananchi kudhihirisha kukubalika kwao.
 
Sasa hawa walioingia katika Bunge Maalumu la Katiba kwa mapenzi ya rais, aliye pia mwenyekiti wa CCM, wakisema Tanzania Kwanza, huku wakionyesha wazi wanaungana na CCM kuchakachua maoni ya wananchi, tuwaeleweje? Ni Tanzania kwanza kwa vile wanaiona Tanzania ni nchi ya kuchakachua?
 
Na ikizingatiwa kwamba CCM haijawahi kuwa na wazo la kuandika Katiba Mpya, tutakosaje kuwaona hawa Tanzania Kwanza kuwa wanafanya kazi ya kutumwa na chama hicho tawala ili kuuvuruga mchakato mzima wa kuipata Katiba Mpya iliyopendekezwa  na wananchi?
 
Mwishoni kabisa nikiri kwamba kwa kadri mambo yanavyojionyesha si wote walio wa CCM wanataka mchakato huu uharibike, wazalendo wapo ndani ya CCM wanaounga mkono Ukawa, ila hawataki kujionyesha wazi kutokana msimamo wa chama chao ulivyo, wakiogopa kisiwachukulie hatua kinazodai ni za kinidhamu kwa kuwaona ni waasi na wasaliti.
 
Mpaka hapo tutakuwa tumeona nani mkweli na nani mpotoshaji kati ya Ukawa na Tanzania Kwanza.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau