FIKRA POTOFU ZINACHANGIA UGUMU WA MAISHA
Na Prudence Karugendo
KUFUATIA makala niliyoandika hivi karibuni
nikilalamikia michango mikubwa ya sherehe, wamejitokeza wasomaji wengi kuniunga mkono.
Karibu wote waliowasiliana na mimi baada ya kuisoma makala hiyo wameniomba niuendeleze mjadala huo kuzidi
kuweka wazi kinachoifanya jamii yetu kuwa na mtazamo huo potofu.
Kinachojionyesha
kwamba mambo hayo ya kuchangishana kwa ajili ya sherehe yanafanyika kwa mtindo
wa kulazimishana, bila kutilia maanani ugumu wa maisha unaoikabili jamii yetu,
ni kwamba sikupata hata mtu mmoja aliyepingana na mtazamo wangu huo wala
kuukosoa, wasomaji wote walikuwa wanailaani tabia hiyo ya kuchangishana kwa
ajili ya sherehe za masaa machache tu huku yakiachwa mambo yenye maana na
yaliyo muhimu. Mpaka nimefikia kujiuliza kama watu wanailaani michango hiyo kwa
nini wanalazimika kuichanga?
Mara nyingi
nimeuliza kwa nini tunalazimika kuingia kwenye gharama zisizo za lazima kwa
kufanya mambo yasiyokuwa na faida endelevu kama haya ya kuchangia sherehe, ziwe
za harusi, kumuaga binti anayeenda kuolewa, sendoff, na nyingine nyingi
zilizojaa kwenye jamii yetu, tena kwa kuchangia kwa pesa nyingi? Lakini mara
nyingi jibu ninalopewa ni la kwamba unapochanga pesa kidogo unategemea
utakunywa na kula nini wakati wa sherehe husika? Eti ukubwa wa michango
unatokana na kupanda kwa gharama ya maisha!
Jambo hilo
linanipa ugumu wa kulitafsiri, sababu kumchangia mtu ili akafanye sherehe yake
haina maana kwamba unachangia unachoenda kukila au kukinywa, hapana, unachangia
ili kumwezesha jamaa yako afanikishe sherehe yake. Kwa maana hiyo sio kwamba
unatakiwa uchangie utakachoenda kukitumia. Suala la kufanya sherehe ni la mwenye sherehe, kwa
maneno mengine ni kwamba alipaswa afanye yeye sherehe na kuwakaribisha walio
karibu naye kwa ajili ya kusherehekea, kula na kunywa bure. Kwa ufupi ni kwamba
mchango wa mwalikwa ni uwepo wake kwenye sherehe husika, huo ni mchango tosha.
Nasema hivyo
kwa sababu mwenye sherehe, hata awe na mapesa mengi kiasi gani, bila kuwa na
watu kwenye sherehe bado hawezi kufanikisha lolote, sherehe bila watu haiwezi
kuhesabika ni sherehe. Ndiyo maana nasema siyo lazima mtu achangie ndipo aweze
kushiriki sherehe.
Yapo mambo
ambayo yanahitaji mtu kuyachangia ili aweze
kuyashiriki. Michezo, kama mpira wa miguu, Simba na Yanga kwa mfano, ili
uweze kuingia uwanjani kuona mpambano huo wa watani wa jadi ni lazima ulipe
kiingilio. Wanaoandaa pambano hilo wanategemea wapate pesa toka kwa watazamaji
au washangiliaji. Pambano la aina hiyo ni moja sehemu ya wahusika kujipatia
kipato zikiwemo timu zenyewe.
Lakini
linapokuja suala la sherehe mambo yanakuwa tofauti. Sherehe sio kwa ajili ya
kukusanya kipato, ni kwa ajili ya kutumia tu kukifurahia kilichokusudiwa. Kama
ni harusi ni kwa ajili ya kuwapongeza wanaooana, kumpongeza aliyeoa au
aliyeolewa.
Na wenye
jukumu la kufanya hivyo ni wazazi wa wahusika au wahusika wenyewe. Wageni waalikwa
kazi yao ni kuhudhuria ili kuwapongeza na kupatiwa kila kilichoandaliwa katika
kusherehesha tukio. Haina maana wala ulazima wa waalikwa kukichangia
watakachokitumia kwenye sherehe husika.
Hatahivyo
sio vibaya kwa watu wa karibu na wenye sherehe kuwapa michango yao kama sehemu
ya kuwaunga mkono, ila izingaiwe kwamba anayekuunga mkono hupaswi kumwekea
kiwango anachopaswa kukuunga nacho mkono kana kwamba bila yeye wewe huwezi
kufanikisha lolote. Kama ni hivyo bora mtu akaachana na sherehe.
Sioni kwa
nini mtu atamani kufanya sherehe kubwa ya kifahari kwa kutegemea mifuko ya watu
wengine. Mambo hayo ndiyo yanayowafanya watu waweke kiwango cha chini, kwamba
kiwango cha chini ni shilingi laki moja chini ya hapo mtu atapewa tu asante
bila ya kadi! La kujiuliza ni kwa nini mtu akupangie kiwango cha kumsaidia
kufanya sherehe halafu mwisho wa siku sifa apate yeye kwamba alifanya sherehe
ya kifahari wakati mambo yote yalikuwa ya kuombaomba?
Mimi naona
sio vibaya kama mtu ana pesa yake, hata akipanga kufanya sherehe ya kifahari
namna gani ni juu yake, kusudi kama ni
sifa ziende kwake kwa maana halisi, kwamba kafanya sherehe ya kifahari kwa
kuwaita watu washerehekee bila kuwatoza kiingilio. Lakini kwa kuwapangia
kiwango wanachopaswa kutoa sifa inastahili iwaendee walioshiriki kwa kukubali
bila sababu za msingi kulipa kiingilio kikuwa kuhudhuria sherehe ya ndugu,
jamaa, rafiki au jirani yao.
Nasema
kwamba sio sababu ya msingi kuhudhuria sherehe ambayo unaambiwa sahani ya
chakula ni shilingi 35,000 – 40, 000 wakati chakula chenyewe ni cha kawaida,
wali vijiko 3, nusu ndizi, kipaja cha kuku na madoido mengine ambavyo kwa
pamoja havifikii thamani ya shilingi 6, 000/=! Papo hapo eti vinywaji, mfano
bia inayouzwa kwa sh. 2,200 eti kwenye sherehe inauzwa kwa sh. 5000/, soda
ambayo kawaida ni sh. 600/ eti kwenye sherehe ni sh. 2000/ nakadhalika!
Mambo
mengine yanayonifanya mpaka nikasikia kizunguzungu ni huu mtindo wa sasa ambao
baadhi ya wafanyabiashara wanajenga maholi yeye viyoyozi kiasi cha kuwazubaisha
watu na kuwafanya wayatamani pamoja na gharama kubwa zinazowekwa ili kuyatumia.
Maholi hayo kwa sasa yanakwenda mpaka shilingi 10, 000, 000/ wakati muda
unaotumika kukaa mle hauzidi masaa manne! Sababu kawaida kuingia kwenye holi,
kama ni sherehe ya harusi au “sendoff” kumuaga mwali anayeenda kuolewa, ni saa 2 mpaka saa 6 usiku. Bila kingine cha
ziada tayari kiasi cha kati ya shilingi milioni 3 mpaka 10 kinakuwa
kimeteketea!
Jambo lingine
ambalo nashangaa kwa nini watu hawalipigii kelele ni ule mtindo wa wenye maholi
ya sherehe kutaka kuhodhi kila mapato yanayotokana na wenye sherehe. Mbali na
kutoza pesa iliyo kama kufuru kwa ajili ya holi tu, bado wenye kumbi hizo
wanataka mapambo, vyakula, vinywaji nakadhalika, vyote vitoke kwao.
Unaweza
kukuta wenye ukumbi wanataka mpaka shilingi milioni 20 kwa ajili ya chakula tu,
wakati chakula kitakachotumika hakizidi cha sh. 7,000,000/, kwahiyo kinachobaki
hakitupwi. Pamoja na kuwa kimenunuliwa chote kikibaki kinahifadhiwa na kuuzwa
tena kwenye shughuli nyingine! Matokeo yake wenye bahati mbaya wanaambulia
kuuziwa kwa bei mbaya chakula kilichooza!
Wakati mambo
yakiwa hivyo bado kumbi za kawaida ambazo zinatoza viwango nya wastani zipo,
ila kwa fikra za ajabu watu hawazipendi kumbi hizo kwa madai ya kwamba
zimepitwa na wakati! Lakini ukija kuangalia wanaosema hivyo wana kitu gani
kinachowafanya wayaone mambo mengine yamepitwa na wakati, kwa maana ya kuwa na
kipato kikubwa kinachowafanya wawe na jeuri hiyo, kipato kinachokwenda na
wakati, unakuta hakuna!
Kipato cha
miaka 20 iliyopita karibu ni kilekile kinachotumika mpaka leo! Ila watu
wanakubaliana na kupanda kwa gharama za maisha wakijiminya kwa kila namna ili
kwenda nazo sambamba gharama hizo! Wanakubali kwamba mambo fulanifulani,
kimatumizi, yamepitwa na wakati ila hakuna anayeona kuwa kipato kilichopo kwa
sasa nacho kimepitwa na wakati!
Hayo ndiyo
mawazo ya Watanzania walio wengi. Kufanya mambo pasipo kutafakari kwanza huku madai ya kwamba gharama
za maisha zinapanda yakiendelea kila kukicha! Lakini ukija kuangalia utakuta
gharama hazipandi zenyewe, zinapandishwa na wananchi walewale wanaolalamika
kutokana na kufanya mambo wakiwa wameegemea kwenye ufahari usio na mpangilio,
ufahari usiojali kiwango cha kipato.
Kwa maana
hiyo nimalizie kwa kusema kwamba upandaji wa gharama za maisha unatokana na
fikra za wananchi zilivyo, wananchi wakisema gharama zisipande haziwezi kupanda
hata kidogo, ila wakiziachia zipande zitapanda mpaka mbinguni, na hakuna
anayepaswa kulalamika. Sababu anayejipiga mwenyewe hapaswi kulia na mtu.
0784 989 512