Bukobawadau

ZAIKO LANGA LANGA NA MAGEUZI YA MUZIKI NCHINI CONGO

 Na Daniel Mbega Bendi hii ndiyo iliyoleta mageuzi ya muziki wa Congo ikiingiza midundo ya kasi iliyoutofautisha muziki wa soukous na rhumba kama lile la African Jazz na TP OK Jazz ambapo walianza kutumia vyombo vya kisasa zaidi yakiwemo Magitaa ya umeme. Midundo ya drums ilirithiwa kutoka kwenye muziki wa asili wa Congo, na hapa ndipo walipoanza kutumia sebene zaidi, kiasi ambacho kinawafanya wataalamu wengi wamuziki waiite bendi hiyo kama “shule ya utatu” ya soukous. Masuala la kurap kwenye muziki wa dansi yaliasisiwa na bendi hii na ndiyo tumeendelea kushuhudia hata sasa bendi nyingi za Afrika Mashariki yote zikiwatumia marapa kuhanikiza muziki hasa wakati wa sebene.
Ghafla Zaiko ikawa bendi maarufu nchini Congo na ilikuwa na mashabiki wengi hasa vijana wa Kinshasa, ambao waliachana na rhumba waliloliita la “wazee”. Katika miaka ya 1970, waimbaji Evoloko "Lay Lay" Joker, Papa Wemba, Gina Efonge, Mavuela Somo, Nyoka Longo na Bimi Ombale walianzisha na kuukuza mtindo mpya uliojulikana kama ‘kavasha’ (cavacha), ambao uliigwa na bendi nyingi za Afrika Mashariki. Mwaka 1973, bendi hiyo ilikuwa imetawala anga la muziki wa Congo kuliko zote huku mwimbaji Evolocko Jocker akiwa ndiye mwanamuziki mashuhuri zaidi wa kundi hilo, hasa kwa ubunifu wake wa mtindo wa ‘kavasha’ ambao uliwapagawisha mashabiki wengi katika ukanda wote wa Afrika Mashariki na Kati katika miaka hiyo ya 1970. Katika mwaka huo wa 1973, bendi hiyo ilitoa albam yao ya kwanza (Long Player – LP) iliyokuwa na nyimbo kama "Eluzam" na " Mbeya Mbeya" (Evoloko Lay Lay), "Zania" (Mavuela Somo), Zena, Semeki Mondo, na Muana Wabi. Mwaka huo wa 1973 Papa Wemba pia alikuwa ameibuka na kibao cha "Chouchouna" wakati Efonge Gina aliibuka na kibao cha "BP ya Munu".

Kufiki mwaka 1974, Zaiko Langa Langa ilikuwa miongoni mwa bendi zilizoalikwa kutumbuiza kwenye tamasha kubwa la Zaire '74, tamasha maarufu na kupromoti pambano kubwa na la kwanza kabisa la ndondi za uzani wa juu duniani kufanyika barani Afrika ambalo liliwakutanisha bingwa mtetezi George Foreman na Muhammad Ali, ambaye alishinda kwa knock out katika raundi ya 8 usiku wa Oktoba 30 kwenye Uwanja wa 20th May. Tamasha la Zaire ’74 lilifanyika kwa siku tatu mfululizo likipiga muziki ‘live’ tangu Septemba 22 hadi 24, 1974 kwenye Uwanja wa 20th May jijini Kinshasa likiwa chini ya uratibu wa mpiga tarumbeta mashuhuri wa Afrika Kusini Hugh Masekela na mtayarishaji wa muziki Stewart Levine ambapo lilihudhuriwa na watazamaji 80,000 kila siku, chini ya udhamini wa promota maarufu wa masumbwi Don King. Jumla ya bendi 31 zilishiriki tamasha hilo, ambapo 17 zilikuwa za Congo (Zaiko ikiwa miongoni mwazo) na 14 kutoka nje wakiwemo wanamuziki mashuhuri kama James Brown, Bill Withers, B.B. King, The Spinners, Miriam Makeba, Celia Cruz na Fania All-Stars. Itaendelea...
Next Post Previous Post
Bukobawadau