Bukobawadau

KANALI MASSAWE ASHIRIKI UJENZI WA MAABARA WILAYANI ILI KUHAKIKISHA MAABARA ZOTE MKOANI KAGERA ZINAKAMILIKA IFIKAPO NOVEMBA 30, 2014

Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Massawe ameonyesha mfano kwa watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya Karagwe na Kyerwa kushirikiana kwa pamoja kusaidiana na wananchi kuhakikisha vyumba vitatu vya maabara kila shule ya kata vinakamilika ifikapo Novemba 30, 2014

Mkuu huyo wa mkoa alionyesha mfano wa kwa watendaji na wananchi kwa kushiriki kusomba matofali  na kuamua kupanda juu ya vitanda kushiriki ujenzi wa maabara  katika shule ya Sekondari Mukile katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa wakati akikagua ujenzi wa maabara katika Wilaya hizo..

 Katika  ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliwaonya watendaji wa Halmashauri hizo mbili kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa  maabara unakamilika kwa tarehe iliyopangwa  la sivyo watapoteza kazi zao kabla yeye Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kufukuzwa kazi na Rais Kikwete.
 Aidha aliwaonya viongozi wa siasa ambao ni madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji  wanaozembea kuhamasisha wananchi kushiriki katika uchangiaji wa ujenzi wa maabara kuwa wasipotimiza wajibu wao yeye Mkuu wa mkoa atawashitaki kwa wananchi ifikapo wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili wananchi wasiwachague tena.
Kasi ya Ujenzi
Katika wilaya za Karagwe na Kyerwa kuna kasi kubwa ya ujenzi wa vyumba vya maabara tatu kila shule  ambapo ujenzi huo unaonekana ifikapo Novemba 30, 2014 watakuwa wamekamilisha vyumba vyote vya maabara kwani ujenzi upo katika hatua mbalimbali hasa kuezeka na hatua za linta.
 Chanagamoto
Kutokana na wananchi kuhamasishwa kuchangia ujenzi wa maabara katika wilaya hizo kumekuwepo na changamoto za baadhi ya viongozi wa kisiasa kuhamasisha wananchi kugomea uchangiaji huo na kupelekea kuleta madhara kwa baadhi ya watendaji kujeruhiwa na na wananchi wakolofi kwa kukatwa mapanga.
Katika kata ya Nyakatuntu Afisa Mtendaji wa kata Bw. Simon Kagaruki alijeruhiwa na baadhi ya wananchi kwa kukatwa panga la kichwani wakati akikusanya michango toka kwa wananchi katika kijiji cha Kyerere kitongoji Omukishambya na kujeruhiwa vibaya sana.
 Kanali Massawe aligiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha wanawakamata watuhumiwa walihusika na kitendo hicho na kufikishwa mara moja katika mkono wa sheria. Aidha aliwaagiza watendaji wa Kata na vijiji kutumia Polisi kwenye vijiji vikorofi wakati wakikusanya michango ili kuthibiti amani na utulivu katika maeneo hayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe inatarajia kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Maabara 57 katika shule 19 ifikapo Novemba 30, 2014. Aidha Halmashauri ya Wilaya Kyerwa inatarajia kukamilisha maabara 63 katika shule 21 za sekondari na kukabidhi mwishoni mwa mwezi huu.

Na; Sylvester Rapahel

Next Post Previous Post
Bukobawadau