Bukobawadau

MABADILIKO YA WAKUU WA MIKOA ;MASSAWE WA KAGERA AONDOLEWA!

Mapema ya jana Mh..Kanali  Mstaafu Fabian Massawe  akihutubia katika hafla iliyoandaliwa na Mshauri wa Ki-mataifa wa kujitegemea (International Independent Consultant) Fr. James Rugemalira, wa Mabibo Breweries, hafla ya kuzungumzia fursa za maendeleo na uwekezaji katika mkoa wa Kagera ndani ya mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Hafla hiyo ilihudhiriwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera , ambaye alikuwa Mgeni Rasmi
 Wengine waliohudhuria ni pamoja na wana Kagera wanaoishi na kufanya Kazi nje ya mkoa wa Kagera wakiwemo wakili wa kujitegemea Bw. Protase Ishengoma wa IMMMA Advocates, mfanyabiashara na Mshauri wa Fr. James, Bw. Anic Kashasha,
 Bw. Abdul Katabaro ambaye amestaafu kutoka utumishi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mzee Andrew Kailembo kutoka Bruxelles, Rev. Fr. David na Bw. Kyabukoba, miongoni mwa wengi.
  Fr. James Rugemalira,wa Mabibo Breweries akiongea na wanahabari katika hafla hiyo.
Fr. James alisisitiza juu ya mkoa kuzitumia fursa nyingi za uchumi zinazotokana na jiografia ya mkoa wa Kagera kupakana na nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki, zikiwemo Burundi, Rwanda, Uganda na Kenya kwa maana hiyo kuufanya mkoa huo kuwa ndicho kiunganishi cha nchi zote (hub). Kwa sababu hiyo alisisitiza umuhimu wa mkoa wa Kagera kuwa na miradi mikubwa ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa uwanja wa Ki-mataifa Omukajunguti, ujenzi wa Bandari Kavu na maeneo huru ya Uzalishaji (EPZ) eneo la Kitengule na kilimo cha Matunda, mboga na mazao mengine ya chakula. Alisisitiza kuwa soko la mazao lipo katika nchi zinazouzunguka mkoa wa Kagera.
Fr. James aliitumia fursa hiyo kuelezea mipango ya kampuni ya Mabibo Breweries kuwekeza kwenye kiwanda cha kuzalisha bia aina ya Windhoek katika mikoa ya Kagera, Tanga na Kilimanjaro. Pia alizungumzia mpango wa kuanzisha taasisi ya ki mataifa ya uchunguzi na tiba kwa maradhi ya Kansa kitakachojulikana kama RUTAKWA BYERA INTERNATIONAL DREAM TANK CANCER CENTER ndani ya Manispaa ya Bukoba.
  Hafla hiyo iliyofanyika kwenye hoteli ya Kolping, mjini Bukoba, pia ilihudhiriwa na waandishi wa habari kutoka kwenye vyombo mbalimbali vya habari. 
 Tukiwa bado katika hafla hiyo tunapokea taarifa kuwa Rais Kikwete afanya mabadiliko ya Wakuu wa Mikoa: Mulongo ahamishiwa Mwanza; Masawe wa Kagera aondolewa!
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amefanya uteuzi wa wakuu wapya wanne wa Mikoa, amewahamisha wengine sita na ameamua kuwa wengine watatu watapangiwa kazi nyingine.

Taarifa iliyotolewa mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue inasema kuwa, Wakuu wapya wa Mikoa ni Bi. Halima Omari Dendego ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Dkt. Ibrahim Hamisi Msengi ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Bi. Amina Juma Masenza ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa na Bwana John Vianney Mongella ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Taarifa inasema kuwa kabla ya uteuzi wake Bi. Dendego alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dkt. Msengi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Bi. Masenza alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilemela na Bwana Mongella alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Arusha.

Taarifa hiyo inasema kuwa Wakuu hao wapya wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi, Novemba 6, 2014 saa saba mchana, Ikulu, Dar es Salaam.

Aidha, taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ambao watapangiwa kazi nyingine ni Kanali (Mst) Fabian Massawe wa Kagera, Dkt. Christine Ishengoma wa Iringa na Kanali Joseph Simbakalia wa Mtwara.

Wakuu wa Mikoa ambao wamehamishwa vituo vya kazi ni Bwana Magesa S. Mulongo ambaye anakwenda Mkoa wa Mwanza kutoka Arusha, Dkt. Rehema Nchimbi ambaye anakwenda Mkoa wa Njombe kutoka Dodoma, Bwana Ludovick John Mwananzila anakwenda Tabora kutoka Lindi, Kepteni (Mst) Anseri Msangi anayekwenda Mkoa wa Mara kutoka Njombe na Mhandisi Everist Ndikilo ambaye anakwenda Arusha kutoka Mwanza.

Wengine waliohamishwa ni Luteni (Mst) Chiku A.S. Galawa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kutoka Tanga, Dkt. Rajab Rutengwe ambaye anakwenda Mkoa wa Tanga kutoka Katavi, Bi Fatma Mwasa ambaye anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita kutoka Tabora na Bwana Magalula S. Magalula ambaye anahamishiwa Lindi kutoka Geita.

Taarifa hiyo imesema kuwa Wakuu wa Mikoa ya Dar es Salaam, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mbeya,Morogoro, Pwani, Rukwa, Shinyanga, Ruvuma, Singida na Simiyu watabakia kwenye vituo vyao vya sasa.

Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi wa Wakuu wapya wa Wilaya, kuhamisha baadhi yao na kutengua uteuzi wa baadhi.

Taarifa kamili itatolewa na Waziri Mkuu baada ya kuwa wamepangiwa vituo vya kazi.


Imetolewa na;
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05 Novemba,2014
Next Post Previous Post
Bukobawadau