Bukobawadau

MH.MASSAWE NA MIKAKATI MIPYA YA UJENZI WAMAABARA KWA MADIWANI NA WATENDAJI

Mkuu wa mkoa wa Kagera aibua mikakati mipya  ya ujenzi wa maabara tatu kila shule ya Kata (shule za serikali) ili ujenzi  ukamilike kwa wakati katika kutekeleza agizo la Rais Kikwete la Januari  2013 linalowataka wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya kuhakikisha maabara zote zinakamilika ifikapo Novemba  30, 2014.

 Kanali Mstaafu Fabian Massawe ameamua  kuhudhuria vikao vya mabaraza ya Madiwani kila Halmashauri kuzungumza na Madiwani ili kupokea taarifa zao na mikakati ya ujenzi wa maabara tatu kila shule imefikia wapi katika utekelezaji aidha kuwapa mbinu mpya kuhakikisha maabara hizo zinakamilika kwa wakati .
 Katika vikao hivyo vinavyoendelea mkoani Kagera katika Halmashauri zote  Mkuu wa mkoa amekuwa akipokea taarifa ya kila kata kutoka kwa Diwani husika kuhusu hatau iliyofikiwa katika kukamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara za fizikia, kemia na Baiologia katika shule husika.

Mikakati mipya aliyowapa madiwani katika mabaraza yao Mkuu wa Mkoa wa Kagera ni kutumia ushawishi  mkubwa badala ya kutumia nguvu kwa wananchi kukusanya michango ili kukamilisha ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule.

Kuhamasisha wananchi kuchangia vifaa vya asili kama mchanga, mawe, kokoto na matofali badala ya kuwabana kuwa watoe michango ya fedha tu ili mwananchi kila mwenye uwezo wa kupata vifaa hivyo avitoe au asiyeweza atoe kiasi cha fedha kulingana na  gharama za vifaa kwa kila mwananchi.

Mkakati mwingine alioutoa kwa madiwani Kanali Massawe ni kuitisha harambee ya wananchi wote na wazawa wenye uwezo walioko nje ya mkoa ili kuchangia  ujenzi wa maabara ukamilike kwa wakati na ifikapo Novemba 30, 2013 akatoe taarifa kwa Rais Kikwete.

Mkakati mwingine  ni Madiwani kukubali kubadilisha vipaumbele vyao ambavyo vilikuwa vimetengewa fedha katika bajeti ya mwaka 2014/15 ili fedha hizo za miradi ya maendeleo ziende katika ujenzi wa maabara kwani maabara pia ni kipaumbele kwa maendeleo ya wananchi.

“Nawashauri sasa Waheshiiwa Madiwani mkishirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na menejimenti yake kuangalia uwezekano wa kufanya mabadiliko ya vipaumbele (re- allocation) ili kuchangia ujenzi wa maabara. Lakini mchakato huo unatakiwa kupitia katika baraza la madiwani ili ukubaliwe na madiwani.” Alisistiza Kanali Massawe.
Aidha, Kanali Massawe katika ziara hiyo aliambatana na Katibu Tawala Msaidizi Serikali za mitaa Bw. David Lyamboko  ambaye alikuwa akitoa ufafanuzi jinsi ya kubadili vipaumbele vya miradi iliyopangiwa fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/15 ili fedha hizo ziweze kwenda katika ujenzi wa vyumba vitatu vya maabara kila shule katika halmashauri husika.

Bw. Lyamboko aliyashauri mabaraza ya Madiwani kuwa mara baada ya kuangalia miradi iliyopangiwa bujeti ambayo itabadilishwa vipaumbele vyake kwenda kwenye ujenzi wa maabara  inatakiwa mchakato uanziae kwenye ngazi ya vijiji kwa kuandikwa mihtasari na kwenda mpaka ngazi ya halmashauri kwa kufuata taratibu na sheria zilizopo.

Madiwani wakiwasilisha taarifa zao walisema wanakabiliwa na changamoto kubwa katika ujenzi wa maabara hasa baadhi ya wanansiasa kuwagomesha wananchi kuchangia, wananchi kuwadhuru kwa kuwapiga watendji wakikusanya michango ya ujenz,i na wananchi kuchangia kwa kasi ndogo sana.

Akijibu changamoto hizo Kanali Massawe aliwaagiza watendaji wa kata kuchukua hatua mara moja kwa mwananchi yeyote anayegoma kuchangia ujenzi wa maabara katika kijiji chake. Aidha aliwaagiza Wakuu wa Wilaya kusimamia siku hadi siku kujua kinachoendea katika maeneo ya ili ifikapo Novemba 30, 2014 maabara hizo ziwe zimekamilika.

Kuanzia tarehe 3/11/2014 Kanali Massawe anaanza kutembelea Halmashauri zote za Wilaya kukagua ujenzi wa maabara tatu kila shule. Hadi kufikia Septemba 2014 kati ya maabara 570 zianazotakiwa kujengwa mkoani Kagera ni 136 zilikuwa zimekamilika asilimia 23.8
Next Post Previous Post
Bukobawadau