MISS HONDURAS 2014 AKUTWA AMEKUFA
Tegucigalpa, Honduras. Polisi wa Honduras
wamesema wamepata miili inayodhaniwa kuwa ya mrembo wa nchi hiyo
aliyepotea siku sita zilizopita pamoja na dada yake.
Mkuu wa Polisi, Jenerali Ramon Sabillon alisema
jana kuwa wanasubiri taarifa rasmi za uchunguzi wa kitaalamu kwenye
mwili unaodhaniwa kuwa wa Maria Jose Alvarado, 19 na dada yake, Sofia,
23.
Alisema jana kuwa rafiki wa kiume wa Sofia, Plutarco Ruiz, na rafiki yake, Aris Maldonado walitiwa mbaroni.
Mrembo huyo alitarajiwa kuondoka Jumapili kwenda
London, Uingereza kushiriki mashindano ya urembo ya dunia, Miss World
2014. Mamlaka za umma nchini Honduras zimethibitisha kushikiliwa kwa
watu wanne wakihojiwa kutokana na kutoweka kwa mrembo huyo. Mbali ya
rafiki wa kiume wa Sofia, mtu mwingine anayeshikiliwa ni mmiliki wa eneo
la biashara ambako wanadada hao walitoweka, alieleza msemaji wa Polisi,
Luteni Joseph Coello, ingawa hakuwa tayari kutoa maelezo zaidi.
“Kimsingi, tuliwakamata watu kumi, lakini sita kati ya hao tuliwaachia,”
alieleza Luteni Coello.
Kwa mara ya mwisho, Maria na dada yake, Sofia
walionekana Alhamisi kwenye eneo la Santa Barbara, maili 240 magharibi
mwa Tegucigalpa,ambako walikwenda kwa sherehe ya kuzaliwa za Ruiz.
“Mashuhuda walieleza kuwa binti yangu aliondoka
akiwa na wanaume watatu,” alieleza mama mzazi, Teresa Munoz. “Nilijaribu
usiku mzima kuwapigia simu zao, lakini hazikujibiwa.”
Kulingana na Umoja wa Mataifa (UN), Honduras ina
matukio kiwango kikubwa cha mauaji mengi. Mengi yanahusishwa na biashara
ya dawa za kulevya, rushwa.