Bukobawadau

UFISADI WAUMALIZA USHIRIKA NCHINI

Na Prudence Karugendo
WAKATI  ushirika nchini unachungulia kaburi wanaushirika wanayo mengi ya kusema kuhusu janga hilo, janga la kutokomea kwa ushirika na kuuacha ubaki kwenye historia tu. Wadau wengi wa ushirika wanasema kwamba janga hilo linaloukabili ushirika halitokani hata kidodo na nguvu za asili zilizo nje ya uwezo wa binadamu wa kulidhibiti, kwamba janga hilo linatokana na nguvu za binadamu wenyewe tena waliopewa jukumu la kuutumikia ushirika, kuulinda na kuuimarisha.
Wanaushirika wengi wanasema kwamba tatizo linalijitokeza ni la viongozi wa ushirika kuuchukulia ushirika kama shamba la bibi ambamo wanaweza kuchuma bila kupalilia, wanaangalia matunda ya shamba tu na sio usitawi wa shambalenyewe.
 Eti kinachofanywa na viongozi wa ushirika ni tofauti na inavyofikiriwa kwamba viongozi hao wameugeuza ushirika kuwa mali yao binafsi, sababu eti mwenye mali binafsi ni lazima aionee uchungu mali yake hiyo na hivyo kuichukulia kwa uangalifu wa hali ya juu, kwamba hiyo ni tofauti na hali halisi ilivyo kwa sasa ambapo viongozi wa ushirika ni kama wanaukomoa ushirika kwa kufanya mambo bila kuujali mustakabali wake.
Wanasema kwamba kitendo cha uongozi wa ushirika, uwe wa kuchaguliwa au wa kuajiriwa, kufuja mali za ushirika kana kwamba ni kukomoana kinadhihirisha ufisadi uliooza. Eti kisichoeleweka ni kwa nini mamlaka ya juu yanayopaswa kuusimamia ushirika na kuuongoza yanayaona hayo yote bila kuchukua hatua yoyote?
Wanasema kwamba waziri mwenye dhamana ya ushirika yupo, anazisikia kelele zinazopigwa na wanaushirika lakini kaamua kukaa kimya bila kuzifanyia lolote kelele hizo, Mrajis wa Vyama vya Ushirika yupo, naye eti anazisikia kila wakati kelele zinazopigwa na wanaushirika lakini kaamua kuzipuuza. Hiyo ni mbali na wale walio karibu zaidi na wanaushirika kwa maana ya warajis wasaidizi pamoja na maafisa ushirika.
Kimya hicho cha wenye jukumu la kuulinda na kuulea ushirika nchini ni kama kinaonyesha kwamba viongozi wa ushirika wanazo baraka zote za kuuhujumu na kuufisidi ushirika kwa namna wanavyoweza hata kama ni kuunyongelea mbali, wanadai wadau hao wa ushirika.
Chama kimojawapo cha ushirika kinachochungulia kaburi ni KCU (1990) Ltd. cha mkoani Kagera. Chama hicho chenye historia ndefu katika nyanja ya ushirika,  kwa sasa kiko taabani. Wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wanasema anayeona kwamba chama hicho kinataabika kwa sababu ya kitu kingine mbali na ufisadi ni bora ajitokeze na kukisema kitu hicho. Eti wao kamwe hawawezi kwenda kwa mganga wa kienyeji kutafuta sababu za ushirika wao kuwa taabani wakati kila kitu kinajionyesha wazi.
Sababu eti mengi yamesemwa na kuuandikwa juu ya ubadhirifu unaofanyika katika chama hicho, ila la kushangaza ni kwamba hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na mamlaka ya juu dhidi ya ubadhirifu huo unaoelekea kuitokomeza KCU (1990) Ltd..
Inasemwa kwamba kutochukuliwa hatua dhidi ya ubadhirifu ndani ya KCU (1990) Ltd. ni sababu moja kubwa inayozidi kuwapa jeuri na kiburi viongozi wa ushirika huo na kuwafanya waongeze nguvu za ufisadi kwa vile wanaelewa hakuna kitakachofanyika. Maana eti wameiziba mianya yote ambayo ingeweza kuwawajibisha na kuwaacha wakulima, wanaushirika, ambao hawana la kufanya kulingana na ubovu wa sheria za ushirika ulivyo.
Mmoja wa wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. anayekerwa sana na ufisadi ndani ya ushirika huo, Archard Felician Muhandiki, anashangazwa sana na hatua ya serikali kuwafumbia macho na kutowachukulia hatua yoyote viongozi na watumishi wa ushirika huo ambao wamejivisha ufisadi husiohojika.
Anasema kwamba pamoja na viongozi wa ushirika huo kukiri tuhuma za ufisadi dhidi yao haoni lolote linaloelekea kukabiliana na kashfa hiyo.
Muhandiki anasema kwamba hakuna kitu kilichomuuma kama kile cha yeye kupeleka malalamiko yake moja kwa moja kwa waziri anayehusika na ushirika lakini waziri huyo akayarudisha malalamiko hayo kwa uongozi wa KCU (1990) Ltd. akiushauri ukamuite Muhandiki na kumfukuza kwenye ushirika kama ingebidi. Muhandiki anasema hayo yalielezwa na mwenyekiti wa KCU (1990) Ltd. kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho na yamerekodiwa.
Muhandiki anasema kwamba yaliyokwisha semwa na kuandikwa juu ya ufisadi unaofanywa na uongozi wa KCU (1990) Ltd. ni mengi sana, eti kama tuhuma zote hizo zingelikuwa ni za uongo ni kitu gani kinauzuia uongozi huo kwenda mahakamani ili kujisafisha?
Anasema, eti badala yake KCU inahangaika usiku na mchana, ikizitumia pesa za chama hicho, kuhakikisha tuhuma hizo zinafukiwa, jambo linalodhihirisha pasipo na shaka kuwa tuhuma hizo ni za kweli. Anasema kwamba inawezekana hiyo ikawa ndiyo sababu ya KCU kuukingia kifua uongozi wa  Chama cha Msingi Kamachumu kwa kutumia vibaya pesa ya wanaushirika kuuwekea mawakili wa kuutetea mahakamani dhidi ya wanachama waliofungua  kesi ya kuuwajibisha.
Anaeleza kwamba ufisadi unafanyika na kuhujumu ushirika halafu inatumika gharama nyingine kubwa ya ushirika huohuo kuifunika hujuma husika. Anauliza katika aina hiyo ya ufisadi kinaofanyiwa chama hicho kikuu kitawezaje kupona?
Wanaushirika wengine wa KCU (1990) Ltd. wanasema kwamba chama hicho kwa sasa kimebaki jina tu bila ya uhai wowote wa kujiendesha. Eti wafanyakazi wengi wa chama hicho wamepunguzwa kutokana na ukosefu wa pesa za kuwalipa mishahara,  na haijulikani pesa ya kununulia kahawa toka kwa wakulima  kwa musimu huu  itapatikana  wapi. Inasemekana hata pesa ya kitengo cha mauzo ya nje, kinachoitwa Moshi Export, imekombwa yote na kukiacha kitengo hicho kikiidai KCU (1990) Ltd..
Kutokana na hali hiyo ya kutatanisha na kutia majonzi kuhusu mwenendo wa ushirika huo, ndiyo maana kwa sasa wakulima wa kahawa ambao ni wanachama wa ushirika huo wanausubiri kwa hamu umoja wa wakulima wa kahawa ulioanzishwa na wanachama wa Kamachumu na kuupa jina la Tweyambe Coffee Growers. Wanasema umoja huo utakuwa mkombozi wao baada ya ushirika kukatishiwa njiani safari yake.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau