Bukobawadau

BALOTELLI AFUNGIWA MCHEZO MMOJA NA FAINI

Chama cha Soka nchini Uingereza, kimemfungia mchezo mmoja, mshambuliaji wa Liverpool, Mario Balotelli ikiwa ni adhabu kutokana na kile Super Mario alichokiandika katika mitandao ya habari ya kijamii.
Adhabu hiyo itamlazimisha nyota huyo wa Italia, kukosa mchezo wakati timu yake ya Liverpool itakapoikaribisha Arsenal Jumapili, katika michezo ya ligi kuu ya England. Pia amepigwa faini ya pauni£25,000 na lazima ahudhurie kozi ya elimu.
Baloteli mwenye umri wa miaka 24 ameadhibiwa kwa mujibu wa sheria za FA kwa kutuma ujumbe ambao umeonekana kuwa na ubaguzi.
Balotelli amekubali adhabu hiyo lakini ameiandikia FA ili iweze kumpunguzia.
Baada ya kujua adhabu yake, aliandika katika ukurasa wake rasmi wa Facebook kwamba uamuzi wa FA "umeonyesha wazi" kwamba ujumbe wake ulikuwa "makosa".
 Mario Balotelli amekuwa akishutumiwa kuweka ujumbe wa kibaguzi mtandaoni
Balotelli aliituma picha iliyotolewa na mtu mwingine tofauti. Alisema: "nasikitika kwamba wachezaji wenzangu na mashabiki wa Liverpool FC wataadhibiwa kwa kosa ambalo nimelifanya na sasa najutia. Ni dhamira yangu kukubaliana na uamuzi wa FA na kuhakikisha kuwa halitatokea tena."
Msemaji wa Liverpool amesema: "klabu inatambua uamuzi uliofikiwa na jopo huru la FA na utapewa uzito unaostahili mara tutakapoupokea kutoka FA.
"Hatua yoyote itakayochukuliwa nasi kuhusiana na jambo hili itakuwa kati ya klabu na mchezaji."
Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester City Balotelli alirudia kutuma picha ya mchezo wa kompyuta yenye kibonzo cha Super Mario katika mtandao wa Instagram ambacho kilikuwa na maneno "ruka kama mtu mweusi na kusanya sarafu kama myahudi."
Baadaye alituma ujumbe wa tweeter akikanusha kuwa ujumbe huo ulikuwa na makosa, kabla ya kuomba radhi.
 Balotelli alirejea katika kikosi cha Liverpool kilichocheza na Manchester United katika uwanja wa Old Trafford Jumapili baada ya kukosa michezo sita kutokana na maumivu ya nyama za paja. Katika mchezo huo Liverpool iliambulia kipigo cha magoli 3-0.
Balotelli ameifungia magoli mawili timu yake katika mechi 15 alizoichezea timu ya Liverpool tangu atoke AC Milan msimu uliopita wa kiangazi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau