Bukobawadau

KCU(1990) Ltd:Yakumbuka shuka kumekucha

NA PRUDENCE KARUGENDO

HATIMAYE  mamlaka ya juu yanayosimamia na kuyalinda masuala ya ushirika nchini yamekifanyia kazi kilio cha siku nyingi cha wanaushirika wa mkoani Kagera kuhusu chama chao kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd.. Mamlaka hayo yameiondoa Bodi ya wakurugenzi ya ushirika huo na kuagiza kwamba wahusika wasiruhusiwe kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika ushirika huo.

Nataja tu mamlaka ya juu kutokana na kutokuwa na uhakika ni mamlaka yapi yaliyoagiza uamuzi huo uchukuliwe. Hiyo ilifuatia wenye mamlaka ya kufanya hivyo, Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mrajis Msaidizi kushindwa kuyashughulikia kwa wakati malalamiko ya muda mrefu ya wanaushirika wa KCU (1990) Ltd..

Kwa karibu kipindi cha miaka minne wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wamekuwa wakitoa malalamiko yaliyosheheni hoja nzito kuhusu mwenendo mbovu wa uongozi wa ushirika wao. Lakini jambo la kushangaza mamlaka husika yalifumba macho na kuziba masikio yakiuacha uharibifu, hujuma na ufisadi viendelee katika ushirika huo kiasi cha kuufanya uonekane unasambaratika kama mali siyo na mwenyewe wala mwangalizi.

Lakini hatahivyo zipo nafasi zilizotengwa mahususi kwa ajili ya kuulinda ushirika, kuuimarisha na kuuboresha. Nafasi hizo ni kama ile ya Mrajis wa Vyama vya Ushirika na wasaidizi wake wakiwemo maafisa ushirika, lakini ni ajabu kwamba nafasi hizo zimegeuka  za kuukandamiza ushirika na kuwaacha wanaushirika wakitaabika huku wakiuona ushirika wao ukisambaratishwa na waliopaswa kuulinda.

Wanaushirika wanasema kwamba Mrajis msaidizi ni mwajiriwa wa serikali,  lakini kimuonekano ni kama mwajiriwa wa ushirika kutokana na kuhudumiwa na chama cha ushirika katika mambo yaliyo mengi kiutendaji! Na katika hilo muda wote Mrajis Msaidizi anakuwa upande wa uongozi wa chama kikuu cha ushirika akifanya kila njia kuwazuia wanachama wa ushirika wasiweze kuuwajibisha uongozi wa chama chama chao pale unapokuwa umezembea katika masuala mbalimbali  nyeti.

Mfano mzuri ni katika sakata ninalojaribu kulionyesha hapa la KCU (1990) Ltd.. Baadhi ya wanaushirika, tena wanaowawakilisha wenzao wa vyama vya msingi, walikuwa na maswali muhimu kuhusu uendeshaji wa chama chao kikuu, KCU (1990) Ltd., lakini badala ya maswali hayo kujibiwa na Bodi ya chama hicho walinyamazishwa kwa nguvu na hata kufukuzwa kabisa kwenye mikutano ya chama hicho bila kujali kuwa wao ni wajumbe waliotumwa na wanaushirika, na wahenga walisema kwamba  mjumbe hauawi.

Na mara nyingi aliyekuwa akiongoza usumbufu huo dhidi ya wawakilishi wa wanaushirika ni Mrajis Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoani Kagera, ambaye kimantiki ndiye aliyepaswa kusimama imara kuhakikisha wanauhoji uongozi kuhusu uozo uliokuwa kwenye chama chao.

Lakini badala yake Mrajis huyo msaidizi alijionyesha wazi anavyoungana na Bodi ya KCU (1990) Ltd. kuuficha uozo ndani ya chama hicho, na matokeo yake KCU (1990) Ltd. ikaanza kusambaratika.

Mtu mwingine ambaye wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wanamlaani sana ni Mrajis wa Vyama vya Ushirika, Dk. Audax Rutabanzibwa, ambaye tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo hakuonyesha juhudi zozote za kuunusuru ushirika wao, ambao kibaya zaidi ni ushirika wa nyumbani kwao.

Inasemekana kwamba badala ya kuushughulikia ushirika wa KCU (1990) Ltd. Mrajis wa Vyama vya Ushirika amekuwa akiwachukulia wote wanaojaribu kuunusuru ushirika huo kama watu wasioupenda ushirika. Ni jambo hilo lililowafanya wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. waanze kuhisi uhusiano haramu kati ya Bodi ya chama chao na Mrajis wa Vyama vya Ushirika.

Wanahoji kitendo cha Mrajis huyo kwenda kuifukuza Bodi ya KNCU ya Kilimanjaro na kushindwa kufanikisha matakwa yake hayo baada ya wanaushirika wa Kilimanjaro kupiga kura wakiugomea uamuzi wake huo.

Kule Kilimanjaro wametamka wazi kuwa Mrajis wa Vyama vya Ushirika amegeuka kikwazo kwa maendeleo ya ushirika nchini.

Swali linalojiweka wazi ni la kwa nini Mrajis aone kasoro kwenye KNCU wakati hajapata malalamiko toka kwa wanaushirika wanaounda chama hicho kuhusu Bodi ya chama chao, lakini ashindwe kuona kasoro kwenye Bodi ya KCU (1990) Ltd. pamoja na malalamiko yote aliyoyakuta na mengine yakizidi kupelekwa kwake na wanaushirika?

Katika hali kama hiyo unawezaje kuzipuuza hisia za wanaushirika wa KCU za kwamba kuna namna ambayo Mrajis wa Vyama vya Ushirika alikuwa akijinufaisha na ubadhirifu uliokuwa ukifanywa na Bodi ya Wakurugenzi wa KCU (1990) Ltd. kutokana na ukaribu na uswahiba aliokuwa akiuonyesha kwa Bodi hiyo?

Na kwa nini isionekane kuwa pengine uamuzi wa Mrajis wa kutaka kuifukuza Bodi ya KNCU ulitokana na Bodi hiyo kumnyima ushirikiano kama ule aliokuwa nao kwa KCU (1990) Ltd. wa kuuminya ushirika kwa manufaa ya wachache?

Sababu mpaka wanaushirika wa KNCU, kule Moshi,  wanatamka kwamba Mrajis ni kisiki katika njia ya maendeleo ya ushirika, ni lazima kuna jambo baya wameliona kwake.

Sasa inasemwa kwamba Bodi ya KCU (1990) Ltd. imeondolewa, ni kweli imeondolewa au imemaliza muda wake? Sababu Sheria ya Ushirika ya 2013 inayotajwa kuwa ndiyo iliyotumika kuiondoa Bodi hiyo bilashaka ilitungwa kuunusuru ushirika, kwahiyo ingetumika mapema lazima kuna mambo yangenusurika katika KCU (1990) Ltd. kuliko sasa ambapo chama hicho ni kama kimefilisika kabisa kutokana na uongozi mbovu wa Bodi hiyo iliyomaliza muda wake.

Ndiyo maana mtu mmoja kasema kwa lugha ya Kihaya kwamba “ajuna akanyonyi akajuna kakyaharara” maana yake ni kwamba anayetaka kumnusuru ndege hufanya hivyo ndege akiwa bado ana uwezo wa kuruka, lakini akisubiri akafa kinachofuatia ni uozo na harufu chafu. Hakuna lingine liwezalo kufanyika.

Aliyekuwa mwakilishi wa chama cha msingi Kamachumu, Archard F. Muhandiki, anasema kwamba Bodi iliyofukuzwa ilimfanyia njama za kila aina kusudi asiweze kutimiza uwakilishi wake kiukamilifu, na hatimaye ikamfukuza kabisa kutoka kwenye uwakilishi. Kwahiyo eti kwa sasa wote, yeye na Bodi,  wako nje ya shughuli za KCU (1990) Ltd.. Kwahiyo anashauri wote, yeye na waliokuwa wakurugenzi wa Bodi hiyo iliyofukuzwa, wafanyiwe uchunguzi wa kina kusudi watakaobainika walihujumu mali za ushirika wakamatwe na kushitakiwa na ikibidi wafilisiwe ili kufidia mali za ushirika.

Nimalizie kwa kusema kwamba, ni kweli Bodi ya KCU (1990) Ltd. imeondolewa na kuwekwa Bodi mpya, lakini hiyo haina tofauti na kukumbuka shuka wakati kumekucha. Nani atoe pongezi kwa hilo?


0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau