Bukobawadau

Prof. Safari to head the CHADEMA delegation to the european parliament

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Bara Prof. Safari Jumbe Abdalla ataongoza msafara wa viongozi wa CHADEMA, unaotarajiwa kufanya ziara ya kikazi kwenye Bunge la Ulaya (EP), mjini Brussels, Ubelgiji kuanzia kesho kufuatia mwaliko wa bunge hilo.

Wengine katika msafara huo watakuwa ni Naibu Katibu Mkuu wa Chama Zanzibar, Salum Mwalimu, Katibu Mkuu wa Baraza la Wanawake (BAWACHA), Grace Tendega, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana (BAVICHA), Patrobas Katambi na Mkurugenzi wa Bunge na Halmashauri, John Mrema.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari kuhusu ziara hiyo ya kikazi kwa siku 10 barani Ulaya, ambayo itaufikisha msafara huo nchini Ujerumani kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Chama Tawala nchini humo cha CDU, Naibu Katibu Mkuu wa Chama, Mwalimu amesema kuwa msafara huo umepangiwa kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali, ukiwemo uongozi wa Bunge la Jumuiya ya Ulaya (EP).

Katika sehemu ya ziara hiyo, msafara wa viongozi hao waandamizi wa CHADEMA pia watapata fursa ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa (African, Caribbean and Pacific) ACP-EU Joint Parliamentary Assembly, jumuiya ambayo huwakutanisha wabunge wa nchi za Ulaya, nchi za Afrika, nchi za Caribbean na zile za Pacific, zilizosaini Mkataba wa Cotonou.

Naibu Katibu Mkuu Mwalimu amewaambia waandishi wa habari kuwa kupitia ziara hiyo ya kikazi, pamoja na masuala mengine, msafara huo utayapatia uzito na kipaumbele masuala 4 kwa niaba ya UKAWA na Watanzania mbele ya Umoja wa Ulaya ambao unajumuisha nchi washirika wa maendeleo na wafadhili wa Serikali ya Tanzania kupitia maeneo mbalimbali, ikiwemo Mfuko Mkuu wa Bajeti.
· Mchakato wa Katiba Mpya
· Umuhimu wa Tume Huru ya Uchaguzi (kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015)
· Uwajibikaji, Rushwa na ufisadi na;
· Uhuru wa Habari, Vyombo vya Habari na Waandishi wa Habari nchini;

“Hawa watu, Jumuiya ya Ulaya ndiyo washirika wakuu wa masuala ya maendeleo kupitia serikali kwa maana ya mikopo, ufadhili na misaada mbalimbali, kupitia miradi ya maendeleo kwenye Mfuko wa Bajeti yaani General Budget Support…sasa wanatoa fedha za walipa kodi wao huko kwenye nchi zao lakini zikifika hapa zinafanyiwa ufisadi, zinafanyiwa ubadhirifu. Kiwa sababu hakuna uwajibikaji wa serikali au viongozi wa serikali kwa wananchi.

“Kwa hiyo masuala ya ufisadi kama haya ya Escrow yanayoendelea au IPTL kwa ujumla wake, ubadhirifu, rushwa inavyoota mizizi kwenye utendaji kazi wa serikali na mambo mengi yanayoonesha namna ambavyo hatuthamini uwajibikaji kama moja ya misingi mikubwa ya maendeleo, tutayazungumza ili hao wafadhili wakubwa wa serikali yetu hii wajue watu wanaofanya nao kazi wakoje.

“Tutawaeleza namna ambavyo mchakato wa katiba mpya ambao ungewapatia Watanzania fursa adhimu ya kuamua namna ya kujitawala na kuongozwa, ulivyoharibiwa na kuingiliwa kwa manufaa ya kikundi cha watu wachache yaani CCM kiasi kwamba masuala muhimu kama uwajibikaji, uwazi, uadilifu yakatupwa.

“Katiba Mpya ya Rasimu ya Warioba ilikuwa inakwenda kutupatia Watanzania fursa ya usimamizi wa rasilimali za taifa kwa faida ya Watanzania…namna ambavyo tunashirikiana na wawekezaji kama wadau muhimu katika maendeleo, lakini maslahi ya Watanzania yakijulikana bayana, badala ya kuporwa kama inavyofanyika sasa kwa sababu CCM inanufaika na ufisadi,” amesema Mwalimu.
Next Post Previous Post
Bukobawadau