Bukobawadau

RAIS KIKWETE ATOA ZAWADI ZA MWAKA MPYA KWA MAKUNDI MAALUM MKOANI KAGERA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete asherekea sikuu ya mwaka mpya na makundi maalum mkoani Kagera kwa kutoa zawadi mbalimbali za sikukuu kwa wahitaji katika makundi ili kusherekea pamoja naye sikukuu ya mwaka mpya.
Zawadi hizo zilitolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera John Mongella kwa makundi maalum ambayo ni vituo vya kulelea watoto yatima Ntoma na Kabirizi, kituo cha kulelea watoto wenye utindio wa ubongo Kemondo na kituo cha kutunza wazee Kiilima vyote vipo katika Halamashauri ya Wilaya ya Bukoba.
 Kwa niaba ya Rais Kikwete Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa mafuta lita 20, kilo 100 za mchele, na mbuzi  mmoja kila kituo isipokuwa kituo cha wazee Kiilima kilipatiwa mbuzi wawili. Akitoa zawadi hizo John Mongella alisema kuwa Rais Kikwete amemwagiza kuzifikisha kwa walengwa washerehekee naye sikukuu za kufunga mwaka.
Akitoa shukrani kwa niaba ya wazee wenzake  Mzee Evalister Kayogera  alisema Rais Kikwete amekuwa akiwakumbuka kila mara na wanamshukuru na kumwombea dua kwa Mwenyezi Mungu ili aendelee kumjalia afya  njema  na kumpa nguvu zaidi kutimiza majukumu yake kwa ufasaha zaidi.
Mzee Evalister Kayogera alisema wao (wazee)  ni kama watoto wa ndege ambao wanawategemea mama zao kuwaletea chakula, kwahiyo  wazee wanaitegemea serikali ambayo  ndiyo mama mlezi wao na imekuwa ikiwakumbuka kwa kutoa  huduma mbalimbali muhimu kwao.
Kituo cha Wazee Kiilima kilianzishwa mwaka 1978, hadi sasa katika kituo hicho kuna jumla ya wazee 12 wanawake 4 na wanaume 8, aidha kituo hicho kinawalea watoto yatima 10 ambapo wasichana ni wawili na wavulana wanane na kuwa jumla ya wahitaji 22.
Next Post Previous Post
Bukobawadau