Bukobawadau

POLISI NA VURUGU

Kwa nini Polisi iwe chanzo cha vurugu?
NA PRUDENCE KARUGENDO
UCHAGUZI  wa serikali za mitaa umemalizika, katika uchaguzi huo yamejionyesha mabadiliko makubwa katika maamuzi ya wananchi. Kwa asilimia kubwa wananchi wameonyesha jinsi wanavyouamini upinzani kuliko utawala uliopo. Hiyo inatokana na matokeo ya uchaguzi huo ambayo yameishusha CCM kutoka kileleni ilikokuwa na kuileta katikati ikiwa ni ishara ya kuibwaga chini muda mfupi ujao.
Lengo la makala haya sio kujadili mwenendo wa uchaguzi huo kwa sasa, isipokuwa kuangalia namna vyombo vya dola  vinavyoyachukulia maamuzi ya wananchi vikiwa havionyeshi kuyaheshimu wala kuyafurahia.
Kwa ujumla uchaguzi huo umeendeshwa kwa amani na utulivu ukiondoa maeneo kadhaa ambako vyombo vya dola, hasa Jeshi la Polisi, lililoamua kuingilia kati na kuanzisha vurugu ikiwa ni ishara ya kutoyafurahia maamuzi ya wananchi. Kwa ufupi ni kwamba wananchi, kama kawaida ya Watanzania ilivyo, waliamua kufanya uchaguzi huo kwa amani na utulivu lakini polisi kwa kukosa kazi ya kufanya baada ya kuona hakuna vurugu jeshi hilo wakaamua kufanya vurugu wenyewe ili waonekane wanatimiza wajibu wao.
Jambo la kusikitisha ni kwamba makamanda wa Polisi wanaamua kufanya kazi ya kuwafurahisha wakubwa wao, hasa viongozi wa kisiasa wa chama tawala, kwa kufanya mambo ya upendeleo wa wazi kwa chama tawala huku wakiwaumiza wananchi ambao ndio waajiri wao katika kutafuta sifa na baadaye kupandishwa vyeo.
Inabidi polisi waelewe kwamba wananchi wote bila aina yoyote ya ubaguzi ndio wanaochangia mishahara yao kupitia kwenye kodi zinazotolewa na kila mwananchi bila kuuliza anatoka chama gani cha siasa. Wananchi wanafanya hivyo ili kujihakikishia usalama wao. Sasa inapokuja wakatenganishwa na kuonekana wengine wanapendelewa dhidi ya wengine hilo ni jambo linaloweza kuamsha hisia za kwamba wanaporwa pesa zao ili zikatumike kuwakandamiza.
Nitoe mfano wa kitu nilichokishuhudia Mjini Bukoba. Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika nchi nzima siku ya Jumapili iliyopita, wananchi wa manispaa ya Bukoba walidhamiria kufanya mabadiliko makubwa ya kisiasa  tofauti na ilivyo kawaida yao ya miaka nenda rudi.
Kabla ya uchaguzi huo CCM ilikuwa na mitaa 55 kwenye manispaa ya Bukoba, Chadema ilikuwa na mitaa 9 na CUF mitaa 2. Lakini baada ya uchaguzi wa mwaka huu CCM imeshuka chini mpaka kufikia mitaa 35 wakati Chadema ikipanda juu mpaka mitaa 29 na kuiacha CUF kwenye mitaa ileile 2. Hiyo inaonyesha kwamba wananchi wa manispaa ya Bukoba  wamedhamiria kufanya mabadiliko kwa kuuamini zaidi upinzani.
Jambo lingine ni kwamba, pamoja na wananchi kufanya maamuzi hayo katika mazingira magumu ya kusakamwa na vyombo vya dola, wananchi wa manispaa ya Bukoba wameonyesha imani yao kwa upinzani kwa kuhakikisha wanawaweka wajumbe wote wa upinzani katika baadhi ya mitaa ambayo waliamua kuwabakisha wenyeviti wa chama tawala. Mfano mmojawapo ni mtaa wa Pepsi, kata ya miembeni, katika eneo la Nyamkazi ambako mwenyekiti kachaguliwa wa CCM lakini wajumbe wake wote 5 wametoka Chadema.
Kinachosikitisha na kuonekana kinalandana na vitendo vya vyombo vya dola ninavyovielezea hapa ni kitendo cha mwenyekiti aliyechaguliwa katika mtaa wa Mtoni, kata ya Bakoba, manispaa ya Bukoba,  anayejulikana kwa jina la Felician Bigambo. Katika mtaa huo wananchi wameamua kumchagua yeye kuwa mwenyekiti kupitia CUF, lakini wajumbe wote 5 wamechaguliwa kutoka Chadema.
Mwenyekiti huyo ameapa waziwazi  kwamba kamwe hawezi kufanya kazi na wajumbe hao wa Chadema, ambao sio wa chama chake. Hiyo maana yake ni kwamba anapingana na maamuzi ya wananchi wa mtaa wake walioamua kuchagua kwa mtindo huo. Lakini badala ya kujiuzulu kwa vile hakubaliani na maamuzi hayo yeye anadai kwamba hataweza kujichanganya na wajumbe hao kuwatumikia watu wa mtaa wake!
Pamoja na wananchi wa mtaa wake kumuamini na kumuona anafaa kuwatumikia yeye hawaamini na ni kama anaona wananchi hao wa mtaa wake hawafai kwa lolote!
 Kwa upande mwingine mtu mmoja aliyechaguliwa kuwa mjumbe kupitia Chadema katika mtaa wa Pepsi, kata ya Miembeni iliyopo eneo la Nyamkazi hapa Bukona Mjini, Delifinus Lwabigene, anasema kwamba watu wa mtaa wake wameonyesha imani kwa Chadema kwa kuwachagua wajumbe wote toka chama hicho, isipokuwa mwenyekiti ndiye wamemtoa CCM kwa kuziamini juhudi zake binafsi za kuwatumikia watu wa mtaa huo wakiwa hawana imani kabisa na chama chake.
CCM imepata mitaa 35 katika manispaa ya Bukoba, ila mitaa hiyo iko katika maeneo ambayo wakazi wake wakijumlishwa pamoja bado idadi yao haifikii idadi ya wakazi wa mitaa 2 ya eneo linalojulikana kama Kashai. Eneo hilo la Kashai lina mitaa 9 ambayo yote imekombwa na Chadema.
Baada ya kutangazwa matokeo ya mtaa wa mwisho katika eneo hilo la Kashai wananchi kwa furaha waliamua kushangilia wakielekea kwenye ofisi ya Chadema ya manispaa ya Bukoba. Walikuwa kwenye magari, pikipiki, baiskeli na wengine kwa miguu. Walikuwa wameshika matawi ya miti kuonyesha kuwa wanachokifanya ni cha amani.
Lakini kwa kukasirishwa na matokeo hayo makamanda wa polisi wa manispaa ya Bukoba waliamuru polisi kuwafuatilia wana Chadema hao na baadaye kuwazunguka kwa mbele ili kuweka kizuizi kabla wana Chadema hao hawajafika ofisini kwao na kuwaamuru watawanyike kwa madai kwamba wamefanya maandamano bila kibali!
Wanachadema bila ubishi wakaamua kutawanyika, hata hivyo kutokana na wingi wao,  bado polisi wakatumia kigezo hicho kudai kwamba watu hao walikuwa bado wanaandamana. Kwahiyo wakaanza kupiga mabomu ya kutoa machozi!
Jambo linaloonyesha kwamba makamanda wa polisi hawakufurahishwa na matokeo ya Chadema kuibuka kidedea, ni kwamba hata katika maeneo yaliyochukuliwa na CCM wanachama wake walishangilia na kuandamana vilevile, lakini hatukuona polisi wakiwazuia wala kuwaingilia kwa namna yoyote ile. Isipokuwa kuwalinda na kuhakikisha furaha yao haiingiliwi na yeyote. Ni katika hali hiyo ambapo polisi wanakuwa tayari kufunga hata barabara ili wana CCM waonyeshe furaha yao!
Mimi nathubutu kusema kwamba matendo hayo yanayofanywa na chombo ambacho kipo kulinda usalama wa raia bila kujali itikadi zao, dini wala rangi zao, ni haramu. Ni kitendo cha kuanzisha vurugu, kitendo cha kuvunja amani ya wananchi na kuhatarisha usalama wao.
Wana Chadema, kama walivyo wana CCM na wafuasi wa vyama vingine, ni raia kama walivyo raia wengine wote. Vilevile ni wanadamu kama walivyo wengine wote. Wanaweza kufikia wakati wakakataa kuona haki zao zinapindishwa na watu walioajiriwa kuzilinda. Na hali inapokuwa hivyo kinachofuatia ni mapambano yanayoweza kuishia kwenye umwagikaji wa damu. Mapambano ya kujilindia haki.
Cha kuangalia ni kwamba wanaopaswa kuhakikisha matukio hayo hayatokei, polisi,  ndio wako msitari wa mbele kuhakikisha wanaanzisha hali hiyo ya upotevu wa amani. Katika hali ya kawaida jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa umakini uliopitiliza kama kweli tunatamani kuendelea kujivunia hali ya amani na utulivu.
Tusiwaachie polisi wakawatumie  wananchi na amani yao kama ngazi za kupandia kuyafikia maslahi yao binafsi. Polisi wanapoviangalia tu vyeo bila kujali vyeo hivyo wanavitumiaje na kwa manufaa ya nani,  basi ieleweke kwamba hayo ni maslahi binafsi. Wananchi hawawalipi polisi mishahara ili kuwaongezea nguvu za kuyasaka maslahi binafsi, wanawalipa ili wakawatumikie kwa kuwahakikishia usalama wao.
Usalama hauwezi kujitokeza kwa kuchokonoa hasira za wananchi, kwa kufanya mambo ya kuwakera wananchi ili polisi wakaonekane wazuri kwa wakubwa wao huku wananchi wakikandamizwa. Kwa maneno mengine ni kwamba usalama wa wananchi hauwezi kupatikana bila ya kutendeana haki.
Inawabaidi polisi wajifunze kutenda haki wa raia, vinginevyo Polisi itajikuta ni idara ya kuanzisha vurugu na kuipoteza amani ya nchi kinyume na inavyotarajiwa. Matokeo yake Tanzania itageuka kuwa kama nchi tunazodhani zimekumbwa na rahana ya Mwenyezi Mungu kumbe ni rahana ya kujitakia.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau