Bukobawadau

AIBU NYUMBA ZA WAKUBWA KUTUNZA MIHADARATI

Tanzania imekuwa katika vita ngumu ya kupambana na matatizo mbalimbali yanayoisumbua, yakiwamo ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa.
Katika baadhi ya nyakati, matatizo hayo yamegeuka kuwa kikwazo kwenye azma ya kuwapa maendeleo na ustawi wananchi.
Pamoja na matatizo hayo, siku za karibuni na pengine miaka michache iliyopita, biashara za dawa za kulevya imegeuka adui anayeichachafya nchi.
Kwa kiasi kikubwa, biashara hii ambayo inaonekana dhahiri kuwa inahusisha wengi, wakiwamo watu wazima na hata watoto na wengine vijana wasomi wazuri, imegeuka vita ambayo kama nchi ijihesabu kuwa imeshindwa kuidhibiti.
Hatuchelei kusema nchi yetu imeshindwa vita ya kupambana na biashara hii ya dawa za kulevya kutokana na kauli lukuki za baadhi ya viongozi wetu wa kisiasa wa ngazi mbalimbali pamoja na juhudi zinazofanyika kuhakikisha biashara hiyo inakomeshwa.
Ipo mifano michache ya jinsi ambavyo biashara hiyo imekuwa ikiendelea kuisumbua nchi yetu katika siku za karibuni na hata watu wake, ikisababisha ongezeko la vijana kugeuka watumiaji, wauzaji.
Tumeeleza awali kuwa Tanzania inapigana vita hii ikiwa kama tayari imeshindwa, hasa kwa kuzingatia ukweli kwamba baadhi ya viongozi wamekuwa wakituhumiwa kujihusisha nayo, lakini hawachukuliwi hatua zozote licha ya kuambiwa kuwa wanajulikana.
Ni bahati mbaya zaidi kuona kauli za baadhi ya viongozi wetu zikiendelea kusikika, zikiwataja wahusika wa biashara hii kuwa wanajulikana, lakini kwa nini hawakamatwi?
Bahati mbaya, baadhi ya vijana wetu ambao ni nguvukazi muhimu ndio watumiaji, wasafirishaji na hata wauzaji wa dawa hizo, huku baadhi yao wakikamatwa na wengine kuhukumiwa vifungo vya muda mrefu au kunyongwa nje ya mipaka ya nchi yetu.
Hukumu hizo chache kati yake zimefahamika, kuripotiwa kwenye vyombo vya habari nchini au nje ya mipaka ya nchi, lakini zinachafua, kutia doa jina zuri ambalo nchi yetu imejijengea kwa miaka mingi iliyopita. Inafaa viongozi watuambie, ni kwa nini kama nchi tumeshindwa kudhibiti biashara hii ya dawa za kulevya kama wahusika wanajulikana?
 Jeshi la Polisi, Kitengo cha Dawa za Kulevya wametueleza kuwa baadhi ya nyumba za wakubwa ndizo zinazotumika kama maficho au vichaka vya biashara hii.
Tunawaamini polisi, walilolisema ni kweli wanawajua wamiliki wa nyumba zile ambao ni wakubwa, lakini tunawauliza wamewachukulia hatua gani ili maficho au vichaka hivyo vya dawa kulevya yaondolewe?

Hakuna shaka, polisi wanaufahamu ukweli wa mtandao huo wa dawa za kulevya, viongozi au wakubwa waliojenga au kumiliki nyumba hizo, ambao hawaishi ndani yake bali wamezipangisha kwa wengine ambao wamezigeuza maficho ya biashara ya dawa za kulevya.
Kama hivyo ndivyo, tunawashauri kuwa badala ya kulalamika, wachukue hatua kwa mujibu wa Sheria ya Dawa za Kulevya, ambayo wanaikariri kuwa inawapa mamlaka ya kuwafikisha wahusika kwenye vyombo vya sheria ambako huchukuliwa hatua zikiwamo za kufungwa maisha au mali zao kufilisiwa.
Tunawashauri viongozi wetu wa kisiasa, vyombo vya dola au ulinzi na usalama wachukue hatua kukomesha tatizo hilo.
Tunadhani, kwa kufanya hivyo, wafanyabiashara wa dawa za kulevya kama ni wapangaji kwenye nyumba hizo za wakubwa, wabanwe wawataje wahusika ili mtandao huo uvunjwe.
CHANZO;MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau