Bukobawadau

JAMBO BUKOBA KUENDESHA BONANZA LA MICHEZO KWA SHULE ZA MSINGI MKOANI KAGERA 30 JANUARI, 2015

Jambo Bukoba ni Shirika lisilokuwa la Serikali linalofanya kazi mkoani Kagera kwa kushirikiana na serikali ya mkoa. Mwanzilishi wa Jambo Bukoba  anaitwa Bw. Clemence Mlokozi ambaye asili yake ni mkoani Kagera katika Wilaya ya Missenyi Kijiji Ishozi na anaishi nchini Ujerumani.
Ili kuleta umoja katika mkoa kwa watoto wa kike na kiume Jambo Bukoba kuanzia mwaka 2012 ilianzisha bonanza la michezo kila mwisho wa mwaka la kuwaunganisha watoto kutoka shule mbalimbali mkoani Kagera ili waweze kushirikiana pamoja kimichezo na kujenga kujiamini kwa pamoja.
Bonanza la michezo la Jambo Bukoba mwaka 2014 litafanyika mwaka huu 30 Januari, 2015 na kushirikisha Wilaya zote za mkoa wa Kagera  pamoja na mwanzilishi wa Jambo Bukoba akiambatana na wenzake kutoka nchini Ujerumani.
Bonanza la michezo  la Jambo Bukoba litafanyika  katika viwanja vya Gymkhana Manispaa ya Bukoba kuanzia saa 2:00 asubuhi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera ikishirikiana shirika la Jambo Bukoba wanawakaribisha wananchi wote kuhudhuria na kushiriki katika bonanza hilo.
Shirika la Jambo Bukoba chini ya mwanzilishi wake Bw. Mulokozi tangu kuanzishwa kwake mkoani Kagera  limekuwa likiwafunza watoto  katika shule za msingi  kila wilaya michezo midogo midogo ya kujenga ushirikiano wa pamoja hasa watoto wa kike kujiamini na  kushirikiana zaidi na wenzao wa kiume.

Jambo Bukoba katika kuhakikisha inapunguza unyanyapaa wa kuwatenga watoto wa kike katika jamii imeweza kueneza elimu kupitia michezo kwa watoto wote kushirikiana kwa pamoja bila kujali jinsia za watoto iwe katika masomo , michezo au katika shughuli nyingine za kijamii.
Shirika hilo pia hutoa vifaa vya michezo kama vile fulana na bukta za michezo, viatu na mipira  katika shule mbalimbali mkoani Kagera. Vilevile ili kuhakikisha watoto wanaendelea kupata elimu nzuri Jambo Bukoba imeanza kukarabati miundombinu mbalimbali katika baadhi ya shule za msingi mkoani hapa.
Miundombinu hiyo ni pamoja na madarasa ambayo yameharibika na kuhitaji ukarabati, kujenga matundu ya vyoo vipya pamoja na kukarabati ofisi za walimu ambazo ziko katika hali mbaya ili kuwarahisishia walimu katika kutekeleza majukumu yao vizuri ya ufundishaji.
Lengo  la mwanzilishi wa Jambo Bukoba Bw. Mulokozi ni kupunguza kasi ya watoto wa kike kuanzisha mahusiano ya kimapenzi wakiwa wadogo, pia  kupunguza unyanyapaa wa wtoto wa kiume kwa watoto wa kike ambapo Jambo Bukoba imepunguza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa mkoani Kagera.
Imeandaliwa na:
Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2014
Next Post Previous Post
Bukobawadau