Bukobawadau

MKUU WA MKOA WA KAGERA AHAIDI KUUTATUA MGOGORO WA MIAKA TISA KATI YA WANANCHI NA WAWEKEZAJI KATIKA KATA YA RUTORO WILAYANI MULEBA IFIKAPO MACHI 30,2015


Mgogoro wa ardhi kati ya wawekezaji na wananchi wa Kata ya Rutoro Wilayani Muleba Mkoani Kagera uliochukua takribani miaka tisa na kusababisha baadhi ya wananchi kupoteza maisha  na wengine kufungwa kwa kesi za mauaji, na wengine wakiwa mahabusu kwa kesi mbalimbali  sasa kupatiwa ufumbuzi na Mkuu wa Mkoa wa Kagera  John Mongella.

Mkuu wa mkoa  John Mongella alihaidi kuupatia ufumbuzi mgogoro huo katika mkutano wa hadhara alioufanya katika Kata ya Rutoro yenye vijiji vine vya Rutoro, Mishambya, Kyobuheke, na Byengeragere alipokutana na wananchi na wawekezaji wenye vitalu  katika Ranchi ya kagoma na kuzungumza nao pia kusikiliza chanzo cha mgogoro.
Katika mkutano huo wa hadhara uliofanyika tarehe 5/01/2015 Mkuu wa Mkoa alitoa muda mrefu wa kuwasikiliza wananchi wa kata ya Rutoro pamoja na wawekezaji  wenye vitalu vya kufugia kisasa walivyopewa mwaka 2006 na serikali ili kujua chanzo cha mgogoro na mizizi yake na kutafuta  ufumbuzi wa kudumu.
 Wakielezea chanzo cha mgogoro wananchi mbele ya  Mkuu wa Mkoa walisema ni kutokana na serikali kugawa vitalu kwa wawekezaji  ikiwemo ardhi yao ya vijiji, pia wakati vitalu hivyo vinagawiwa tayari wao wananchi  walikuwepo katika maeneo hayo na wawekezaji wamekuwa wakifukuza katika maeneo yao na kulisha ng’ombe katika mashamba yao.
Wananchi hao pia walisema kuwa tatizo kubwa ni wawekezaji kuwadharau hata serikali za vijiji na vitongoji wamekuwa hawathaminiwi na kuwaeleza kuwa wao kama wawekezaji wanaongea na viongozi wa serikali wa ngazi za juu na siyo serikali za vijiji.
Wananchi walimweleza RC Mongella  kuwa wamekuwa wakibambikiziwa kesi na Wawekezaji hao mara wanapolalamika kuwa mashamba yao yanaharibiwa na mifugo ya wawekezaji hao. Aidha wananchi wamekuwa wakichomea nyumba zao na kunyanganywa mifugo yao kuwa hawaruhusiwi kufuga isipokuwa wawekezaji tu, na kutishiwa na bunduki na walinzi wa wawekezaji pengine kuuwawa.
Wawekezaji nao walimweleza Mkuu wa Mkoa wa Kagera  kuwa wanaingiliwa katika vitalu vyao na wananchi kwa kuchochewa na wanasiasa hasa mbunge wa Muleba Kaskazini Charles Mwijage. Pia walisema kuwa wananchi  wa Rutoro tayari walishatengewa kitalu 291/2 ili kuwapisha wafanye shughuli zao za uwekezaji katika ufugaji.
Wawekezaji wanawatuhumu wananchi kuvamia vitalu vyao na kukatakata mifugo yao mapanga pia kuhamasishana  ili kuvamia wafanyakazi katika vitalu vyao na kuwaua kwa kuwapiga ama kuwajeruhi bila kufuata utaratibu wa haki na sheria katika mfumo wa serikali.
Kwa mujibu wa wananchi wanapendekeza, kuwa kwa kuwa serikali iligawa vitaliu kwa wawekezaji na wananchi  tayari wakiwa katika maeneo hayo wananpendekeza kuwa wawekazaji watengewe eneo lingine ambalo ni kitalu namba 291/2 kwa kuwa mali zao zinahamishika na kuacha maeneo ambayo tayari yanakaliwa na wananchi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau