Bukobawadau

TUNACHOHITAJI NI UFUMBUZI WA MATATIZO SIYO SAUTI NZURI

Na Assumpta Nalitolela
Nimeandika makala kadhaa zinazohusu huduma bora kwa wateja katika safu hii. Nalazimika kuandika tena leo kwa sababu kwa kweli maeneo mengi ya nchi hii huduma ni mbovu sana. Yapo mabadiliko katika maeneo machache ambayo yanaonyesha angalau watu wanatambua kuwa kuna ushindani katika biashara zetu hivyo wanatakiwa kutoa huduma kwa ushindani; hao nawapa hongera.

Watu wengi bado wanababaika ni namna ya kuhudumia kwa ushindani. Wapo wale ambao wanaamini kwamba kutabasamu, kusema karibu na nikusaidie nini ndio mambo ya msingi ya kumfanya mteja abaki kwenye biashara yako.

Ni kweli mambo hayo ni ya msingi lakini kama mteja hatatatuliwa tatizo lake lililomleta kwa mtoa huduma mambo hayo ya kutabasamu yanakuwa hayana maana. Ni bahati mbaya kwamba tabia za watoa huduma wetu wengi zinaonesha kuwa na fikra hii; na hii ni hatari kwa ustawi wa biashara. Tembelea maeneo mengi ya huduma hata zile za taasisi kubwa utayakuta hayo. mifano ifuatayo ni kielelezo cha malalamiko yangu.

Unakwenda kwenye taasisi kutaka kujua kitu fulani halafu unakutana na mtoa huduma ambaye ameandaliwa kujibu maswali yako lakini hana hata habari kwamba hicho unachotaka kukijua kipo kwenye taasisi yake.

Nakumbuka nilishawahi kwenda kwenye duka kubwa tuu nikitafuta moja ya vifaa vinavyoturahisishia shughuli zetu za jikoni. Nilikaribishwa vizuri sana na binti aliyekuwa katika duka hilo huku akionesha uso wenye tabasamu na ukarimu.

Hilo likaisha na mimi ninayejali sana huduma ninayopewa na wengine nikaridhika kwa hatua hiyo ya awali ya utoaji wa huduma.

Hata hivyo, nilipofika hatua ya pili sasa ya kupata ufumbuzi wa hicho kifaa cha jikoni nikakwama. Chombo kile kilikuwa tofauti na vile nilivyovizoea; kulikuwa na vifaa vya ziada ambavyo sikujua nitavitumiaje.

Nikaomba msaada kwa mhudumu wangu aliyenikaribisha vizuri sana lakini cha kusikitisha alikuwa hata hajui hicho kifaa ni cha nini.

Kwa kweli yale yote aliyoyafanya awali yakayeyuka katika kichwa changu kilichobakia ni maswali mengi ambayo mengine nilimuuliza hapohapo kwamba inakuwaje mtu anauza kitu asichokijua hata ni kitu gani. Kwa kweli nilikasirika. Nikashindwa kununua kifaa kile na kuondoka.

Jamani watanzania wenzangu ndio nini hii. Unajiitaje mtoa huduma kama hujui hata kama hicho unachokiuza? Kwa ufahamu wangu ni kwamba mtu muuzaji anapaswa kujua jina la bidhaa yake, inatumikaje, mambo kadha wa kadha yanayoambatana na bidhaa ile, bei yake. Unakwenda dukani eti mhudumu hajui bei ya bidhaa mpaka hapo atakapofika mtu anayejua; kwa nini mtu huyo auze bidhaa hiyo.

Aina nyingine ya wahudumu wanaonikera sana ni wale wanaotoa ahadi ambazo hawana hata uhakika kama watakuwa na uwezo wa kutekeleza.

Mfano hai nilionao katika kampuni moja ya simu ambayo nilipewa ahadi, hili ni ahadi ambayo nimekuwa nikipewa na watoa huduma wa kampuni ya airtel kwa kipindi cha zaidi ya mwezi moja lakini mpaka leo hii sijapata suluhisho.
Nilituma shilingi 20,000 kwenye kampuni hiyo nikitaka kuuziwa umeme, mpaka leo hii sijapata umeme na wala sijarudishiwa fedha.

Hiyo ilikuwa 11/1/2015. Nilishapata taarifa kwamba siku hiyo kulikuwa na matatizo katika mitambo ya Tanesco. Baada ya hapo nimekuwa nikipiga simu Airtel na kupokelewa na wahudumu ambao wanakukaribisha kwa sauti nzuri na baada ya kujieleza tatizo langu, wote wanasema “mama leo kuwa tu na amani utapata tuu umeme wako”.

Najua kabisa kwamba mimi ninapowapigia simu nao wanaulizia Tanesco ambako ndiko walikopeleka hela yangu ili nipate umeme, hivyo ufumbuzi wa suala hili upo mikononi mwa Tanesco. Nawapelekea wao malalamishi yangu kwa sababu fedha yangu ilipitia kwao. Siwashangai wahudumu hao kwa kushindwa kunipa umeme la hasha, ninawashangaa kwa kutoa ahadi ya kutekeleza kitu kwa siku hiyo hiyo wakati wanajua fika kwamba lazima wawasiliane na taasisi nyingine.

Hawa ni wahudumu ambao wanafikiria watamfurahisha mteja kwa kumwambia kuwa na amani. Kweli maneno hayo ni mazuri kuyasikia kwenye masikio ya mteja kama mimi lakini hayafanyi mimi kupata umeme au kurudishiwa fedha yangu. Ufumbuzi kwangu ni ama kupewa umeme au kurudishiwa fedha. Kwa hiyo tabasamu, maneno mazuri na ahadi hewa havinisaidii mimi katika kupata umeme na fedha.

Watoa huduma wa nchi hii watambue kwamba pale tunaposisitiza mtoa huduma kuwa na tabasam lenye mvuto, lugha nzuri, mavazi safi hatumaanishi kwamba hivi ndivyo vinavyotoa suluhisho kwa matatizo ya mteja hapana.

Ni lazima njia sahihi zitumike ili kupata ufumbuzi wa tatizo la mteja hapo ndipo tutakaposema umemtendea haki mteja wako.
MWANANCHI.
Next Post Previous Post
Bukobawadau