Bukobawadau

BODI YA PAROLE YA MKOA WA KAGERA YAZINDULIWA RAMSI KUSHUGHULIKIA WAFUNGWA WENYE MWENENDO MZURI MAGEREZANI


Bodi ya Parole ya Mkoa yazinduliwa rasmi Mkoani Kagera na Mkuu wa mkoa Mheshimiwa John Mongella na kupelekea bodi hiyo kukaa kikao chake cha kwanza cha kisheria  Mrchi 26, 2015 baada ya kuteuliwa rasmi na Waziri wa mambo ya Ndani ya Nchi ili kujadili wafungwa waliojirekebisha na kuonesha tabia na mwenendo mzuri gerezani.
Parole ni utaratibu au mfumo wa kumwachilia mfungwa kutoka gerezani baada ya kutumikia sehemu ya kifungo kwa imani kwamba mfungwa huyo hatatenda kosa tena, na kwamba atafuata masharti. Mfungwa huyo lazima awe ameonesha tabia njema na kujirekebisha kwa kipindi chote alichokaa gerezani.
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilaini

Katika uzinduzi huo wa Bodi ya Parole ya Mkoa Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Magereza  Mtiga H. Omary  alisema wajumbe wanne na Mwenyekiti walioteuliwa na Waziri wa Mambao ya Ndani watadumu katika nafasi hiyo kwa muda wa miaka mitatu kuanzia na tarehe 26/12/2014 hadi tarehe 26/12/2017.
Kamishina Mtiga aliwataja walioteuliwa na Waziri kuwa wajumbe wa Bodi ya Parole kuwa ni Askofu Methodius Kilaini (Mwenyekiti), na wajumbe ni Alhaji Haluna Kichwabuta (Manispaa ya Bukoba), Thepista Balagama (Biharamulo), Stella Ndyekobora (Karagwe) na Peter Emmanuel Buhiye (Missenyi).
Kamishina Mtiga pia alibainisha kuwa bodi za Parole  za Mkoa wa Mkoa wa Kagera zilizowahi kuwapo ni nne tangu mwaka  Juni 2003 aidha, bodi hizo kwa vipindi vya miaka mitatu mitatu ziliweza kukaa vikao 35 na wafungwa 370 walijadiliwa katika vikao hivyo, wafungwa 229 waliweza kuachiliwa kwa mpango wa Parole na Waziri wa Mambo ya Ndani ya nchi chini ya kifungu namba 6(4) cha sheria za Parole.
Akizindua Bodi hiyo ya Parole ya Mkoa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. John Mongella aliwasistiza wajumbe kuzingatia uadilifu, uaminifu, na umakini mkubwa katika utendaji wao wa kazi ili kutenda haki kwa wafungwa wanaoonesha mwenendo mzuri wakiwa magerezani.
Mhe. John Mongella aliwakumbusha wajumbe hao kutoshughulika na wafungwa ambao waliingia magerezani kwa makosa ya kuua wenzao kikatili au wale wote wanaojihusisha na kuwaua watu wenye albinism, ama kutowapendelea wafungwa ambao jamaa zao wana uwezo mkubwa wa kifedha na walitenda makosa ambayo hayawaruhusu kutoka kwa sheria za Parole.
Mwenyekiti wa Bodi ya Parole ya Mkoa wa Kagera Askofu Kilaini akitoa shukrani zake alisema atahakikisha yeye na wajumbe wake wanatenda haki  ili kulinda usalama wa jamii kule wafungwa hao wanakotoka na kuachiwa kurudi kuishi ili amani katika jamii isivurugike kwa kuisi kuwa mfungwa aliyeachiwa bado ni jambazi.
Bodi ya Parole ya Mkoa inaundwa na Mwenyekiti na wajumbe wanne wa kuteuliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mfawidhi wa serikali katika Kanda husika, Afisa Mwandamizi toka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mganga Mkuu wa Mkoa, Afisa Ustawi Mwandamizi Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, na wengine wanaoingia kwa nyadhifa zao ni Kamanda wa Polisi Mkoa na Mkuu wa Magereza wa Mkoa.
Changamoto kubwa inayoikumba Bodi ya Mkoa ya Parole ni Wananchi kutokuwa na uelewa mzuri juu ya sheria ya Parole, Sheria yenyewe kuacha wafungwa wengi ndani ya magereza, aidha jamii kuwa na mtazamo hasi juu ya wafungwa wanaoachiwa, pia jeshi la magereza kutokuwa na raslimali fedha kwenda vijijini kupata taarifa za wafungwa.
Next Post Previous Post
Bukobawadau