Bukobawadau

TAFITI ZA KUFANYIWA TAFITI


NA PRUDENCE KARUGENDO
IMEKUWA  kawaida kujitokeza taassisi mbalimbali zinazojifanya kuendesha tafiti kuhusu hali ya kisiasa hapa nchini wakati wa uchaguzi mkuu. Mara nyingi,  kama sio mara zote,  tafiti zinazofanywa zinalenga kutoa mwelekeo wa uchaguzi utakavyokuwa kwa maana ya ni mtu gani au chama gani kilicho kwenye mwelekeo wa kushinda uchaguzi.
Jinsi inavyoonekana tafiti hizi zinalenga kushawishi, kwa namna ya kampeni, badala ya kutoa mwelekeo wa halihalisi ilivyo. Katika kufanya hivyo tafiti hizi zinaonekana kuwapigia “debe” baadhi ya watu au vyama vya siasa kwa kuonyesha kuwa ndio au ndivyo vinavyopendelewa na wananchi walio wengi ambao ndio watakaofanya uamuzi katika uchaguzi mkuu unaokuja.
Mimi nadhani ipo haja ya kuzifanyia tafiti hizi taasisi zinazojitokeza kila uchaguzi mkuu unapokaribia. Nazo zifanyiwe utafiti ili kujua malengo yake na walio nyuma ya hizi taasisi za utafiti kutokana na tafiti zake mara nyingi  kuwa za utata.
Mfano katika Tanzania hakuhitajiki sayansi kubwa ili kujua nani atashinda hasa katika ngazi ya urais kulingana na hali halisi tuliyoizoea inayotokana  na sababu zilizo wazi.
Mojawapo ya sababu hizo ni kwamba uchaguzi wenyewe kwa hapa Tanzania haujakaa kisayansi kiasi cha kuufanya utoe picha halisi ya matakwa ya wapiga kura. Katika mazingira hayo ni vigumu kujitokeza mtu na kudai ametumia mbinu za kisayansi na kujua ni mtu gani anaweza kushinda au chama kipi kinaweza kushinda kwa maana halisi ya matakwa ya wananchi.
Mfano Tanzania, kama zilivyo nchi nyingi zinazoitwa za dunia ya tatu, ambako uchaguzi unafanywa tu kutimiza mazoea ili ionekane kwamba viongozi wa nchi husika wanatokana na matakwa ya wananchi, haijataka kuwa na vifaa vya kisasa vya kufanyia uchaguzi tangu kwenye ngazi ya uandikishaji wa wapiga kura. Na hilo sio jambo ambalo linaweza kuchukuliwa kama uduni wa nchi wa kutoweza kumudu vifaa vya aina hiyo, la hasha.
Tunayo mambo mengi ambayo wakati mwingine yanayazidi hata ya nchi zilizo na uwezo zaidi ya nchi yetu, japo mambo yenyewe si muhimu kama lilivyo suala hilo la vifaa vya kufanyia uchaguzi.
Mfano rais wetu anayo ndege ya kusafiria ya kisasa na ya gharama kubwa sana,  wakati waziri mkuu wa Uingereza anatumia ndege za abiria wa kawaida anapotaka kusafiri! Ikumbukwe nchi yetu inajiendesha kwa kutegemea zaidi hisani ya Uingereza na nchi za aina hiyo.
Lakini pamoja na kuonyesha ufahari wa namna ya kumtunza kiongozi wetu mkuu kuliko wanavyofanya Wangereza, bado nchi yetu inaona ugumu wa kumwezesha mwananchi kuonyesha matakwa yake halisi kwa kisingizio cha ufukara!
Tunabaki kufanya uchaguzi kwa njia za kubahatisha bila ya uhakika wa ni namna gani mtu anaweza kuthibitisha matakwa yake, kamchagua nani na kumuacha nani. Sababu vifaa vya kutupatia uhakika huo hatuna. Katika mazingira ya aina hiyo ambayo mpiga kura hawezi kuwa na uhakika kama alichokikubali ndicho kilichoonyeshwa mtu wa pembeni anawezaje kutafiti mpaka akajua mpiga kura atamtaka nani na kumuacha nani?
Fikiria katika mazingira ambayo idadi ya wanaojitokeza kupiga kura wakati mwingine haifiki nusu ya waliojiandikisha kupiga kura, inawezekanaje mtu atafiti na kutoa mwelekeo wa uchaguzi ulio sahihi?
Mara nyingi tumeshuhudia matokeo ya kura yakichezewa kadri ya wasimamizi wa vituo vya kupigia kura wanavyotaka, kitu ambacho hakitoi taswira ya kweli ya uchaguzi husika. Tumeona aliyeshinda akionekana ameshindwa na aliyeshindwa akionekana ndiye kashinda! Hiyo ni  kutokana na kutokuwa na vifaa vya kuzuia uovu wa aina hiyo!
Hizo ni kura halisi za uchaguzi unaofanyika chini ya usimamizi na ulinzi, inawezekanaje sasa utafiti usio na usimamizi wala ulinzi ndio utoe matokeo yaliyo sahihi kiasi cha wananchi kukubaliana nayo kuwa ni ya kweli?
Kitu kingine kilicho kigumu katika kuzifanya tafiti hizi zisiaminike ni mazoea waliyo nayo Watanzania ya kutofanya tathimini kabla ya kufanya maamuzi. Kwahiyo ugumu unakuwa kwamba huwezi kujua mtu ambaye hafanyi tathimini ataamua nini kesho baada ya leo kuonyesha msimamo fulani. Watanzania walio wengi wamezoea kufanya maamuzi kwa kitu kilichowafurahisha kwa wakati huo na dakika hiyo, hata kama kitu chenyewe hakionyeshe mustakabali wa siku kumi zijazo!
Mfano mwaka 2005 Watanzania walitokea kumpenda Kikwete aliyeonyesha mvuto wa aina yake, naye kwa kuutumia mvuto huo aliokuwa nao kwa wananchi akawapa wananchi ahadi za ajabu akimalizia na maisha bora kwa kila mwananchi, hiyo ilikuwa zawadi aliyowapa wananchi waliotokea kumkubali kwa wingi. Na kweli,  kwenye uchaguzi mkuu akapata ushindi wa kishindo ambao wengine walisema ni wa kimbunga.
Lakini  baada ya miaka 5 hatukuyaona maisha bora kwa kila mwananchi. Kikwete akaongezewa miaka mingine mitano japo kwa kusuasua, yeye akazidi kuwapa matumaini wananchi kwa kuongeza ahadi, mpaka sasa anapoelekea kumaliza miaka 10 ya kipindi chake cha kukaa Ikulu ni mafanikio gani yanayoweza yakaakisi mvuto  aliokuwa nao kwa Watanzania? Je, ni kweli kila Mtanzania anayo maisha bora yaliyoahidiwa?
Baada ya kuangalia namna Watanzania walivyo wagumu kufanyiwa tafiti zinazoonyesha msimamo na mwelekeo wao kisiasa,  sasa tuangalie namna tafiti zenyewe zinavyofanyika.
Maranyingi tafiti hizi zinatoa takwimu ambazo zinaonekana ni za kubuni au kuhisi, sababu hazionyeshi zilikofanyikia. Kila mtu anaweza kujiuliza ni lini amewaona watafiti wakimuuliza kuhusu masuala ya uchaguzi kwamba ni chama gani au mtu gani anayetaka kumpigia kura. Kama hakuna aliyewaona tuseme hizo tafiti zao wanazifanyia wapi?
Hii inaweza kutuleta kwenye hitimisho la kwamba tafiti hizi zina malengo fulani kwa watu au vikundi fulani ikiwa ni njia mojawapo ya kuwashawishi wananchi wavifikirie vikundi hivyo au watu hao kwa maana kwamba ndivyo,  au ndio,  walio kwenye uwezekano wa kukubalika. Hizo ni kama njama tu kwa mtazamo wangu. Tafiti za kinjama.
Utafiti kuhusu matakwa na maamuzi ya Watanzania ni vigumu kufanyika katika hali ya sasa waliyomo Watanzania. Hii ni hali ya kubahatisha tu ambapo mambo hayawekwi wazi kwa makusudi mazima kwa hofu ya uwazi huo kuleta matokeo yasiyopendeza kwa baadhi ya watu. Kwa mantiki hiyo ni lazima matokeo yanayopatikana kwenye tafiti hizo yawe ya kubahatisha vilevile ambayo hayapaswi kutiliwa maanani.
Kinachoshadidia mawazo yangu haya ni kama hiki; niliamua kufanya utafiti binafsi katika maeneo ya vijijini ambako watu hawajali suala la kutathimini mambo, nikawapata watu kama 100 na kuwauliza ni chama gani wanakitaka kati ya CCM na Chadema,  wakanijibu tofauti na swali langu lilivyokuwa. Wao walisema wana kiu, kama nataka kuuliza maswali yangu kwanza niwapoze kiu. Nikajitutmua na kuwapa kinywaji.
Baada ya kupata kinywaji wakawa wanatafuta jibu la kunifurahisha, nao wakaniuliza, kwani wewe ni chama gani? Nikawajibu CCM, wakacheka na kusema sasa unawezaje kutuuliza habari ya Chadema wakati unaelewa kuwa hapa miaka nendarudi sisi tunaijua CCM tu? Nilipowambia kuwa huu ni wakati wa vyama vingi vya siasa na nimeishahamia Chadema papo hapo wote wakageuka wakawa Chadema, wakisema walikuwa wananipima tu!
Kwa mtindo huo umawezaje kusema umefanya utafiti na kujua ni chama gani au mtu gani anayekubalika kwa wananchi wa aina hiyo?
Tafiti za aina hiyo zinafanyika na kufanikiwa katika nchi ambazo chaguzi zinaakisi matakwa halisi ya wapiga kura. Kama tunataka kuziiga tafiti hizo basi tuanze kuiga namna ya kufanya kitu cha kweli, kwa maana ya kuhakikisha kwamba matakwa ya wananchi yanakuwa ya kweli bila kupindishwa.
Mfano wa wazi ni wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1995.  Katika mkoa wa Dar es salaam wananchi walikuwa wamedhihirisha kukikubali chama cha upinzani cha NCCR- Mageuzi. Ikaonekana kwamba majimbo yote ya Dar es salaam yangekwenda kwa chama hicho. Kilichofuatia ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuuvuruga kwa makusudi uchaguzi katika mkoa wa Dar es salaam na baadaye kutangaza kuwa utarudiwa baada ya muda fulani. Uliporudiwa mambo yakabadilika!
Sababu zilizotolewa na Tume ya Uchaguzi hazikuwa na pahala pa mashiko. Sababu haiwezekani uchaguzi ukaenda vizuri sehemu za Karagwe, mpakani mwa Tanzania na Uganda na Rwanda, zaidi ya kilometa 1500 toka makao makuu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, halafu uchaguzi huohuo uvurugike kwa kutotimia vifaa vya uchaguzi maeneo ya Mtaa wa Shabani Robert, hatua chache toka ofisi za Tume ya Uchaguzi.
Nihitimishe kwa kusema kwamba tafiti hizi kuhusu uchaguzi zingekoma kuliko kuendelea kuwapotosha wananchi kwa kuwaelekeza na kuwashawishi namna ya kufanya uchaguzi. Wananchi waachwe wachague wanavyoona wao inafaa kwa sababu mambo yote ni ya kubahatisha tu.
0784 989 512Next Post Previous Post
Bukobawadau