Bukobawadau

KATIKA KUMBUKUMBU:MJUWE MAREHEMU LUTENI JENERALI MAYUNGA 1940-2011

Itakumbukwa Novemba mosi, 1978, majeshi ya aliyekuwa Rais wa Uganda, Idi Amin yalivamia Mkoa wa Kagera. Uvamizi huo ulimsukuma Mwalimu Nyerere kuashiria ushindi kabla vita kuanza.

Nyerere aliashiria ushindi kabla vita kuanza akisema; “sababu ya kumpiga tunayo, nia ya kumpiga tunayo na uwezo wa kumpiga tunao.” Hakika, kauli hii ilihitaji si tu risasi za kutosha, mizinga au makombora na silaha za kila aina kuisimamia, bali mashujaa wa mstari wa mbele vitani.
Miongoni mwa wapiganaji waliotwikwa dhima hiyo nzito ni pamoja na Luteni Jenerali Silas Mayunga, sambamba na wapiganaji wote wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Watanzania kwa ujumla, waliotoa ng’ombe hata kuku kulisha wapiganaji uwanja wa mapambano.
Mstari wa mbele katika uwanja wa vita, Luteni Jenerali Silas Mayunga na wenzake, kazi ilikuwa moja tu-kufa au kupona ili kulinda si tu hadhi ya Tanzania, heshima ya wapenda haki duniani.

Ni vita hii ya Kagera ndiyo inayotajwa kumtambulisha zaidi Luteni Jenerali Mayunga ndani ya JWTZ na Jeshi la Uganda. Vita hiyo ilimpambanua ni mpiganaji wa aina gani akiwa mstari wa mbele.

MAYUNGA;Safari yake kijeshi imegusa nchi za Israel na Canada, akihitimu mafunzo ya kijeshi Julai 26, mwaka 1963 nchini Israeli na miaka 10 baadaye (1973), akafuzu kozi ya unadhimu na ukamanda wa jeshi nchini Canada. Kozi ya Ukamanda wa Juu wa Jeshi alihitimu mwaka 1974 nchini.

Juni 21, mwaka 1995, ni siku ambayo Mayunga alijiwekea rekodi binafsi ya kushika cheo cha juu jeshini, akipandishwa cheo kuwa Luteni Jenerali na miezi sita baadaye (Desemba 31, 1995) alistaafu.
Mti mkavu akiwa jeshini

Mayunga ni kamanda kiongozi. Amekuwa Mkurugenzi wa Mafunzo makao makuu ya jeshi, Kamanda wa Brigedi ya 202 ya Tabora, na Kamanda wa Divisheni za 20 na 30 za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Huwezi kuzungumzia Operesheni Chakaza wakati wa vita dhidi ya majeshi ya Idi Amin bila kumtaja kiongozi wa operesheni hiyo ambaye ni Luteni Jenerali Mayunga.

Katika Operesheni Chakaza, Mayunga ndiye aliyekuwa Kamanda wa Brigedi ya 206. Ndani ya Jeshi la Uganda Mayunga ana historia muhimu. Amekuwa Kamanda wa Kikosi Maalumu cha JWTZ nchini Uganda kati ya 1979 na 1980.

Lakini ukiondoa pilikapilika za kijeshi, Mayunga amekuwa Mkuu wa Mkoa Singida mwaka 1977 – 1978, Balozi wa Tanzania nchini Nigeria mwaka 1989 hadi 1998 na Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia Kongo (DRC) 1998 na 2002, alipostaafu.
 Mayunga alizaliwa Maswa, Shinyanga, mwaka 1940
  Luteni Jenerali Silas Mayunga, alifariki  Agosti 5, 2011 nchini India hakufa kwa risasi, mizinga wala milipuko yoyote pengine kama familia yake ilivyohofia kipindi yupo vitani bali alikufa akiwa kitandani wakati wa matibabu
Ewe Kamanda Mayunga tunakulia ,tunasikitika kwa kifo, lakini tunafurahi umetimiza wajibu.

Mungu ibariki Tanzania, Mungu ibariki Afrika
Next Post Previous Post
Bukobawadau