Bukobawadau

WASIFU WA MAREHEMU LUTENI KANALI BENEDICTA KITENGA

Marehemu Lt.Col.(Mst) Benedict Kulikila Kitenga 

OFISI YA MKUU WA MKOA WA KAGERA
TANZIA

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Kagera inasikitika kutangaza kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mhe. Lt. Col. Benedict Kulikila Kitenga aliyefariki tarehe 20.04.2015 katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili.
Marehemu Lt.Col.(Mst) Benedict Kulikila Kitenga alizaliwa mnamo tarehe 15.06.1953 Ifakara Wilayani  Kilombero katika  Mkoa wa Morogoro.
ELIMU.
Marehemu Lt. Col. (Mst) Benedict Kulikila Kitenga alisoma  shule ya Msingi Mafimba  Wilaya ya Ulanga Mkoani Morogoro na kuhitimu darasa la nne 1963, aidha alifaulu na kujiunga na darasa  la tano shule ya Ilete Middle School iliyoko katika Wilaya ya Ulanga na kuhitimu mwaka 1970. 

Baada ya hapo marehemu alijiunga shule ya Sekondari Galanosi iliyoko Mkoani Tanga na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1974.
Mafunzo mengine aliyoyapata marehemu wakati wa uhai wake ni mafunzo ya awali ya Uhandisi nchini Pakistani mwaka 1978.  Vile vile marehemu alipata mafunzo ya Diploma ya uhandisi nchini Ujerumani  mwaka 1999.
KAZI ALIZOWAHI KUFANYA.
Wakati wa Uhai wake marehemu aliweza kufanya kazi kama Mwanajeshi katika Jeshi la Wananchi Tanzania na kuweza kupanda vyeo hadi kufikia Cheo cha Luteni Kanali.  Aidha akiwa katika Jeshi la Wananchi Tanzania alikuwa; Mkuu wa kikosi Songea, Mkuu wa kikosi Ngerengere, Mkuu wa mafunzo IMT-Monduli Mkoani Arusha.
Mwezi Machi, 2009 marehemu Lt. Col. (Mst) Benedict Kulikila Kitenga aliteuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mlisho Kikwete kuwa Mku wa Wilaya Rorya iliyoko Mkoani Mara ambapo alifanya kazi hadi tarehe 08 Machi, 2012 alipohamishiwa katika Mkoa wa Kagera Wilaya mpya ya Kyerwa.

USHIRIKI WAKE KATIKA SHUGHULI ZA KITAIFA.
Marehemu Benedict Kulikila Kitenga alishiriki vita ya Operesheni Zimbabwe, Vita ya Operesheni Kagera na Vita ya Operesheni Chakaza.
Akiwa Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa yafuatayo ni machache kati ya mengi aliyoyafanya; Alikuwa Mwanzilishi wa Wilaya Mpya ya Kyerwa mwaka 2012, Alisimamia utekelezaji wa mradi wa Umeme vijijini, na Aliimarisha mahusiano mema kati ya nchi jirani za Rwanda na Uganda.
Aidha Marehemu Kitenga alisimamia na kuinua uchumi wa wananchi wa Wilaya ya Kyerwa. Alikuwa mchapakazi hodari  na aliweza kusimamia na kupambana na wimbi la magendo ya kahawa na bati, pia alikuwa ni kiungo mahususi kati Serikali Kuu na Halmashauri ya Wilaya, na alikuwa kiongozi mwepesi, aliweza kutoa huduma wakati wowote.

UGONJWA HADI MAUTI
Marehemu Lt. Col (Mst) Benedict Kulikila Kitenga alianza kuugua siku ya Jumanne tarehe 14/04/2015 akiwa anasumbuliwa na maumivu ya moyo na miguu na tarehe 15/04/2015 Jumatano jioni alilazwa katika hospitali Teule ya Nyakahanga iliyoko katika  Wilaya ya Karagwe.

Kutokana na hali yake kutokuwa nzuri siku hiyo hiyo  Jumatato usiku wa  saa 6.00 ililazimika kuhamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera lakini hali yake iliendelea kutokuwa nzuri ndipo tarehe 16/04/2015 siku ya Alhamisi alipewa rufaa na kupelekwa katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam ambapo alikuwa akiendelea na matibabu hadi mauti yaliyomkuta hapo tarehe 20/04/2015 saa 9.15 alasiri kutokana na shinikizo la damu na kupooza.

SHUKRANI
Kwa niaba ya Uongozi wa Mkoa wa Kagera, napenda kutoa shukrani kwa madaktari na Wauguzi wa Hospitali Teule ya Nyakaanga – Karagwe, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Dar es Salaam kwa jitihada kubwa walizozifanya kuokoa maisha yake.

Mwisho kwa masikitiko makubwa napenda kutoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na wananchi wa Wilaya ya Kyerwa na Mkoa wa Kagera kwa ujumla, kutokana na msiba huu mkubwa.

Bwana Ametoa, Na Bwana Ametwaa jina Lake Lihimidiwe.
AMEN.
 
Next Post Previous Post
Bukobawadau