Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dr. Margaret F. Chan amemteua Dr.
Winnie Mpanju-Shumbusho kutoka Tanzania kuwa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa
Shirika la Afya Duniani, upande wa masuala ya Ukimwi, Kifua Kikuu
Malaria na Magonjwa yaliyosahaulika.
Uteuzi huu umetangazwa
rasmi na Dr. Chan wakati wa kikao cha 68 cha Baraza Kuu la Shirika la
Afya Duniani kilichoanza tarehe 14 mpaka tarehe 26 Mei 2015, Geneva, Uswisi.
Dr. Mpanju-Shumbusho ni mtaalamu na kiongozi mwenye uzoefu wa zaidi ya
miaka 30 katika ngazi za juu za uongozi katika sekta ya Afya na
Ushirikiano wa Kimataifa.
Kabla ya uteuzi huu, Dr.
Mpanju-Shumbusho alikuwa Naibu wa Mkurugenzi Mkuu Msaidizi ndani ya
Shirika la Afya Duniani upande wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na
Magonjwa yaliyosahaulika na akiwa na cheo cha Ukurugenzi wa Idara
inayoshughulikia Ushirikiano wa Shirika la Afya Duniani na Mfuko wa
Dunia wa kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (Global Fund to
Fight AIDS, Tuberculosis na Malaria). Dr. Mpanju-Shumbusho pia ni
mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani kwenye Bodi ya Mfuko wa Dunia wa
kupambana na Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria na Bodi mbalimbali za
kimataifa.
Hapo awali, Dr. Winnie Mpanju-Shumbusho alikuwa
Mkurugenzi wa Idara ya kudhibiti Ukimwi na magonjwa mengine husika
katika ya Shirika la Afya Duniani (WHO), makao makuu Geneva, Uswisi.
Kabla ya kujiunga na Shirika la Afya Duniani, amewahi kuwa Mkurugenzi
Mkuu wa East, Central and Southern Africa Health Community Secretariat
yenye makao makuu yake, Arusha, Tanzania. Vilevile, aliwahi kuwa Mkuu wa
Idara na Mhadhiri Mwandamizi, Idara ya Afya ya Jamii na Mgonjwa ya
Watoto, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (Muhimbili University of Health
Science). Katika wadhifa huu, Dr. Winnie pia alikuwa mwanzilishi wa
mipango mbalimbali ya Afya na taaluma na Mshauri Mkuu wa Wizara ya Afya,
Tanzania upande wa Afya ya Jamii. Pia amewahi kuwa mjumbe wa Bodi
mbalimbali za kimataifa.
Dr. Mpanju-Shumbusho ana Shahada ya
Udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam; vilevile ana Shahada ya
Uzamili katika Afya ya Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Tulane, Marekani na
Shahada ya Uzamili katika Medicine (Paediatric and Child Health) kutoka
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, vilevile ana Shahada ya Uzamifu na Shahada
nyingine mbalimbali.
Akiwa Mkurugenzi na mtaalamu katika
Shirika la Afya Duniani, amekuwa mstari wa mbele katika kuandaa,
kuongoza na kutekeleza mipango mkakati ya Dunia ya kujenga na kuimarisha
sekta ya Afya hususani katika nchi maskini na zile zinazoendelea.
Mipango hii imezaa mafanikio makubwa ikiwemo kujenga uwezo wa nchi
maskini kukabiliana na maradhi ikiwemo pia afya za kina mama na watoto.
Sambamba na hilo, mipango hii pia ilifanikisha upatikanaji wa madawa ya
gharama nafuu katika nchi maskini ili kuweza kumudu gharama za matibabu
kwa watu maskini. Nchini kwetu, Dr. Mpanju-Shumbusho ameweza
kufanikisha upatikanaji wa matibabu na huduma nasaha za kusaidia
kudhibiti ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu, Malaria na magonjwa
yaliyosahaulika.
Dr. Shumbusho ameolewa na ana watoto wawili, wa kiume na kike.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comment:
Post a Comment