Bukobawadau

HOTUBA YA MSEMAJI MKUU WA KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI KATIKA WIZARA YA AFRIKA MASHARIKI MHE. JOSEPH ROMAN SELASINI (MB), AKIWASILISHA BUNGENI MAONI YA KAMBI YA UPINZANI KUHUSU BAJETI YA WIZARA YA AFRIKA MASHARIKI KWA MWAKA WA FEDHA 2015/2016Inatolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 99(9) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Mwaka 2013
____________________________

1.   UTANGULIZI
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii, kwanza, kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia afya njema na kuniepusha na dhoruba mbalimbali katika shughuli zangu za kibunge na kijamii. Pili napenda kuchukua nafasi hii kueleza masikitiko yangu kutokana na matusi, kashfa na kejeli zinazotolewa kwa wananchi wa jimbo langu kwenye vyombo vya habari, mitandao ya kijamii na mbaya zaidi hata ndani ya Bunge hili tukufu.

Mheshimiwa Spika, dharau na kejeli hizi zilitokana na kauli ya Mkuu wa Wilaya ya Rombo Lembris Kipuyo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rombo Anthony Tesha kwamba wanaume katika Jimbo langu hawana nguvu za kiume kutokana na ulevi uliokithiri na hivyo kuwafanya akina mama wa Rombo kukodisha wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kuwapatia huduma hiyo. Kauli hii iliyotokana na baadhi ya wananchi kuhojiwa na kutoa maoni yao kuhusu hali ya ulevi jimboni; imechukuliwa visivyo kwa kuwajumuisha wananchi wote.

Mheshimiwa Spika, vita dhidi ya ulevi uliokithiri na matumizi ya pombe zisizo na viwango ilianzishwa na Mhashamu Baba Askofu Isaack Amani wa Jimbo Katoliki la Moshi mwaka 2010 alipoandika waraka maalum kwa parokia zote Jimboni Moshi Rombo ikiwemo kuwakemea na kuwakataza waumini na wananchi wote kutojihusisha na ulevi uliokithiri wa pombe zisizo na viwango. Na kwa kipindi chote hicho mimi kama Mbunge wa Jimbo la Rombo nimekuwa nikiunga mkono na nitaendelea kuunga mkono jitihada hizo za Baba Askofu, Mapadre, Wachungaji na Mashehe  katika vita hiyo.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Serikali ya Wilaya ya Rombo, ikiongozwa na Mkuu wa Wilaya, ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama haikuwahi kuchukua hatua yoyote madhubuti kushirikiana na viongozi wa dini katika vita hiyo zaidi ya udhalilishaji tuliousikia katika wiki hii ndani ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Rombo inayoongozwa na CCM kwamba wanaume hawana nguvu za kiume na wanawake wanakodisha wanaume nchi jirani ya Kenya.

Mheshimiwa Spika, Serikali ndiyo inayotekeleza sheria ya vileo, biashara na uhamiaji na vyombo mbalimbali vya udhibiti wa ubora kama TBS na TFDA na viko chini yake. Serikali inashindwa vipi kutekeleza sheria hizo au kutumia vyombo vyake na badala yake inawatukana na kuwadhalilisha wananchi. Napenda kumalizia utangulizi wangu kwa kulaani udhalilishaji huu na kwamba wananchi wachache waliohojiwa na vyombo vya habari katika Kijiji kimoja na kitongoji kimoja cha  Kikelelwa alikozaliwa na anakoishi Mwenyekiti wa Halmashauri ya Rombo na ambako ndiko Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya walikotembelea hakiwezi kuchukuliwa kama kielelezo cha taswira ya udhaifu  kwa  Wilaya nzima ya Rombo yenye kata 28, vijiji 68 na vitongoji 311.

Mheshimiwa Spika, nitaendelea kuunga mkono jitihada za Baba Askofu Isaack Amani na Kanisa kuwashauri waumini na wananchi kwa ujumla kunywa pombe zilizothibitishwa ubora wake, kunywa kwa kiasi, kunywa kwa wakati unaokubalika kisheria na au kutafuta vinywaji vingine  badala ya vileo.

Mheshimiwa Spika baada ya kusema hayo napenda pia kuchukua nafasi hii kuupongeza UKAWA chini ya uongozi shupavu wa Mhe. Freeman Aikaeli Mbowe (Mb) ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, kwa kazi kubwa ya kuwahamasisha wananchi kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura ili wawe na sifa ya kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2015. Ni matumaini na matarajio ya wananchi kwamba Upinzani unakwenda kushinda katika uchaguzi huo na kuunda Serikali na hivyo kubadili maisha ya watanzania ambao wamedanganywa na kufanywa maskini tangu tupate uhuru miaka 53 iliyopita.

Mheshimiwa Spika, napenda pia kutumia nafasi hii, kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutoa pole kwa majirani zetu wa Kenya kwa tukio la uvamizi wa  kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa tarehe 2 Aprili, 2015  ambapo wanafunzi 147 walipoteza maisha na wengine 79 kujeruhiwa vibaya.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inalaani mauaji ya Kiongozi wa chama cha Upinzani cha Union for Peace and Development (UPD) nchini Burundi, Zedi Feruz. Kiongozi huyu aliuwawa kwa kupigwa risasi yeye na mlinzi wake na watu wasiojulikana nyumbani kwake mjini Bujumbura

Mheshimiwa Spika, sote tunatambua kwamba kuna machafuko ya kisiasa nchini Burundi, na machafuko hayo yanatuathiri pia sisi watanzania kwa kuwa wakimbizi kutoka Burundi  zaidi ya 70, 000 wapo nchini kwetu. Burundi ni nchi  tuliyopakana nayo na ni nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Rais wa  Tanzania kwa sasa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni jitihada gani  Tanzania inafanya kama Jirani wa  nchi ya Burundi lakini pia kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya  Afrika Mashariki ili kuleta utulivu na amani Burundi?  Na ni namna gani Tanzania inasaidiwa na nchi za Jumuiya ya Africa Mashariki kubeba mzigo wa wakimbizi walioingia nchini.

2.    ULINZI NA USALAMA KATIKA JUMUIYA

Mheshimiwa Spika katika hotuba yangu kuhusu bajeti ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2014/15 nilieleza jinsi Jumuiya Afrika Mashariki inavyokabiliwa na tishio kubwa  la ugaidi. Ukiacha matukio makubwa ya kigaidi ya Garissa na West Gate, kumekuwa na matukio mengi madogomadogo ya kigaidi nchi Kenya na Uganda.

Mheshimiwa Spika Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inatambua umuhimu wa kuimarisha Ulinzi na Usalama ndani ya Jumuiya kwa sababu inatambua kwamba  hata Tanzania haipo salama kutokana na kuzungukwa na majirani ambao ni wahanga wa matukio ya kigaidi.

Mheshimiwa Spika, kutokana na  kuongezeka kwa vitendo vya kigaidi na kiharamia duniani na kuongezeka kwa  aina mbalimbali za uhalifu mataifa mbalimbali duniani yamebuni mbinu mbalimbali za kiulinzi ikiwa ni pamoja na kuanzisha mashirikiano baina ya nchi na nchi kuhusu namna ya kujilinda na kujihami dhidi uvamizi au uhalifu unaoweza kujitokeza katika nchi moja au ukanda ambao uko katika ushirikano.

Mheshimiwa Spika, kwa muktadha huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliunga mkono Azimio la Bunge la Kuridhia Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya Ushirikiano katika Masuala ya Kiulinzi (The East Africa Protocol on Cooperation in Diffence Affairs) lililopitishwa na Bunge tarehe 21 Novemba, 2014.
Mheshimiwa Spika, pamoja na kuunga mkono azimio hilo, Kambi Rasmi ya Upinzani ilitoa ushauri ufuatao:
                                                        i.            Kutotumia kivuli cha iitifaki hiyo kuitetea au kuilinda Serikali yoyote ya nchi zilizoridhia itifaki hiyo ambayo itakataliwa na wananchi wake. Kambi Rasmi ya Upinzani ilisisitiza kwamba Azimio hilo  lisiwe kinga kwa Serikali ambazo zitakuwa zimekataliwa na wananchi wake.
                                                      ii.            Nchi zilizoridhia itifaki hiyo zisishiriki katika ukandamizaji wa wa raia wa nchi zao au nchi nyingine halafu zikategemea kupata ushirikiano wa kiulinzi kutokana na itifaki hiyo.
                                                    iii.            Utatuzi wa migogoro utumie njia ya mazungumzo ya kidiplomasia  zaidi kuliko kutumia nguvu za kijeshi ili itifaki hiyo ifikie malengo yaliyokusudiwa na iwe na manufaa ya kuduma katika nchi zilizoiridhia.
                                                  iv.            Kupitia mara kwa mara taarifa za makubaliano ya Azimio hilo na utekelezaji wake ili kuhakikisha hakuna mabadiliko hasi ya Azimio hilo kulingana na wakati.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili imetekeleza vipi Itifaki ya Jumuiya ya Afrika Mashariki juu ya Ushirikiano katika Masuala ya Kiulinzi katika kuisaidia nchi ya Kenya ambayo imekumbwa na madhila ya mashambulizi ya kigaidi?
Mheshimiwa Spika, machafuko yanayoendelea nchini Burundi hivi sasa yanaashiria kuwa Serikali ya Burundi haiungwi mkono na wananchi wa Burundi. Zipo taarifa kwamba wakati wa jaribio la Mapinduzi nchini humo Rais wa Nchi hiyo Pierre Nkurunzinza alikuwa Tanzania, na baada ya jaribio la Mapinduzi kushindwa, Serikali ya Tanzania ilimsaidia kurudi Burundi. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama ni mpango au sera ya Serikali ya Tanzania kuzisaidia Serikali zinazokataliwa na wananchi wake kuendelea kubaki madarakani kimabavu.
3.   BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI (EALA) NA MCHAKATO WA UCHAGUZI WA WABUNGE WA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikiulalamikia mchakato wa kibaguzi wa uchaguzi wa wabunge wa Afrika Mashariki uliofanywa na Bunge letu tarehe 17 Aprili, 2012.

Mheshimiwa Spika, msingi wa malalamiko hayo ulitokana na ukiukwaji wa Kifungu cha 50(1) cha Mkataba wa Jumuiya ya  Afrika Mashariki kinachotoa mwongozo wa namna ya kuwapata wawakilishi katika Bunge la Afrika Mashariki.  Bunge la Tanzania, ama kwa makusudi au kwa kutoelewa matakwa ya Mkataba wa Jumuiya, liliweka mfumo wa kibaguzi katika  uchaguzi wa wabunge wa EALA katika bunge letu ambao hautoi fursa kwa vyama vya upinzani kupata uwakilishi.  

Mheshimiwa Spika, Kutokana na hali hiyo, aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Ubunge wa Afrika Mashariki  kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo Ndugu Anthony Calist Komu, alifungua kesi katika Mahakama ya Afrika Mashariki dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu ukiukwaji wa Mkataba wa Afrika Mashariki katika kuwachagua wabunge wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Afrika Mashariki ya tarehe 26 Septemba 2014, Ndugu Anthony Komu ameshinda kesi hiyo jambo linalothibitisha kwamba haki haikutendeka, lakini baya zaidi ni kielelezo kwamba hatufahamu vipengele vya mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambapo sisi ni wanachama wa Jumuiya hiyo.

Mheshimiwa Spika, sehemu ya hukumu hiyo inasomeka kama ifuatavyo, nanukuu
For all the above reasons, the final orders in this Reference are that:
(a)       Prayer (ii) is dismissed
(b)       Prayer (i) is granted in the following terms only:
  “A declaration is here by issued that to the extent that the election for Members of Parliament of East African Legislative Assembly conducted by the National Assembly of Tanzania on 17 April, 2012 was premised on only Political Parties as the sole grouping as opposed to all other groups envisaged in Article 50(1) of the Treaty, then the National Assembly of Tanzania violated the said Article”.
(c)        Prayer (iii) is granted in the following terms only:
“A declaration that, by allowing a political party without representation in the National Assembly (TADEA) to field a candidate in the election of 17 April, 2012 for representative to EALA, then the National Assembly of Tanzania was in violation of Article 50(1) of the treaty”.
It is so ordered.

Mheshimiwa Spika, Kwa kuwa Serikali hii ya awamu ya nne inamaliza muda wake, Serikali mpya ya UKAWA itafanya mapitio ya Kanuni za Bunge ili kuhakikisha kwamba zinaendana na mikataba na itifaki mbalimbali za Afrika Mashariki tulizoridhia ili kujenga mazingira ya uwazi na haki Bunge linapotekeleza majukumu yake kuhusiana na mikataba au itifaki hizo.

4.   KASI NDOGO YA TANZANIA KUCHANGAMKIA FURSA KIUCHUMI KATIKA  JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ina fursa za wazi kabisa za kufaidika na Jumuiya ya Afrika ya Mashariki. Cha kusikitisha ni kwamba, serikali hii ya CCM badala ya kuwa na mpango kabambe wa kufaidi fursa hizi imekuwa ni kikwazo kikubwa katika kukua na kusonga mbele katika Jumuiya hii. Kuna lawama za kila aina kuwa serikali ya Tanzania ni kikwazo katika utekelezaji wa Mkataba wa Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, Ikumbukwe kuwa nchi yetu inapakana na nchi nane katika mipaka yake. Kushindwa kutumia fursa za kiuchumi ambazo tunazo ni kikwazo kikubwa cha maendeleo ya wananchi wetu. Kwa sasa tunanunua kwa wingi kuliko tunavyouza. Ni katika hali hii thamani ya  shilingi yetu inazidi kuporomoka. Tungetumia fursa za kiuchumi kwa nchi nane tu tulizopakana nazo, hakika Tanzania ingesonga mbele kiuchumi.

Mheshimiwa Spika, Serikali hii imeshindwa kufukuzia fursa za kiuchumi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki kiasi kwamba hata wale wananchi waliopo mipakani kama wananchi wangu wa Rombo hawaelewi hii Jumuiya inawasaidiaje kujikwamua kiuchumi.

5.   MFUMO WETU WA ELIMU NA FURSA ZA AJIRA NDANI YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI        

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba zetu za Kambi Rasmi ya Upinzani katika Wizara ya Elimu tumekuwa tukitoa mapungufu makubwa katika mfumo wetu wa elimu ambao umepelekea kuathiri hata fursa za ajira za wahitimu wetu nchini.

Mheshimiwa Spika, Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi na wanasiasa kuwa utekelezaji wa soko la pamoja la Afrika Mashariki utaathiri fursa za ajira za watanzania hapa nchini, kwa hofu kuwa ajira nyingi zitaenda kwa jirani zetu wa Kenya au Uganda.

Mheshimiwa Spika, Hofu hii ya wananchi na wanasiasa ni dhahiri inatokana na mfumo mbovu wa elimu ambao umechangiwa na serikali hii ya CCM. Kutokana na hali hiyo;  viongozi na baadhi ya wananchi wenye uwezo wanawapeleka  watoto wao nchi za nje hasa nchi jirani ya Kenya kwa ajili ya kupata elimu bora.  Ni rai ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Serikali kuupitia upya mfumo wa Elimu yetu ili ushabihiane na nchi washirika ili kuwe na ushindani wenye mizania sawa ya kigezo cha elimu katika kuwania fursa za ajira katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inawaahidi wananchi kuwa itaufumua upya mfumo wa elimu yetu ili kuendana na hali halisi ya soko la ajira katika Afrika Mashariki baada ya kuipumzisha CCM katika Uchaguzi wa Oktoba Mwaka huu 2015.
6.   MAFUNZO KWA MAJAJI WA MAHAKAMA YA AFRIKA MASHARIKI

Mheshimiwa Spika, Katika hotuba yetu kwa mwaka wa fedha 2014/2015 tulieleza  kwa kina namna mchakato  mzima  wa uteuzi wa Majaji wa Afrika Mashariki unavyofanyika na namna ambavyo Majaji wanavyochukua muda mrefu katika mafunzo kuliko kuhudumia  mahakama na aukufanya kazi zao.

Mheshimiwa Spika, Jambo hili linatokana na Majaji kutoka katika mifumo tofauti ya kisheria katika nchi zetu. Tuliitaka Serikali hii ya CCM kupeleka hoja ya kuongeza muda wa Majaji ili kuwapa muda wa mafunzo lakini pia kuwapatia muda wa kuhudumia katika Mahakama hiyo, lakini mpaka sasa hakuna liliofanyika.

Mheshimiwa Spika, Serikali itakayoundwa na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni itahakikisha kuwa inapeleka hoja ndani ya Jumuiya kuboresha utaratibu wa uteuzi wa Majaji na mfumo mzima wa Mahakama hiyo kwa manufaa ya nchi washirika na wananchi wetu.7.   FAIDA NA HASARA ZA UANACHAMA PACHA KATIKA MASHIRIKIANO YA KIKANDA

Mheshimiwa Spika, katika hotuba yangu kuhusu bajeti ya Wizara hii kwa mwaka wa fedha 2014/15, niliitaka Serikali kuainisha uwiano wa fursa na faida za kiuchumi Tanzania inazopata katika Jumuiya ya Afrika Mashariki na SADC ili hatimaye tuweze kuchagua ushirika mmoja wenye tija kwetu zaidi kuliko kuwa katika sehemu zote mbili bila ufanisi.

Mheshimiwa Spika, ni katika muktadha huo niliwakumbusha Waheshimiwa Wabunge methali moja isemayo “Mshika Mawili Moja Humponyoka” nikimaanisha hatuwezi kuwa “effective” katika mashirikiano yote mawili kwa asilimia mia moja. Lazima katika ushirika mmoja tutalegalega. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kulieleza Bunge hili ni nini mantiki ya kung’ng’ania kuwa katika mashirikiano yote mawili. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua kama msingi wa mashirikiano hayo umezingatia ukuzaji wa diplomasia ya uchumi au Serikali imeendelea kung’ang’ania diplomasia ya kisiasa ili kusaidiwa kuendelea kubaki madarakani na nchi washirika  kwa kuruhusu “free movements” ambapo imebainika kwamba raia wa kigeni wanaingia nchini bila viza na  wanaandikishwa kama wapiga kura hapa nchini. Tunaitaka Serikali kutoa kauli kuhusu jambo hili.
Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni iliishauri Serikali kufanya utafiti ili kuona ni katika umoja upi ambapo Taifa litanufaika zaidi kiuchumi ili kubaki katika umoja huo na kujiondoa kwenye umoja uliobaki. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilirejea Ripoti ya Uchumi ya Benki ya Dunia ya mwaka 2012 kuhusu mwenendo wa kibiashara katika Nchi za Afrika Mashariki. Katika Ripoti hiyo ilibainika kwamba mwenendo wa kibiashara  wa Tanzania (kwa maana ya kuuza na kununua bidhaa);  katika nchi kumi ambazo tunanunua bidhaa duniani, Kenya ni nchi ya 8;  na katika nchi kumi za ambazo tunauza bidhaa katika bara la Afrika, Kenya ni nchi ya pili.

Ilibainika pia kwamba maingiliano ya kibiashara ya wananchi wa Tanzania katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni makubwa zaidi kuliko maingiliano na nchi za SADC. Hili linatokana na takwimu ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo zinaonesha kuwa Tanzania inafanya biashara zaidi na nchi za Kenya na Uganda.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, ni dhahiri upande wenye faida zaidi kiuchumi unajulikana nao ni Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kueleza faida za kiuchumi katika SADC ikiwa watanzania wanawindwa kama swala huko Afrika ya Kusini kutokana na ubaguzi katika ajira?
8.   WAHAMIAJI HARAMU KUTOKA KWA NCHI WASHIRIKA

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua Serikali itaweza vipi kudhibiti uhamiaji haramu hapa nchini ikiwa imefungua mipaka na kuondoa masharti ya viza kwa baadhi ya nchi inazopakana nazo. Aidha, Kambi Rasmi ya Upinzani inataka kujua ni kwa nini  masharti ya viza yaondolewe kwa Msumbiji na sio katika nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki? Kuna ajenda gani ya siri na Msumbiji?

9.   MAFURIKO YA WAKIMBIZI KUTOKA BURUNDI

Mheshimiwa Spika, machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi yamesababisha mafuriko ya wakimbizi wa Burundi nchini kwetu. Kwa mujibu wa shirika la Kimataifa la Oxfam, zaidi ya wakimbizi 70,000 wameshaingia Tanzania kutokana na machafuko yanayoendelea nchini Burundi.

Mheshimiwa Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka Serikali kueleza ina mikakati gani ya kukabiliana na  athari za wimbi la wakimbizi wanaoingia nchini kama vile mahitaji ya chakula, maji safi, huduma za afya ukizingatia kuna magonjwa ya mlipuko ya kuhara  na kipindupindu ambayo yamewapata wakimbizi na wananchi wetu pia.

10.               MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA BAJETI YA WIZARA  KWA MWAKA  2014/15 NA UCHAMBUZI WA BAJETI YA 2015/16

Mheshimiwa Spika,  wizara hii ilitengewa shilingi bilioni 23.06 katika mwaka wa fedha 2014/15  lakini hadi kufikia Machi, 2015 fedha iliyotolewa na hazina ilikuwa ni shilingi bilioni 14.35 sawa na asilimia 62.2 tu ya bajeti iliyoidhininshwa. Kambi Rasmi ya Upinzani inataka Serikali kulithibitishia bunge hili kama itaweza kutekeleza asilimia 37.8 iliyobaki kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika.

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa randama ya wizara fungu 97 (uk.13) katika shilingi bilioni 14.35 iliyotolewa na hazina kufikia machi, 2015, ni shilingi bilioni 3.09 tu iliyotumika kutekeleza majukumu ya wizara huku kiasi cha shilingi bilioni 9.85 kikitumika kama mchango wa Tanzania katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Spika, kwa mwaka mpya wa fedha 2015/16 Wizara hii inaomba kuidhinishiwa kiasi cha shilingi bilioni 24.59.
Fedha za matumizi mengineyo ni shilingi bilioni 21.9, Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 14.45 sawa na asilimia 66  ni kwa ajili ya michango wa Tanzania katika  Jumuiya ya Afrika Mashariki na shilingi bilioni 7.52 sawa na asilimia 34 ya matumizi mengineyo ni kwa ajili ya kutekeleza majukumu ya wizara kwa mwaka wa fedha 2015/16.
Mheshimiwa Spika, kiuhalisia bajeti ya wizara hii ni ndogo sana, na  kwa uzoefu fedha hazitolewi kwa wakati. Pengine hii ni sababu mojawapo ya Tanzania kulaumiwa na nchi wanachama wa Jumuiya kwamba iko nyuma katika kutekeleza baadhi ya programu na miradi ya maendeleo ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

11.               HITIMISHO

Mheshimiwa Spika, napenda kumalizia hotuba yangu kwa kuwatakia maisha mema uraiani baada ya Bunge kuvunjwa, napenda pia kuwatakia kila la heri na ushindi wa kishido wabunge na watia nia wote wa UKAWA katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu wa 2015.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kuwapa wosia wana CCM kuanza kujiandaa kisaikolojia kupokea mabadiliko kwani ifikapo Oktoba, Taifa litaandika historia mpya kwa UKAWA kuingia madarakani.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba kuwasilisha.
Joseph Roman Selasini (Mb)
MSEMAJI MKUU WA KABI RASMI YA UPINZANI NA
WAZIRI KIVULI WA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI
29 Mei, 2015
Next Post Previous Post
Bukobawadau