Bukobawadau

KIGOMA WAPONGEZWA KWA UBUNIFU WA KUSAFIRISHA WAOMBA HIFADHI YA UKIMBIZI KUTOKA BURUNDI WANAOINGIA NCHINI

Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya (mwenye koti) akipata maelezo ya njia ya kutembea kwa miguu kutoka Kagunga hadi Mkigo kutoka kwa  mkazi wa kijiji hicho, Mahmud Ahmad wakati alipokagua njia hiyo ili itumike kuwasafirisha waomba hifadhi ya ukimbizi wa Burundi, tarehe 17 Mei, 2015, (mwenye Kaunda suti ) ni Mkurugenzi Idara ya uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jen, Mbazi Msuya
 Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya (mwenye koti) akiwa katika kijiji cha Kilemba kwa ajili ya  kuwapokea waomba hifadhi ya ukimbizi wa Burundi waliokuwa wanasafirishwa kwa kutembea kwa miguu kutoka kijiji cha kagunga hadi  kijijini hapo ili wapelekwe kambini (mwenye Kaunda suti ) ni Mkurugenzi Idara ya uratibu maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jen, Mbazi Msuya, Mkuu wa Kikosi  cha Jeshi la Wananchi 24 KJ  Kigoma, Luteni Kanali Donald Msengi (katikati) na Kaimu Katibu tawala wa mkoa wa Kigoma, Salvatory Shauri tarehe 17 Mei, 2015.
 Mkuu wa mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya akiongea na  vijana ambao ni waomba hifadhi ya ukimbizi kutoka Burundi mara baada ya kuwapokea vijana hao walipofika kijijini Kilemba ili wapelekwe kambini baada ya kusafirishwa kwa kutembea kwa  miguu kutoka kijiji cha kagunga  tarehe 17 Mei, 2015.
Baadhi ya vijana takribani 36 ambao ni waomba hifadhi ya ukimbizi kutoka Burundi wakiwa wamepunzika kijiini Kilemba kabla ya kusafirishwa na basi kwenda kwenye kambini mara baada ya  kusafirishwa kwa kutembea kwa  miguu kutoka kijiji cha kagunga  tarehe 17 Mei, 2015.
 Mkurugenzi Idara ya uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen, Mbazi Msuya akiongea na mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la kusafirisha wakimbizi, Son Ha Dinh,  mara baada ya kuwasafirisha vijana takribani 36 ambao ni waomba hifadhi ya ukimbizi kutoka Burundi kutoka kijiji cha kagunga,  tarehe 17 Mei, 2015.

Na. Mwandishi Maalum.
Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu imeupongeza mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa yanayowahudumia wakimbizi kwa ubunifu wanaoufanya wa kusafirisha waomba hifadhi ya ukimbizi kutoka Burundi. Kutokana na zoezi linaloendelea mjini Kigoma la upokeaji waomba hifadhi hao, tayari waomba hifadhi wapatao elfu 90 wameandikishwa kuingia nchini kupitia kijiji jirani na Burundi cha Kagunga. Hadi tarehe 15, Mei tayari waomba hifadhi wapatao elfu 21 walikuwa wamesafirishwa kwa meli hadi Kigoma mjini na baadae kusafirishwa  kwa basi hadi katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.
Kutoka kijijini  Kagunga  hadi Kigoma mjini usafiri unaoaminika ni usafiri wa majini. Meli ya Mv. Liemba ambayo hutumika kubeba abiria inaouwezo wa kubeba abiria wapatao 600. Mkoa wa Kigoma kwa kushirikiana na mashirika ya Kimataifa wameweza kutumia meli ya kukodi ya Mv. Malagarasi kwa ajili ya kubeba abiria yenye uwezo wa kubeba abiria wapatao 300. Aidha, kwa kuzingatia idadi kuwa kubwa ya waomba hifadhi dhidi ya  vyombo vya usafri salama vya majini vinavyotumika, tayari njia nyingine imebuniwa ya kutumia njia ya kutembea umbali wa km 10 kwa vijana wenye nguvu , kutoka kagunga hadi Kilemba ambapo husafirishwa na mabasi  hadi katika kambi ya Nyarugusu wilayani Kasulu.
Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Brigedia Jenerali  Mbazi Msuya akiongea hivi karibuni mara baada ya kuwatembelea waomba hifadhi hao waliopo kijijini Kagunga na kushiriki zoezi la kuwapokea waomba hifadhi  hao mjini Kigoma wapatao 600  waliowasili kwa meli ya Mv. Liemba na kuwapokea wengine kijijini Kilemba wapatao vijana 36 waliosafirishwa kwa kutembea kwa miguu kutoka Kagunga, alisema kuwa kutokana na idadi ya watu waliopo kijijini hapo na vyombo salama vya usafiri wa majini vilivyomo mkoani humo ubunifu wa namna ya kuwasafirisha waomba hifadhi hao hadi kambini ni vyema ukapongezwa.
“Takwimu za uhamiaji za Kagunga zinaonesha kuwa hadi hivi sasa wapatao watu elfu 90 wamejiandikisha kuingia nchini kupitia mpaka uliopo hapa  kagunga na kati ya watu hao watoto ni wapatao elfu 75 , ile hali kwa mujibu wa mtendaji wa kijiji hiki kuna wakazi wapatao elfu 17, kwa mantiki hii idadi hii ya watu ni kubwa ukilinganisha na uwezo wa kijiji hivyo ubunifu wa kutumia njia ya kusafirisha vijana wenye nguvu kutembea mwendo wa km 10, hadi Kilemba utapunguza idadi ya watu waliopo hapa na hatimaye tutakuwa nauwezekano mkubwa wa kuepuka magonjwa ya mlipuko kijijini hapo” alisema Msuya
Aliongeza kuwa palipo na watu wengi  yakilipuka magonjwa ya mlipuko ni maafa makubwa. Hivyo idara ya uratibu wa maafa nchini inaupongeza uongozi wa  mkoa wa Kigoma unavyofanya zoezi hilo kwa kushirikiana na serikali ya kijiji cha kagunga , halmashauri za wilaya  pamoja na mashirika ya kimataifa yanayowahudumia wakimbizi na Taasisi za kitaifa zinazowahudumia wakimbizi kwa kuwapokea waomba hifadhi hawa kwa kuhakikisha wanakuwa salama.
Vilevile alifafanua kuwa lengo ni kuepusha maafa kwa waomba hifadhi na jamii ya kitanzania hivyo tayari wameshajadiliana na uongozi wa mkoa juu ya njia nyingine mbadala za kuharakisha usafiriishaji wa waomba hifadhi hao ambapo kwa kuwa njia hizo zinashirikisha wadau tofauti wenye mamlaka mbalimbali  baada ya kuwafikishia mawazo hayo njia hizo zitaanza kutekelezwa mara moja ili kuepusha maafa yanayo weza kutokana na idadi kubwa ya watu waliopo Kagunga.
Awali, akiongea mara baada ya kuwapokea vijana wapatao 36 ambao ni waomba hifadhi ya ukimbizi  waliotembea kwa miguu umbali wa km 10 kutoka  kijijini Kagunga hadi kijijini Kilemba Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu, Issa Machibya  aliwataka waomba hifadhi ya ukimbizi kutoka Burundi hao kutii na kufuata sheria na kanuni wanazo elezwa na uongozi husika pindi wanapokuwa katika kambi watakazo hifadhiwa hapa nchini.
Mwisho.
Next Post Previous Post
Bukobawadau