Bukobawadau

MABERE MARANDO AWAONYA NEC 'KUTOCHEZEA' BVR DAR ES SALAAM, PWANI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAMKO KUHUSU KUAHIRISHWA KWA MUDA WA UBORESHAJI WA DAFTARI LA
KUDUMU LA WAPIGA KURA KWA KUTUMIA TEKNOLOJIA YA “BIOMETRIC VOTERS
REGISTRATION” (BVR) KATIKA
JIJI LA DAR ES SALAAM NA MKOA WA PWANI
Kufuatia Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuutangazia umma kuwa zoezi la uboreshaji wa
Daftari la kudumu la wapiga kura liliokuwa lianze tarehe 04/07/2015 kwa Jiji la Dar
es Salaam na tarehe 25/06/2015 kwa mkoa wa Pwani kwamba limeahirishwa hadi
tarehe itakayotangazwa tena; Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
Kanda Pwani (Mikoa ya Temeke, Kinondoni, Ilala na Pwani) kinaitaka Tume ifanye
yafuatayo:
1. Tume ya Uchaguzi itangaze tarehe ya kuanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la
kudumu la wapiga kura katika Jiji la Dar es Salaam na mkoa wa Pwani baada ya
kuahirishwa ili kuwasaidia wananchi kujipanga kwa zoezi zima la uandikishaji.
2. Tume ya Taifa ya Uchaguzi izingatie mfumo wa kiuchumi na kimazingira uliopo
katika mikoa hii unaowafanya watu wengi muda wa mchana kuwepo
makazini/katika shughuli za kiuchumi. Na kupanga muda wakutosha kwa
kuzingatia idadi ya wakazi. Hii ni pamoja na kuzingatia kuwa Jiji la Dar es
Salaam na mkoa wa Pwani pekee, kwa takwimu za serikali, vina wapiga kura
wapatao asilimia 15 ya wapiga kura wote nchini.
3. Tume ya Taifa ya Uchaguzi ihakikishe changamoto zote zilizotokea sehemu
mbalimbali zinapatiwe ufumbuzi kabla ya zoezi halijaanza Dar es Salaam na
Pwani. Changamoto hizi ni pamoja na; mashine kuwa mbovu, idadi ya mashine
kutokukidhi mahitaji, idadi ya vituo kwenye kata kutoendana na idadi ya
wanaotakiwa kujiandikisha, utaratibu wa kuchukua majina bila kuzingatia
waliopanga mistari, na waandikishaji kutokuwa na uwezo thabiti wa kutumia
mashine za uandikishaji. Uzoefu umeonyesha kuwa, changamoto hizi
zimeendelea kujirudiarudia katika sehemu nyingi bila kutolewa ufumbuzi wa
uhakika na Tume ya Uchaguzi.
4. Tunaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuweka wazi mbele ya umma kuwa Jeshi
la Polisi halihusiki katika kupanga utaratibu wa BVR hali inayosababisha
vurugu na ukosefu wa amani vituoni. Uzoefu uliopatikana wakati wa ziara za
viongozi wakuu wa chama kukagua zoezi la BVR katika maeneo mbalimbali
unaonesha kuwa maeneo yote ambayo polisi hawakuwepo vituoni wakati wa
uandikishaji, utaratibu ulikwenda kwa utulivu lakini hali imekuwa tofauti
kabisa kote ambako jeshi hilo limehusika kusimamia uandikishaji. Mf; Arusha
Tunapeda kusisitiza kuwa; CHADEMA haitofumbia macho mikakati yoyote
itakayoonekana ina dhamira ya kudhoofisha zoezi la uandikishaji ambayo
itasababisha kuwanyima wananchi haki ya kikatiba ya kupiga kura, maana bila
kujiandikisha mtu hawezi kupiga kura.
Mwisho, CHADEMA inapenda kuwahamasishwa wananchi kujitokeza kwa wingi
wakati wa zoezi la uandikishaji litakapoanza katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa
Pwani.
Asanteni!
IMETOLEWA NA
Mhe. MABAERE N. MARANDO
MWENYEKITI WA CHADEMA KANDA YA PWANI
Next Post Previous Post
Bukobawadau