Bukobawadau

RITA YAZUNGUMZIA UMUHIMU WA KUWA NA CHETI CHA KUZALIWA

 Ofisa Uhusiano wa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Jafarri Malema (kushoto), akizungumza na wafanyakazi wa gazeti la Jambo Leo (hawapo pichani), Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu shughuli zinazofanywa na Rita na umuhimu wa cheti cha kuzaliwa. Kulia ni Ofisa Uhusiano wa Rita, Grace Kyasi.
 Ofisa Uhusiano wa Rita, Grace Kyasi akizungumza katika mkutano na wafanyakazi wa gazeti la Jambo Leo.
Wafanyakazi wa gazeti la Jambo Leo wakiwasikiliza maofisa wa Rita walipokuwa wakizungumza nao.

Dotto Mwaibale

WANANCHI wametakiwa kuwa na vyeti vya kuzaliwa kwani vina umuhimu katika maisha ya kila siku ndani na nje ya nchi.

Mwito huo umetolewa na Ofisa Uhusiano wa Wakala wa  Usajili Ufilisi na Udhamini (RITA), Jafarri Malema wakati  akizungumza na wafanyakazi wa gazeti la Jambo Leo Dar es Salaam leo asubuhi, kuhusu shughuli zinazofanywa na Rita na umuhimu wa kuwa na cheti cha kuzaliwa. 

"Cheti za kuzaliwa ni msingi wa mafanikio ya kila mmoja wetu na ni muhimu kuwa nacho" alisema Malema.

Alisema Rita imekuwa ikifanya shughuli za usajili wa vizazi,vyeti vya kuzaliwa, kuandika wosia, kusajili ndoa na talaka na udhamini kama mali za umma na ile isiyokuwa na mwenyewe.

Alisema faida ya kuandika wosia unasaidia kuepusha watoto, mke au mume kunyang'anywa mali pale kinapotokea kifo na inawezesha kumchagua msimamizi wa mirathi.

Alitaja faida nyingine ya kuandika wosia kuwa ni kuepusha migongano katika familia, ndugu au jamaa na kuwa unampa uhakika wa maisha bora ya baadae warithi wa mali waliziachiwa.

Alisema jambo linalofanyika baada ya kufariki kwa mtu aliyeandika wosia mmoja wa mashahidi anatakiwa kwenda kutoa taarifa Rita ambapo taratibu za wosia kuwasilishwa mahali husika hufanyika.

Naye Ofisa Uhusiano wa Rita, Grace Kyasi alisema umuhimu wa kuwa na cheti cha kuzaliwa ni mkubwa kwani ni nyaraka pekee yenye mamlaka kisheria kuthibitisha tarehe na mahali mtu alipozaliwa na ni nyaraka muhimu kwa kila mwananchi kwani hutumika kupata huduma nyingine za msingi kama elimu, afya na makazi.

Alisema cheti cha kuzaliwa kinawawezesha watoto kujiunga na elimu ya msingi na sekondari na kuwawezesha kupata nafasi ya masomo ya elimu ya juu pamoja na mikopo ya masomo.
(Imeandaliwa na mtandao wa www.habari za jamii.com-simu namba 0712-727062)


Next Post Previous Post
Bukobawadau