Bukobawadau

WASANII KUTUMIKA KUELIMISHA UMMA MENEJIMENTI YA MAAFA

Askari wa Jeshi la Zima moto nchini, Josephat John akieleleza matumizi ya Kizimamoto wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, mjini Dodoma tarehe, 21 Juni, 2015.
Afisa Tawala, Ofisi ya Waziri Mkuu, Leah Kibassa, akifanya mazoezi ya kutumia kizima moto wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa watumishi wa Ofisi hiyo, mjini Dodoma tarehe, 21 Juni, 2015.
 Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu  Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brig. Jen. Mbazi Msuya (mwenye tai) akishuhudia, Salma Juma akikabidhiwa Kizima moto kilichonunuliwa na washiriki wa mafunzo ya menejimenti ya maafa wa Ofisi hiyo mjini Dodoma tarehe, 21 Juni, 2015,  Kwa lengo la kuhamasisha watumishi wa Ofisi hiyo kukabili majanga ya moto,
Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu wakifuatilia mafunzo ya majanga ya moto  wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa mjini Dodoma tarehe, 21 Juni, 2015.
 
Wasanii kutumika kuelimisha umma menejimenti ya maafa
Na. Mwandishi Maalum
Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa inaandaa mkakati wa elimu kwa umma wa menejimenti ya maafa ambao utawatumia watu maarufu nchini wakiwemo wasanii wa sanaa mbali mbali  kwa lengo la kufikisha elimu kwa umma ya menejimenti ya maafa.
Akiongea wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Mjini Dodoma mwishoni mwa wiki hii, Brig.Jen, Mbazi Msuya alibainisha kuwa jamii ikielimishwa  kikamilifu  juu ya menejimenti ya maafa athari za maafa zinapunguzika.
“Tunaposema menejimenti ya maafa tunazingatia, kuzuia, kukabili  maafa na kurejesha hali ya awali baada ya maafa kutokea. Kwa mantiki hii kama  tunavyo elewa Wasanii wanao uwezo wa kufikisha ujumbe kwa haraka, lugha nyepesi,  kwa watu  wengi na  kwa ujumbe mmoja, hili ndo linalotusukuma kufikiria kutumia hawa watu katika kutoa elimu ya menejimenti ya maafa kwa jamii yetu” alisema Msuya.
Msuya aliongeza kuwa nchi yetu imekuwa ikikumbwa na majanga ya asili  na yale yanayosababishwa na binadamu, ambapo majanga yanayosababishwa na binadamu kwa kiwango kikubwa jamii inaweza  kuyakabili  tu ikiwa elimu ya menejimenti ya  maafa hayo imemfikia kila mwanachi. Hivyo kwa kuwa wasanii wengi msingi wa kazi zao za sanaa huaksi yanayojiri katika jamii yao hivyo hii itakuwa ni fursa kwao kuijengea jamii uwezo wa kuyakabili maafa.
“Athari za Majanga yanayosababishwa na binadamu kama moto yanaweza kuzuilika ikiwa menejimenti ya majanga hayo itatolewa kwa umma. Wananchi wakielimishwa umuhimu wa kuwa na vizima moto majumbani mwao na katika vyombo vya moto wanaweza kukabili majanga ya moto na hili litawezekana kwani tayari tunayo mikakati ya mawasiliano ya kukabiliana na maafa ” alisisitiza Msuya.
Ofisi ya waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu maafa tayari imeshaandaa  Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa  mkoa wa Mtwara, Shinyanga na Dodoma lengo ikiwa ni kila mkoa nchini kuwa na mkakati huo utakowezesha menejimenti ya maafa kwa jamii ya watanzania. Aidha mkakati huo unabainisha kila mdau wa maafa wajibu wake katika menejimenti ya maafa wakiwemo wasanii.
Next Post Previous Post
Bukobawadau