UPINZANI WAKIMSIMAMISHA MWENYE SIFA HIZI NA SISI CCM TUKAFANYA MAKOSA KWA KUMPITISHA "FISADI" TUMELIWA
Ni
jana tu nimemaliza uchambuzi wa watu wanaotajwa au waliojitokeza
kugombea urais au wale ambao hawajajitangaza na hawana nia lakini jamii
ndani na nje ya vyama vyao inawataja kama watu wenye sifa, uwezo na hata
vigezo vya kuiongoza nchi yetu, kutoka vyama vya upinzani.
Lengo
la uchambuzi huu ni kuwafanya Watanzania waanze kuwafahamu viongozi wao
wajao na hata aina ya sifa wanazoweza kuwa nazo. Inawezekana kabisa
kuwa wagombea waliochambuliwa asitokee mmoja wao kugombea au la, lakini
hapa ninachoangalia ni kwamba tayari wananchi watakuwa “wamesogezwa
karibu na ajenda ya uchaguzi” na hata akiletwa mgombea kutoka wapi,
walau wananchi watakuwa wanajua wafanye uamuzi wa namna gani.
Leo
nahitimisha hoja ya wagombea wa upinzani kwa kutoa sifa 10 za mgombea
urais bora kutoka upinzani ambaye anaweza kupigiwa kura nyingi na
Watanzania na hatimaye kuwa rais mpya wa Tanzania:
1. Mwenye umaarufu/umashuhuri na anayekubalika
Sifa
hii ni muhimu, unapokuwa nje ya dola na nje ya chama tawala siyo rahisi
kukishinda chama kinachoongoza Serikali. Umaarufu, umashuhuri na
kukubalika ni mambo ya lazima. Ukitizama historia ya dunia na hata
Afrika, vyama vikongwe vilipoondolewa madarakani waliofanya hivyo
walikuwa wapinzani mashuhuri. Umuhimu wa sifa hii ni kuwa walau mtu
maarufu na mashuhuri au anayekubalika, tayari amewekeza “mbegu” kwenye
mioyo ya wananchi, wanaweza kumwamini ili waondoe hatima ya nchi
mikononi mwa chama kilichowaongoza kwa miaka 50 na kuiweka mikononi mwa
watu wapya. Wananchi wasipomwamini kiongozi wa upinzani anayekuja kwa
sababu wanamkubali, ndipo huzuka ile kasumba ya “tupige kura kwenye
zimwi likujualo”.
Hatari ya sifa hii
Umaarufu,
umashuhuri na kukubalika vitaweza kufanya kazi kwa upinzani ikiwa
mgombea husika hatatumia mwanya wa kukubalika kwake kujenga kiburi na
hatimaye kuwasaliti wananchi. Ndiyo kusema kuwa vyama vya upinzani
vitapaswa kuchagua mtu bora ambaye atatimiza matakwa ya wananchi “hata
kama ni maarufu kuliko jua”.
2. Atakayebeba ajenda bora na kuifafanua vizuri
Kubeba
ajenda bora na kuwa na uwezo wa kuifafanua kwa lugha rahisi ni jambo la
muhimu kwa mtarajiwa kutoka upinzani. Moja kati ya makosa makubwa ya
vyama vya upinzani katika bara la Afrika ni kutaka kubeba ajenda nyingi
na kumrundikia mgombea urais, nakubali kuwa Afrika ina matatizo katika
kila sekta ya maisha ya mwanadamu, lakini lazima iwe na vipaumbele
vinavyowaumiza wananchi. Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa
kuwa na ajenda bora kuliko ile ya CCM na atapaswa kuwa na uwezo wa
kuifafanua akaeleweka na mipango ya utekelezaji wake ikawa siyo ya
“kusadikika”.
Hatari ya sifa hii
Ni
pale inapotokea kuwa mgombea bora wa urais kutoka upinzani anazunguka
nchi na ajenda iliyo bora kabisa lakini utekelezaji wake ukifanana au
kushabihiana moja kwa moja na ule wa mgombea wa CCM. Wananchi wakiona
upinzani unahubiri mipango na mbinu zilezile za CCM wataamua pia
kuchagua “shetani wanayemjua” ili kujiweka kwenye mazingira ya usalama
zaidi. Hivyo, ajenda ya mgombea bora wa upinzani na utekelezaji wake
vinapaswa kuwa “vya kipekee”
.3. Mwenye uzoefu na rekodi ya uchapakazi
Uzoefu
wa uongozi na uchapakazi unaofahamika ni jambo la msingi kwa mgombea
bora wa urais kutoka upinzani. Vyama vya upinzani haviwezi kushinda
uchaguzi na mgombea bora vitakayekuwa naye ikiwa mtu huyo si mzoefu na
mchapakazi anayefahamika, mtu mwenye kujali wengine katika kazi lakini
ambaye wananchi wataamini kuwa huyu atasimama pamoja na sisi usiku na
mchana kuleta mabadiliko ya nchi.
Katika
siasa, wananchi hupaswa kwanza kuamini na kisha hufanya uamuzi. Ikiwa
mgombea bora wa urais wa upinzani hatakuwa na rekodi za uzoefu wa
utumishi (katika taasisi za dini, serikali, vyama vya siasa na
nyinginezo) si rahisi kumuuza kwa wananchi. Pia, ni lazima awe ni mtu
ambaye rekodi zake zinatajwa kuwahi kuleta mabadiliko makubwa mahali
alipofanya kazi.
Hatari ya sifa hii
Sifa
hii hupaswa kuelezewa na kufahamika kwa wananchi kutoka kwa timu za
kampeni za wagombea, wakati mwingine wapambe wa wagombea huchukua muda
mwingi kutaja elimu ya mgombea wakidhani wananchi wanachagua elimu,
kumbe elimu ni jambo moja tu kati ya sifa 100 za kiongozi. Ikiwa sifa
hii muhimu haielezwi kwa uwazi kwa wananchi na hasa kwa kutaja rekodi
bora za mgombea wa upinzani, wananchi wanaweza kumpa kisogo.
4. Mwenye uadilifu usio na shaka
Mgombea
bora wa upinzani katika uchaguzi, anapaswa kuwa na uadilifu uliotukuka,
usio na madoa wala shaka. Hapa nina maana kuwa, awe ni mtu ambaye
uadilifu wake unatambulika kwa wananchi na kwa Taifa zima. Awe na rekodi
za uadilifu kumshinda mgombea wa CCM, nina maana kuwa, wananchi
wakimpima huyu wa upinzani na yule wa CCM – haraka haraka wasimame na
kusema, “…naam! Huyu wa upinzani ni mwadilifu zaidi”. Marais wengi
walioingia madarakani hasa hapa Afrika na hata Ulaya na Marekani kwa
kuviondoa vyama vilivyokuwa madarakani, walipimwa kwa sifa hii.
Hatari ya sifa hii
Kigezo
hiki hupata shida kubwa katika nchi ambazo uelewa wa wananchi vijijini
na hata mjini si mkubwa. Wagombea waadilifu nao huweza kuchafuliwa ndani
ya siku moja tu. Katika nchi ambayo si ajabu mgombea akawa hata na
uwezo wa “kuhonga” chombo cha habari ili kimchafue mwenzake, sifa za
mgombea bora zinaweza kuingizwa katika tope. Vyama vya upinzani
vitapaswa kuwa na mfumo sahihi wa kuhakikisha uadilifu wa mgombea wake
unazungumzwa kama ulivyo na haubadilishwi na propaganda za CCM.
5. Mwenye uwezo wa kusimamia, kuinua uchumi
Moja
ya matatizo ambayo hayana dawa hapa Tanzania ni usimamizi wa uchumi.
Nchi yetu inayumba kila mara na tunashindwa kutekeleza mipango yetu kwa
sababu ya uchumi dhaifu, unaobadilika kila dakika na ambao hauna dira.
Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa na uwezo wa
kusimamia na kuinua uchumi wa nchi. Awe ni mtu ambaye akisimama na
kuweka ajenda ya uchumi mezani, Watanzania wote wanamwelewa, kwamba
“naam, huyu ana uwezo wa kusimamia uchumi na kuondoa umaskini wa nchi”.
Hatari ya sifa hii
Ni
pale mgombea wa upinzani atazunguka na mipango kabambe ya uchumi lakini
yenye shaka kubwa kwenye utekelezaji au kuondoa umaskini, lakini pia ni
pale mipango hiyo haitakuwa ya muda mfupi. Katika nchi maskini,
wananchi wanahitaji matokeo haraka, vyama vya upinzani vitakuwa na
jukumu la kuwa na mipango ya mfano ya muda mfupi ili kuwahakikishia
wananchi kuwa ile ya muda mrefu pia itaweza kutekelezeka kwa wakati
6. Kuongoza mapambano dhidi ya rushwa
Rushwa
ni adui wa haki na ni tatizo kubwa katika ukuaji wa uchumi wa Afrika.
Mgombea bora wa urais kutoka upinzani atapaswa kuwa mtu wa kipekee
ambaye moja ya sifa zake kuu ni mapambano dhidi ya rushwa, ndogo na
kubwa. Awe ni Mtanzania ambaye si tu kwamba anapiga vita rushwa, bali
anawachukia wala rushwa kama “kifo” na ni mtu ambaye yuko mbali kabisa
na wala “rushwa”. Ndani ya CCM kwenyewe nadhani watatafuta mgombea wa
namna hii ili kulinda hadhi yao, vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu
la kutafuta mpinga rushwa mahiri kuliko yule wa CCM, kwamba ukiwaweka
pamoja hawa wawili – wananchi wenyewe waseme “…naam huyu wa upinzani
anaweza mapambano haya zaidi kuliko huyu wa CCM”
Hatari ya sifa hii
Ikiwa
upinzani utakuwa na mtu mashuhuri katika mapambano ya rushwa lakini
ukawa hauna mipango ya kuhuisha haraka mifumo inayoleta mianya ya rushwa
ndani ya nchi. Ndiyo kusema kuwa moja ya mipango ya upinzani inapaswa
kuwa ni pamoja na kuweka wazi mifumo mipya ya usimamizi wa mapambano
dhidi ya rushwa na hata kueleza watu watakaokuwa na sifa za kufanya kazi
na mifumo hiyo.
7. Asiyependa kulipiza visasi na atakayefuata sheria
Jambo
hili si dogo katika siasa. Rais ajaye kutoka upinzani anapaswa kuwa na
sifa hii. Kwamba afahamike na kujulikana kwa kutokuwa na tabia ya
kulipiza visasi lakini ambaye atazingatia matakwa ya sheria katika
utendaji na awe na rekodi hizo. Unajua, kuna mambo ya kisheria ambayo ni
lazima rais yeyote yule akiingia lazima ayafuate, mfano, wizi wa pesa
za umma, hata kama umefanywa mwaka 1960 na ushahidi upo, lazima
watuhumiwa wachukuliwe hatua leo, “jinai haifi wala kupotea”. Lakini
kuna masuala mengine mengi tu ya kawaida ambayo yalikuwa yanatendwa na
uongozi uliopita kwa sababu “za kipuuzi” na zisizo na maana, hayana haja
ya kuwa kichwani kwa rais anayekuja.
Hatari ya sifa hii
Wananchi
wengi huhofia masuala ya usalama iwapo vyama vipya vitaingia
madarakani, hasa Afrika na moja ya masuala ambayo hupoteza usalama ni
“kulipiza visasi”. Ndiyo maana vyama vya upinzani vinawajibika kuwa na
mgombea ambaye hatalipiza visasi kwa makosa ya nyuma ya kiutendaji, ila
atafanya hivyo kwa yale yaliyokosewa kwa makusudi na kwa kutofuata
sheria.
8. Uwezo wa kubadilisha mfumo wa nchi
Tangu
tumepata uhuru, nchi yetu imekuwa inasifika kwa kuwa na mifumo mibovu
na isiyo na tija katika kila sekta. Hili ni janga kubwa. Rais bora ajaye
kutoka upinzani ana kazi kubwa ya kubadilisha mfumo wa sasa wa nchi
katika kila eneo ili mifumo ifanye kazi kwa mbio na kwa tija kubwa
zaidi. Leo kuna watu walishtakiwa miaka ya 1990 na bado wako gerezani
bila kuhukumiwa, kuna Kiwanda cha Sukari Kilombero na huko bei ya sukari
ni kubwa kuliko Dar es Salaam. Haya ni matatizo makubwa ya kimfumo.
Wananchi watahitaji kuwa na kiongozi ambaye atakuja kubadilisha kabisa
mifumo ya utendaji kazi katika nchi. Kwa bahati nzuri, upinzani unaweza
kuwa na hoja kama hii kwani vyama hivyo havikuwahi kuongoza Serikali na
vimekuwa “waathirika” wa mfumo uliopo.
Hatari ya sifa hii
Ubadilishaji
wa mifumo ukifanywa haraka na kwa pupa, utaingilia na kuvunja hata
mifumo ambayo ilikuwa imeanza kukua na kukomaa kwa upande chanya. Ni
jukumu la mgombea bora wa upinzani na timu zake kutambua mifumo yote ya
utendaji katika sekta za jamii na kubainisha tangu wakati wa kampeni,
ipi itavunjwa na ipi itarekebishwa ili kutoleta hofu yoyote kwa wapiga
kura.
9. Msimamo unaoeleweka juu ya Katiba
Suala
la katiba mpya ni ajenda muhimu katika uchaguzi wa mwaka huu. Mgombea
bora wa upinzani atapaswa, yeye mwenyewe kuwa na busara za kutosha na
msimamo thabiti juu ya masuala ya kikatiba na hasa mchakato wa Katiba
Mpya. Naona kuna Watanzania wengi watapiga kura katika uchaguzi wa mwaka
huu kwa chama au mgombea ambaye atakuwa na misimamo ya wananchi katika
suala la katiba. Hadi sasa hatuelewi kama katiba itapitishwa au la na
hatuelewi kama wananchi wanaikubali au wanaikataa. Nani atatuvusha na
kwa utaratibu gani? Majibu atakuwa nayo mgombea bora wa urais kutoka
upinzani.
Hatari za sifa hii
Msimamo
wowote ule wa mgombea urais wa upinzani katika jambo hili unaweza kuwa
na athari chanya au hasi kulingana na namna wananchi wanavyolitazama
suala la katiba. Kama mgombea huyu atakuwa na msimamo katika kuikataa
Katiba Inayopendekezwa na kwamba ataanzisha mchakato mpya na ikiwa hayo
ndiyo matakwa ya wananchi walio wengi, jambo hili peke yake
litamuongezea kura za kutosha. La ikiwa kinyume chake, litakuwa na
athari ya kiwango hichohicho bila kujali kama athari yenyewe ni chanya
au hasi.
10. Uzoefu wa masuala ya kimataifa
Moja
ya kazi kubwa za mkuu wa nchi ni kuliwakilisha Taifa katika masuala ya
kimataifa. Rais bora kutoka upinzani hakwepi kuwa na rekodi imara ya
masuala ya kimataifa, si kuishi Ulaya na Marekani, lakini kuwe na
ushahidi wa kutosha kuwa amewahi kushiriki katika baadhi ya shughuli
muhimu za kimataifa na kwamba huenda hata kimataifa yeye ni mtu bora.
Nadhani CCM inaweza kuwa na mgombea mwenye sifa hii pia, ni jukumu la
upinzani pia kuwa na mtu ambaye amejipanga vyema kimataifa na mambo
aliyoyasimamia kimataifa pia yanajulikana, si lazima yawe ya kiserikali,
yanaweza kuwa ya kijamii, ya kitaasisi au ya kitaaluma.
Hatari ya sifa hii
Sifa
hii inaweza kufanywa moja ya propaganda za kuisaidia CCM, kwamba ndicho
chama pekee chenye watu waliofanya kazi za kimataifa na wataifanya
Tanzania ikubalike kimataifa. Vyama vya upinzani vitakuwa na jukumu la
kupambana na propaganda hii kwa kuwa na mgombea ambaye tayari wananchi
wanatambua kuwa ana uzoefu wa kimataifa usio na shaka ili kusiwe na tabu
ya kuanza kumwelezea muda mrefu kwa wapigakura juu ya eneo hili.
HITIMISHO
Andiko
hili peke yake haliwezi kujadili sifa zote muhimu za kiongozi bora
kutoka vyama vya upinzani anayeweza kulivusha Taifa. Nimechokoza mjadala
wa masuala muhimu tu. Tukumbuke kuwa, kazi ya kuongoza Serikali si
nyepesi, inataka kujipanga kila idara na kuwathibitishia wapigakura kuwa
mnaweza bila shaka. Tabia ya wapigakura huwa ni kutafuta namna gani
watawaamini watu wanaowapa madaraka. Bahati nzuri vyama vya upinzani
katika Taifa letu vimekwishafanya kazi ya kupigiwa mfano
inayothibitisha, uzalendo, uadilifu, uzoefu uwajibikaji na utendaji kazi
bora.
Julius
Mtatiro ni Mchambuzi wa Masuala ya Kisiasa na Kijamii; ana uzoefu
mkubwa wa uongozi wa kisiasa hapa Tanzania. Ana Cheti cha Juu cha Sarufi
na Lugha, Shahada ya Sanaa (B.A) katika Elimu (Lugha, Siasa na
Utawala), Shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A) na ni
mwanafunzi wa fani ya sheria (LLB) – Anapatikana kupitia +255787536759.
Uchambuzi huu unatokana na utafiti na maoni yake binafsi.