Bukobawadau

MH. WILFRED RWAKATARE AANZA KAZI YA UBUNGE KWA KASI YA MAGUFULI.

Mh. Rwakatare, MB, akiwa na Bw. Anic Kashasha, Mshauri wa Uwekezaji na Miradi na mdau mkubwa wa maendeleo ya Bukoba, jana, Jumatano, tarehe 25 Nov. 2015.
 Mh. Rwakatare, MB akisalimiana na Bw. Adam Mayingu, Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, alipomtembelea ofisini kwake jana Jumatano, tarehe 25 Nov. 2015. PSPF ni mdau wa BK

Na, Anic R. Kashasha, Alhamis, tarehe 26 Novemba, 2015
Ule msemo wa kwamba nyota njema uonekana asubuhi umejidhihirisha kwa jinsi Mh. Wilfred Rwakatare, Mbunge mpya wa jimbo la Bukoba mjini, ambavyo ameanza mara moja kazi zake mara tu alipotoka kuapishwa Bungeni Dodoma, hata kabla ya kwenda jimboni kwake na kuingia ofisini rasmi.  Mbunge huyo ameamua kujitosa kuwasaka wadau wa mendeleo kwa lengo la kuwashukuru na kuwarejeshea matumaini, kwamba sasa kazi ya kuisisimua Bukoba ki-maendeleo inakwenda kufanyika kweli kweli baada ya kukwama kwa muda mrefu.
Mh. Rwakatare, alibainisha kwamba Jimbo la Bukoba Mjini lina umuhimu wa kipekee kwa mkoa mzima wa Kagera kwa maana ya maendeleo, kwamba Bukoba ambayo ndiyo makao makuu ya mkoa wa Kagera, ndiyo kioo na ufunguo wa maendeleo ya mkoa mzima. Kwa hiyo anatoa rai kwa wananchi wote wa mkoa wa Kagera kumpatia ushirikiano ili kwa pamoja kuiendeleza Bukoba. Mh. Rwakatare, alitanabahisha kwamba nje ya mkoa wa Kagera hususan Dar es salaam wapo wana Kagera wengi wenye taaluma katika fani mbali mbali ambazo ni muhimu kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya Bukoba na Kagera kwa ujumla. Kwa hiyo wadau hao ni muhimu sana kwake ili aweze kufanikisha azma yake.
Mh. Rwakatare, alizidi kuongeza kwamba yeye haingii kwenye uongozi kuanzisha gurudumu jipya la jitihada za kuleta madendeleo kwa kumsifia aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba, kipindi kilichopita kupitia CCM,  Mh. Dk. Anatoli Amani, kwamba kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo wakiwemo wana Kagera na taasisi mbali mbali za umma kama Unit Trust of Tanzania (UTT); Tanzania Postal Bank (TPB); Mzinga Corporation; Tanzania Investment Bank (TIB); Public Service Pensions Fund (PSPF) and National Health Insurance Fund (NHIF), waliweza kubuni na kuanzisha miradi mbali mbali ambayo endapo ingelikuwa imetekelezwa yote, leo hii Bukoba na watu wake wangelikuwa na hali tofauti ki-uchumi, kwani miradi hiyo ilikuwa iingize fedha nyingi kwenye uchumi wa Manispaa ya Bukoba. Kwa hiyo mbunge huyo aliona ni vyema kuwatembelea wadau wote walioshiriki katika jitihada hizo na kuwashukuru. 
Ni dhahiri kwamba kila ambaye angelijibidisha kufanya kazi katika eneo lake basi mguso wa uchumi huo (economic impact) ungelimfikia na kuyabadilisha maisha yake. Miradi hiyo ni pamoja na:
  1. Unit Trust of Tanzania (UTT);   iliingia makubaliano na Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba katika mradi wa kupima viwanja ndani ya manispaa ya Bukoba. Jumla ya viwanja 5000 vilipimwa baada ya waliokuwa wamiliki wa ardhi husika kulipwa fidia kadiri ya sheria na taratibu. Viwanja hivyo vyote vilinunuliwa na waombaji mbali mbali wakiwemo waendelezaji binafsi, taasisi za umma na binafsi. Uendelezaji wa viwanja hivyo bado upo katika hatua za awali kutokana na matatizo yaliyojitokeza ya malumbano ya kisiasa baina ya viongozi wa kisiasa. Kwa hakika huu ndio mradi wa kipekee ambao ulilenga kuwaondolea umaskini wana Bukoba kwa njia iliyo endelevu. Ikumbukwe kwamba tangu kupata uhuru hadi mwaka 2010, Manispaa ya Bukoba ilikuwa na viwanja vilivyopimwa na kuwa na hati visivyotimia 5000. Mradi huo ulioanza mwaka 2011, hadi kufikia 2012 ulipima viwanja 5000 kuvipatia hati. Manispaa ya Bukoba na UTT katika mradi huo pia walishirikiana na Benki ya Posta (TPB) ambayo ilitoa huduma za ki-benki kwa utaalam na ufanisi wa hali ya juu. 
2. Mzinga Corporation; hili ni shirika la maendeleo linalomilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania. Ilishirikiana na Manispaa ya Bukoba kwa kutoa huduma za ki-taalam, kwa kuandaa michoro na utaalam mwingine wote wa kuandaa miradi (Engineering design, Quantity Surveying and Service Engineering) hadi kufikia kuweza kutumia matokeo ya utaalamu huo kutafutia mikopo kwa ajilia ya miradi ya stendi kuu ya mabasi kule Kyakairabwa. Mzinga Corporation walikuwa na makubaliano ya kuwa wabiya katika mradi huo. Aidha, Mzinga Corporation, walikuwa wameandaa pia miradi ya kuboresha makazi katika maeneo zilipo nyumba za Manispaa ya Bukoba kwenye maeneo mazuri kama Miembeni na Kashai. Mradi huu wa nyumba za kisasa ulikusudia kuboresha makazi kwa kuongeza idadi ya nyumba (modern apartments) na kubadilisha mandhari ya mji wa Bukoba, tofauti na vijumba vidogo vya zamani vilivyoko katika maeneo hayo.
3. Tanzania Investment Bank (TIB); ambayo ni taasisi ya umma, walikubali kuingia mkataba wa mashirikiano na Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba na kuwakopesha pesa za kuandaa mradi (project design and preparations). Gharama za kuandaa mradi katika hali ya kawaida hubebwa na mwenye mradi, kwa hiyo zilitakiwa kulipwa na Manispaa ya Bukoba ambayo haikuwa na pesa kabisa. Lakini kwa kuwa Mradi wa Soko Kuu la Bukoba lililopo katikati ya mji wa Bukoba ulikuwa na viashiria vyote vya kwamba ulikuwa ni mradi mzuri, ulikuwa hauwapi hofu yoyote TIB kwamba mradi huo ungeliweza kujilipa na kurejesha fedha zote katika muda ambao benki hiyo ilikuwa inaridhishwa nao. 
4. National Health Insurance Fund (NHIF), ni taasisi nyingine ya ambayo pia ilinunua kiwanja chenye eneo kubwa katika kata ya Kagondo ndani ya manispaa ya Bukoa, ambako wanakusudia kujenga jengo la ofisi za makao makuu ya mkoa wa Kagera. 
Kutokana na sababu ambazo Mh. Rwakatare, alisema ni za kusikitisha na hakupenda kuzirudia, miradi hiyo badala ya kuleta neema na kuwa chachu ya maendeleo ya Bukoba, ileguka kuwa laana na kusababisha malumbano makubwa ya kisiasa yaliyodumu kwa miaka mitatu na kusababisha Manispaa ya Bukoba kuwa kama imefungwa kwani hakuna kitu chochote kilichofanyika kwa miaka mitatu. Hali hiyo ya malumbano ilipelekea hata hao wawekezaji ambazo zote zilikuwa ni taasisi za umma kushindwa kuendeleza hiyo miradi waliyokuwa wameichagua kwani kulikuwa hakuna vyombo vya maamuzi, baada ya Madiwani walio wengi, wakati huo kutoka CCM kugomea vikao na mwisho wake walishitakiwa na baadhi ya madiwani walivuliwa udiwani kwa makosa ya kutohudhuria vikao vitatu mfululizo kadiri ya sheria zinavyowataka.
Kwa hiyo ziara aliyoifanya Mh. Rwakatare, na kukutana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya Manispaa ya Bukoba wakiwemo watu binafsi na baadhi ya taasisi zilizotajwa hapo juu, ililenga kuwahakikishia kwamba maadam sasa yeye ni Mbunge wa CHADEMA/UKAWA ambao ndiyo waliopata Madiwani wengi na hivyo kupelekea kuunda na kuingoza Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, kwamba sasa tuyaache yale yaliyopita tugange yaliyopo na yanayokuja.  Mh. Rwakatare, amewahakikishia wadau alioweza kukutana nao kwamba yeye na madiwani wenzake, wakiwemo hata wale wa CCM wamekwisha kuongea na kukubaliana kufanya kazi kama kitu kimoja na kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo kwa ajili ya kuinasua Bukoba kutoka kwenye mkwamo wa ki-maendeleo wa muda mrefu. 
Mh. Rwakatare, ameahidi kwamba atakapo fanya ziara nyingine Dar es salaam, atawafikia wadau ambao hakuweza kuwafikia ikiwemo TPB, TIB na Mzinga Corporation pamoja na wadau binafsi mmoja mmoja. Kwa wadau wa maendeleo ambao ni mtu mmoja mmoja, anakusudia kufanya hivyo kwa nia na lengo la kufikisha ujumbe kwamba katika awamu yake ya uongozi, yeye atakuwa ni mhamasishaji wa wananchi kwa ajili ya kujiletea amendeleo.  Alimalizia kwa kusema kwamba dhana ya kuwa kiongozi kwamba wewe ndiye utakayeweza kuleta maendeleo peke yako ni ubabaishaji ambao hauwezi kuleta maendeleo ya kweli.
“Bukoba tuitakayo inawezekana; kila mmoja atimize wajibu wake.”
Imeandikwa na Anic Kashasha
Simu: 0754 - 281229
Next Post Previous Post
Bukobawadau