Bukobawadau

HADITHI YA MWANGAZA SEHEME YA 1 & 2

Asubuhi sana, au wanasema alfajiri, majira ya saa 10, usingizi ulikata licha ya kuwa nililala saa sita usiku. Nilikaa kitandani nikiwaza itakuaje, na nilijikuta nikitumia muda mwingi sana kuwaza kiasi kwamba japo ilikuwa msimu wa ‘winta’ ambao jua huchelewa sana kuchomoza kwa nchi ya ughaibuni, jua ndilo lilinifanya nijue nimechelewa kazini.
Niligundua kuwa siku hiyo tayari nilipoteza masaa kadhaa ya kazi yangu. Niliamka haraka na kuanza kujiandaa. Haikunichukua nusu saa kabla sijamaliza kujiandaa na haraka sana nilielekea kituo cha usafiri (treni), kusubiri ili niende kazini.
Ghafla, nikiwa natembea, huku akili inashindwa kujizuia kuwaza na kutafakari juu ya kile kilichotokea kwa mpenzi wangu aliyeko Tanzania, nilikutana na yule niliyekuwa nikimtafuta kwa muda wa zaidi ya mwaka sasa. Sikuamini macho yangu kumuona rafiki yangu Mawazo. Inaonekana alikuwa anatoka supermarket (supamaketi). Hakuonekana kama mawazo niliyemfahamu. Nilimtazama kwa muda na kumuita lile jina la kijijini kwetu tulilolizoea ‘Luzoki’
Ni dhahiri na mimi nilikuwa nimebadilika kidogo hivyo sikushangazwa na yeye kutonikumbuka kwa haraka. Ila niliona mshangao machoni na akilini mwake kusikia jina la kijijini Tanzania katikati ya wazungu. Ilimpa tabu kidogo; nguo nyingi za baridi nilizovaa, ikiwemo kofia; pamoja na hali ya hewa ua Ughaibuni , vilinifanya nibadilike. Sikuwa Nathani yule wa miaka nane iliyopita tulipoagana na Mawazo. Tuliposogeleana, alishangaa sana sana. Hakutegemea kuwa tunakutana kwa mara nyingine.
Aliponifahamu, alinikumbatia huku machozi yakimtoka. Nilielewa sasa kuwa japo hali ya hewa, marafiki, na hali ya uchumi aliyonayo sasa ni tofauti kabisa , ukiachilia mbali mwonekano ambao pia umebadilika, bado moyo wa huruma na upendo wa Mawazo haukuweza kubadilishwa na hayo yote. Macho yake yalifanya nimuone Mawazo yule niliyekuwa tayari hata kugombana na wazazi wangu kwa ajili yake
Kwa mara nyingine nilijisemea moyoni ‘Sijutii uamuzi wangu’. Akiba yangu ya fedha niliyotumia kumsaidia akamilishe mipango yake ya safari ilinifanya nigombane na wazazi na ndugu zangu pia. Japo nilifanya hivyo kwa ajili ya thamani ya urafiki wetu, lakini pia nilikuwa na mategemeo makubwa kuwa kuna siku Mawazo angenisaidia kutimiza ndoto na malengo yangu ya kuagana na ufukara ambao familia zetu zilikuwa nao...
 MWANGAZA, Sehemu ya 2

Mwaka 1994, nikiwa ni kijana mdogo wa miaka 13, katika shule ya msingi ya Kilimahewa mkoani Singida, nilifanya uamuzi wa kuacha shule. Haukuwa uamuzi rahisi kwangu. Umasikini na hali ya maisha katika familia yetu ilinifanya nichelewe kuanza shule na hivyo nikiwa darasa la pili tayari nilikuwa naelewa nini maana na umuhimu wa elimu. Akili zangu darasani hazikuwa dhaifu japo hali ya maisha ilinifanya nishindwe kufanya vizuri darasani.
Tumezaliwa watoto nane kwa baba na mama, na mimi ndiyo mzaliwa wa kwanza. Wakati huo nilikuwa na wadogo zangu watano wote wa kiume. Baba hakufurahishwa nasi sana. Mara zote alisema, ”Nahitaji binti atakayejaza zizi langu”. Kila alipoenda kwenye sherehe za kuozesha watoto wa rafiki zake, alirudi akiwa amelewa na tulisikia akimpiga mama na kumwambia, nataka mtoto wa kike.
Vilevile baba hakuona kama ni kipaumbele kutusomesha. Mara nyingi alisema elimu ni gharama kubwa isiyo na faida. Nilipoona watoto wenzangu wakienda shule niliumia sana sana. Nilifatilia kujua gharama za kujiunga shule ni kiasi gani nikiwa na miaka tisa na nusu hivi. Haikuwa gharama kubwa sana japo sikuweza kumwambia baba. Wakati huo kazi yangu kubwa ilikuwa ni kuchunga mbuzi wa nyumbani. Mama alijua jinsi gani napenda kusoma na kila wakati alijaribu kumweleza baba juu ya elimu lakini mara nyingi hiyo mada ilimfanya aambulie kipigo au matusi.
Nilifanya uamuzi wa kutafuta pesa mwenyewe ili nijisomeshe. Nilipoenda kuchunga niliongea na wazee wenye mifugo ambao watoto wao wanasoma ili kwamba muda wa shule niwachungie mifugo yao, wanilipe. Kwa bahati nilipata hiyo fursa na ndani ya miezi sita nilifanikiwa kupata fedha ya kutosha kununua mahitaji yote ya shule pamoja na ada. Nilimshirikisha mama nia yangu ya kusoma, Machozi yalimtoka. Pengine aliwaza jinsi baba atakavyompiga akijua nimeanza shule. Au labda aliguswa na nia yangu na shauku ya kusoma. Siku hiyo mama alinambia maneno mazito sana. “Mwanangu, najua unapenda kusoma. Naumia kwamba wazazi wako tumekuwa tukikunyima hiyo nafasi mara zote, lakini naamini unajua mimi mama yako nataka usome. Najua haitakuwa rahisi kwako. Baba yako hatafuirahishwa na uamuzi wako. Wakati mwingine shuleni utapata changamoto nyingi, lakini mara zote kumbuka nipo upande wako. Hata kama sitakutetea utakapoumizwa, nitakuombea. Lengo lako liwe kusoma kwa jitihada zote ili siku moja ulete maendeleo kwangu na kwa wadogo zako."
Jinsi mama alivyoongea, japo nilikuwa bado mdogo, nilielewa ilikuwa ni hatari kwake na kwa ndoa yake kuniruhusu nisome. Siku hiyo usiku sikulala. Niliwaza sana na kulia. Kichwani zilinijia kumbukumbu za mama akipigwa na baba alipojaribu kuzungumza suala la shule. Mbele yangu kulikua na njia mbili, ’Nijiunge na shule na kumtesa mama, kisha baadaye nimtoe kwenye umasikini’ au ‘Niachane na shule na hizi hela ninazopata niwe nampa mama.'
Kesho yake niliamka nimefanya maamuzi. Tabia ya baba yangu kumtesa mama na kutuchukia ilinifanya nisimpende hata kidogo. Niliwaza moyoni, “Mama hatakiwi kuishi na baba siku zote. Lazima nisome, nipate maisha mazuri ili nimtenganishe mama na baba”. Hilo tu lilinipa nguvu na ujasiri wa kwenda kuanza shule. Nilimuahidi mama kuwa nitasoma kwa ajili yake na wadogo zangu. Sikuhiyo nilienda shule na kuonana na mwalimu aliyenipeleka kwa mwalimu mkuu. Nilimueleza mwalimu mkuu vitu vingi maana haikuwa kawaida mtoto kujiandikisha shule mwenyewe. Kwa bahati mbaya nilitakiwa kusubiri miezi kadhaa kabla muda wa kuandikisha watoto haujafika.
Nikiwa na miaka karibu kumi na mmoja nilianza chekechea. Nilikuwa mtoto mkubwa darasani lakini sikujali. Siku ambayo baba aligundua nimeanza shule, nadhani ilikuwa siku mbaya zaidi maishani mwangu kwa wakati huo. Baba alitufungia chumbani mimi na mama halafu alitumia mkanda wake maalumu wa ngozi kutuchapa. Mara zote nilisikia baba akimpiga mama wakiwa chumbani, lakini sikuwahi kujua alimpiga akiwa mtupu bila nguo yoyote. Baba alitoa nguo za mama mbele yangu na kumuacha na chupi tu, kisha akanilazimisha nami nitoe nguo. Alitupiga bila huruma. Alisema mama amepata wanaume wa kunilipia mimi ada. Aliniambia lazima niache shule. Siku hiyo mama alipigwa sana maana alionekana ni mwenye ujasiri. Alimweleza baba ukweli kuhusu namna nilivyofanya kazi mwenyewe kutafuta ada, japo baba alijifanya kutomuamini. Na pia alimwambia kuwa sitaacha shule hata kama itabidi anihamishe nyumbani.
Kesho yake sikuweza kwenda shule. Nilikuwa na maumivu makali. Kwakua baba hakuwa mtu wa kushinda nyumbani, nilipata nafasi nzuri ya kukaa kuongea na mama. Alijitahidi kutonionesha jinsi alivyoathiriwa na tukio la jana usiku. Aliniambia, hata ikimbidi apigwe kila siku, nisiache shule. Alisema, baba yako akiendelea kukupiga na wewe, nitakutafutia sehemu nyingine ukaishi. Kwa bahati, baba hakufanya hivyo tena siku nyingine, japo mara kadhaa alimpiga mama (kama alivyozoea), na kuna wakati alinitafutia sababu na kunipiga bila makosa, lakini si kwa namna alivyofanya usiku ule.
Nikiwa naendelea na shule, maisha yangu hayakuwa sawa na watoto wengine. Muda wangu wa kufanya kazi ya kuchunga kwa malipo ulipungua, hivyo kufanya kipato changu kipungue pia. Pesa haikunitosha tena kujilipia ada, kununua sare na mahitaji mengine ya shule. Nyumbani pia maisha yalizidi kuwa magumu kwani mama alipata ujauzito mwingine ambao ulimfanya aumwe na hivyo kushindwa kufanya shughuli zake za kuingiza kipato kama awali. Ni dhahiri baba hakuwa mtu wa kujali familia hivyo chakula chetu kilitegemea zaidi biashara za mama. Pesa kidogo niliyokuwa naipata niliigawana na mama ili kusaidia mahitaji ya nyumbani.
Mwaka huo nadhani ulikuwa mgumu zaidi kwangu na kwa mara ya kwanza niliruhusu wazo la kuacha shule linishinde. Ilikuwa siku ya jumatano niliporudi nyumbani na kumkuta mama yangu anaumwa sana. Alikuwa akitapika mfululizo na damu ilimtoka. Wadogo zangu walonifuata walikuwa wamekwenda kuchunga na kuteka maji. Aliyekuwa nyumbani na mama ni mdogo wangu wa mwisho kwa wakati huo aliyekuwa na miaka miwili, ambaye hangeweza kufanya chochote kumsaidia mama. Nilijua mama anatakiwa kupelekwa hospitali, hivyo niliita majirani tukampeleka hospitali.
Kabla hatujatoka nyumbani mama alinambia, “Mwanangu nisipopona utaenda kwa fulani (alimtaja mmoja wa rafiki zake wa karibu kijijini), utamwambia mama aliomba unisaidie niishi kwako. Lakini wadogo zako, bibi yako akija kwenye msiba utamwambia mama alisema aondoke nao.”[Bibi yangu aliishi kijiji kingine. Maisha yake na nguvu zake zingemfanya asipate shida kutunza wadogo zangu iwapo mama angefariki].“Ukikaa hapa baba yako hatakuruhusu uendelee na shule” aliongeza kusema kwa uchungu. “Pia anaweza kukuumiza kwa kukupiga”. Jinsi hali ya mama ilivyokuwa, na namna alivyoongea, nilijua fika kuwa baba ndo alisababisha kuumwa kule. Tulimuacha mama amelazwa hospitali halafu nilirudi nyumbani niliwa na hofu kubwa mno. Nilijilaumu sana kwani nilihisi kwa kung’ang’ania kwangu kusoma, ninakwenda kumpoteza mama yangu. Nilisema kuwa sitaendelea tena kusoma endapo mama atapona, au labda nitamshawishi sote tuhamie kwa bibi.
Baba aliporudi usiku na kumuulizia mama, nilimwambia kuwa tumemwacha hospitali. Aliniuliza kwa hofu kubwa maswali kadhaa na kunitaka twende wote hospitali usiku huo. Akiongea na daktari, sikuamini kile nilichosikia, japo nilijifanya siwasikii. Daktari alimwambia baba kuwa inaonesha mgonjwa kapigwa sana kiasi cha kusababisha tatizo kwa mtoto, na kama asingewahishwa hospitali huenda asingeishi. Aliongeza kuwa inatakiwa ripoti ya polisi ili kumtibu, japo walimpa huduma ya kwanza kuokoa maisha yake. Baba alimpa daktari kiasi cha hela na kumwambia aachane na habari ya polisi, amtibu tuu. Hapo ndipo nilipohakikisha kuwa kweli baba alikuwa amerudi nyumbani mchana na kumpiga sana mama kisha kuondoka tena. Nilipomuuliza mama sababu baada ya kupona alisema siku hiyo baba alitudi na kukuta mdogo wangu tunayefatana alikuwa amerudi kutoka machungoni akilia kuwa mbuzi mmoja kapotea. Baba alikasirika sana na kusema ni kwa sababu mama aliruhusu nisome badala ya kuchunga mali zetu, hivyo kuwapa majukumu wadogo zangu ambao bado ni wadogo. Baba alimrudisha mdogo wangu machungoni na huku nyuma alianza kumpiga mama. Alimpiga kwa hasira hadi mama kufikia hali mbaya, kisha akaondoka na kumuacha.
Siku mbili zilizofuata sikwenda shule. Ijumaa jioni alikuja rafiki yangu Mawazo. Ki-umri nilimzidi Mawazo kiasi, lakini tofauti na watoto wengi shuleni ambao walinidharau na kunichokoza kwa ajili ya utulivu wangu na umri wangu mkubwa, Mawazo alinijali sana. Mara zote huwa nasema, pengine Mungu alimleta ili kuongeza thamani ya maisha....
USIKOSE SEHEMU YA 3
SHARE na LIKE Ukurasa wetu wa Bukobawadau Entertainment Media
 AHSANTE KWA KUENDELEA KUPATA HUDUMA ZETU PIA KUJITANGAZA NASI , IWAPO UNAHABARI AMA TANGAZO WASILIANA NASI 0754 505043 / 0784 505045 Email .bukobawadau@gmail.com ,Insta @bukobawadau ANGALIZO KUMBUKA KILA MMOJA ANA MTAZAMO WAKE HIVYO TUMIA LUGHA NZURI KATIKA KUTOA MAONI YAKO IWAPO UTASHINDWA BASI NI HERI USITOE MAONI SI LAZIMA ILI KUEPUSHA MAKWAZO KWA WENGINE
Next Post Previous Post
Bukobawadau