Bukobawadau

HADITHI YA MWANGAZA SEHEMU YA 3

MWANGAZA, Sehemu ya 3:
Nilimueleza Mawazo juu ya uamuzi wangu wa kuacha shule. Katika umri mdogo, nilikuwa nimejifunza kuwa jasiri au pengine sugu, na mtu asiyependa kuonesha udhaifu au maumivu yake hasa kwa machozi, lakini siku hiyo nikiongea na rafiki yangu nililia sana kiasi cha kumfanya nayeye alie na kushindwa kunifariji. Nilimuelezea hali halisi ya nyumbani, japo alikuwa anafahamu kwa kiasi kikubwa tayari. Nilimuhadithia jinsi ambavyo nilikuwa hatiani kumpoteza mama yangu siku mbili zilizopita. Kisha nikamwambia juu ya uamuzi wangu wa kuacha shule. Nilijua Mawazo lazima angepinga uamuzi huo bila kujali ni kiasi gani namaanisha, ila sikujua ni kwa kiasi gani hasa Mawazo alijali elimu yangu.
Nilimuangalia Mawazo akiwa kama mtu aliyepigwa na butwaa akinisikiliza. Kadiri nilivyoanza kusisitiza kuwa sitaki tena kuendelea na shule ndivyo alivyozidi kubaki kama mtu aliyepoteza fahamu. Alinitolea macho huku akitokwa na machozi. Alinisikiliza na kukaa kimya kwa muda kiasi cha kunifanya nitamani kusikia kilichomo akilini mwake.
Urafiki wetu ulianza mara tu tulipoonana, nah ii nadhani kwa sababu yeye ni mtu mwenye huruma nyingi. Japo familia zetu sote zilikua na hali duni ya kiuchumi, wazazi wake walikua wanaelewana na kupendana, baba yake hakuwa mlevi kama baba yangu, alisapoti elimu na alipenda watoto wake, na hivyo kufanya hali ya maisha na uchumi kwao kuwa bora sana kuliko ya kwetu.
Mawazo alianza kuwa karibu na mimi baada ya kuona ni mtu niliyependelea kukaa pekeangu na vile wanafunzi wenzangu walivyonidharau. Sikuwa huru kwake mwanzoni kwani ki kawaida sikuwa mtu wa kujiamini au kuamini marafiki, lakini hiyo haikumsumbua. Alijipendekeza kwangu kana kwamba yeye ndo mwenye uhitaji sana wa urafiki wetu. Darasani Mawazo alikuwa kati ya watoto wanaofaulu sana. Na japo tulikuwa kijijini, lakini mipango yake na malengo makubwa aliyokuwa nayo yalinifanya nione kuwa kuna nafasi ya kufanikiwa kimaisha kama tungetia bidii kwenye masomo.
Urafiki wetu uliimarika zaidi nilipokuwa nikipata changamoto mbalimbali za maisha. Mawazo alinitambulisha kwa wazazi wake na ilinishangaza sana sana kuona kuwa kuna familia zinazoishi kwa upendo na maelewano. Wazazi wake pia walionesha kunijali kana kwamba tuna undugu. Nakumbuka mara ya pili kumtembelea Mawazo nyumbani kwao, nikiwa sina viatu baada ya viatu vyangu kuisha, baba yake alimwambia anipe viatu vyake vipya (alivyomnunulia vikawa vikubwa kwake), japo alikuwa amepanga kuvirudisha dukani. Kwakweli sikuwahi kukutana na mwanadamu wa namna hiyo maishani mwangu kabla. Siku ile yule mzee alinifanya nijisemee moyoni kuwa, japo baba yangu ni mtu katili na asiyefaa, bado nikiwa mkubwa nitataka niwe baba mwema na mwenye upendo kwa familia yangu na kwa watu wengine.
Rafiki yangu Mawazo alikuwa amenisaidia sana kufika hapo nilipokuwa. Japo bado tulikuwa madarasa ya chini lakini alikuwa amenionesha thamani kuu ya urafiki wetu. Alinifanya kujikubali tena mara zote nilipohisi kujikataa, alinifanya nimsamehe baba licha ya kuwa aliniumiza mara nyingi, alinisaidia kuwa na ndoto na malengo makuu maishani, alinifanya nijipe moyo wa kuendelea na shule licha ya vipingamizi nilivyokuwa nakutana navyo nyumbani, na mara zote alipoongea na mimi, hata kama nilikuwa nakaribia kukata tama, nilipata nguvu mpya. Kijana huyu mdogo alikuwa mwenye hekima nyingi na akili si tu za darasani, bali pia za kuishi na watu wote. Alipendwa na walimu shuleni na pia wanafunzi wengi tulimpenda kwani hakukuwa na kasoro ya kumtoa.
Baada ya kunitazama dakika kadhaa akilia, Mawazo alifungua kinywa kusema,”Nasikitikika kuwa ni uamuzi umekwisha fanya na siwezi kuubadili. Pengine ingekuwa ni mimi ningeamua hivyo pia kwani sidhani kama nina uwezo wa kubeba mzigo ulionao moyoni. Kinachoniuma ni jinsi ambavyo ndoto na maono yetu makubwa yanaishia njiani. Tulipanga tusome, tupate maisha mazuri, familia zetu zifaidi matunda yetu. Tulipanga tukiwa wakubwa wake zetu wasiishi kijijini na watoto wetu wasisomee shule za vijijini. Tulipanga tutajenga magorofa jirani mimi na wewe, na watoto wetu watakuwa marafiki kama sisi tulivyo.
Wewe ulipanga kuwa daktari mkubwa na mimi niwe rubani. Nilitamani siku moja nikiumwa nije hospitali kwako unitibu, lakini naona ndoto zote zinaishia hewani. Mimi nitaendelea kusoma, na nitakuwa na maisha mazuri. Nitakupa msaada wa kiuchumi kadiri nitakavyoweza, lakini sitaweza kutoa msaada wa kuitosheleza familia yako, wazazi wako, wadogo zako, mke na watoto wako na kukujengea nyumba mjini. Msaada pekee ninaoweza kukupa ni ushauri wa kukuomba usiache shule”.
Maneno ya Mawazo yalinifanya nisahau kama siku mbili zilizopita mama yangu alikaribia kuuawa kwa ajili yangu. Pia yalinifanya nisahau kama baba yangu anaweza fanya chochote ili nisiendelee kusoma. Nilifanya uamuzi mwengine tofauti siku hiyo kuwa NITASOMA, kwa gharama yoyote. Nilimuahidi Mawazo kuwa sitarudi nyuma na hakika kuna siku tutatimiza pamoja zile ndoto zetu. Japo alionekana kutoamini ninachomwambia, lakini alionekana mwenye furaha sana kujua kuwa nimeupokea tena ushauri wake na kubadili maamuzi
Siku zilipita, mama alipona, alijifungua salama, alibeba mimba nyingine na kwa bahati mtoto wa nane alikuwa wa kike. Siku mdogo wangu wa mwisho alipozaliwa, nikiwa darasa la tano, nilirudi nyumbani na kukuta furaha ya ajabu. Wakati huo baba alikuwa ameamua kuniruhusu nisome japo alikua hajishughulishi na gharama yoyote ihusuyo elimu yangu. Pia wadogo zangu wengine hawakuweza kusoma, alikataa kabisa. Ilibidi nifanye bidii zaidi shuleni nikijua mzigo wote wa familia ni wangu. Kwa sasa akili yangu ilikuwa imekomaa zaidi. Sikusumbuliwa na mambo ambayo awali yalinifanya nishindwe kujiamini na pia kufanya vizuri darasani. Walimu walinijua kama kijana mtulivu zaidi na aliye makini kwa kazi zake.
Wakati huo mimi na Mawazo tulikua tukichuana vizuri kwenye mitiani. Katika somo la hesabu yeye alifanya vizuri siku zote lakini katika somo la sayansi nilimzidi. Hii ilifanya mara zote yeye akiwa wa kwanza mimi ninafuata, ama mimi nikiongoza yeye anafuata. Urafiki wetu ulijulikana shuleni na nyumbani, na wanafunzi wenzetu walituonea wivu. Muda wa ziada tuliutumia kuomba walimu watufundishe na maisha yangu sasa yalikuwa yenye furaha zaidi.
Siku hiyo baba alikuwa amerudi mapema nyumbani kwani alipata taarifa akiwa katika shughuli zake, kuwa mama anajifungua. Mkunga aliyemzalisha mama alitoka ndani na kumpa baba habari njema kuwa amepatikana mtoto wa kike. Baba alikwenda kuita marafiki zake kadhaa, alichinja mbuzi haraka mchana huo na walikaa na rafiki zake wakisherehekea mpaka usiku wa manane nyumbani.
Kwa mara ya kwanza niliona baba yangu akimfurahia mama yangu kama mke wake. Alimpa pole, alimwambia kwa sauti ya upole, umenizalia mama yangu, na pia alimuahidi kuwa huo ni mwisho wa ugomvi wao. Japo alikuwa amelewa, lakini niliona hali ya kumaanisha katika maneno ya baba siku hiyo.
Baba alimpa jina la Neema, na kwa hakika neema ilikuwa imeingia nyumbani kwetu. Baba alianza kuonesha kubadilika. Kwa muda wa kama wiki mbili hakwenda tena kunywa pombe na mida ya mchana alirudi nyumbani na kukaa na mama na mtoto. Upendo wake kwa Neema ulionekana na kujulikana kwa kila mtu. Tofauti na nilichokiona kwa wadogo zangu wengine, baba alijifunza kukaa na mtoto na kumlea. Japo hakufanya lolote la ajabu ila kwa jinsi nilivyomjua ilikua ni ajabu sana kukaa amemshika mtoto mikononi mwake kwa muda wa nusu saa mfulilizo, akimuacha mama apumzike na kufanya shughuli nyingine. Kwa miezi ya mwanzo baba hakutaka mama afanye kazi yoyote na kwa bahati nzuri tulikuwa tayari ni vijana wakubwa tuliofundishwa kufanya kazi zote za ndani.
Like Ukurasa wetu wa Bukobawadau Entertainment Media kwa mundelezo wa Hadithi hii.
Next Post Previous Post
Bukobawadau