Bukobawadau

ZAO LA NDIZI KULIMWA KIBIASHARA NA KUTAFUTIWA MASOKO YA KIMATAIFA ILI KUKUZA UCHUMI WA MKOA WA KAGERAWakulima na Wajasiliamali wa zao la ndizi Mkoani Kagera wapewa somo na shirika lisilokuwa la Serikali la BTC Tanzania (Belgium Training Cooperative Tanzania) juu ya kulima kwa wingi zaidi zao hilo kibiashara na kufundishwa mbinu mbalimbali za kutafuta masoko ya uhakika ndani na nje ya nchi.

Kutokana na zao la ndizi kuwa ndiyo zao tegemezi  kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera  Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepokea ufadhili kutoka nchini Ubelgiji kupitia shirika la BTC Tanzania wa kutekeleza miradi mbalimbali itakayoendeleza zao la ndizi ili liwe zao la biashara Kitaifa na Kimataifa.

Kupitia BTC Tanzania vikundi vya wakulima wa zao la ndizi ikiwa ni pamoja na wajasiliamali walijengewa uwezo  jinsi  ya kuongeza uzalishaji wa zao hilo, kuongeza thamani (mnyororo wa thamani wa zao la ndizi) pamoja na uwezo wa kutafuta masoko ndani na nje ya nchi.

Mafunzo hayo yaliyofanyika tarehe 10 Februari, 2016 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera yalikuwa ya mwanzo kabla ya miradi hiyo ya kukuza uchumi wa Mkoa kupitia zao la ndizi haijaanza kutekelezwa kwa ngazi za chini kabisa vijijini.
Miradi hiyo ya kuendeleza zao la ndizi kwa kuliongezea thamani na kulitafutia masoko itatekelezwa na Makampuni  mawili yasiyokuwa ya Serikali chini ya Belgium Training Cooperative Tanzania ambayo yatahusika na wakulima moja kwa moja hadi ngazi za chini nayo ni, Ndugu Tanzania LTD na Bluwat and Investment.

Ndugu Tanzania LTD, Hii ni Kampuni ambayo itakuwa inajihusisha na uongezaji wa thamani ya zao la ndizi pamoja na upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Aidha, Bluwat and Investment, ni Kampuni itakayojihusisha na kuwafundisha wakulima katika vikundi jinsi ya kutunza fedha zao (kuweka akiba), na jinsi ya kuanzisha SACCOS za kukopeshana, na pia watawaelekeza wakulima jinsi ya kujiongezea kipato na kukuza uchumi wao kwa ujumla.

Wananchi wa Mkoa wa Kagera wanahamasishwa kuchangamkia fursa hiyo ili kujiajiri katika sekta hiyo ya kilimo na kulifanya zao la ndizi kuchangia uchumi wa nchi na kwa mwananchi mmoja mmoja ambaye ni mkulima  hasa kwa zao la ndizi ambalo limekuwa likistawi kwa wingi Mkoani humo.


Next Post Previous Post
Bukobawadau