Bi Paschazia Barongo pichani Mkurugenzi wa Chuo cha Ualimu ERA kilichopo Bukoa
Anaandika Phinias Bashaya,Mwananchi
Mapambano ya wanawake wenye
malengo ya kuhakikisha ndoto zao zinatimia kwa kutumia fursa zilizopo
yanakumbana na vikwazo vya kukatisha tamaa katikati ya mfumo unaoibua
changamoto mpya kila siku.
Ndivyo ilivyo kwa Paschazia Barongo
ambaye pengine ndiye mwanamke pekee nchini aliyefikia kiwango cha
kufanikiwa kupambana na changamoto mbele yake kuanzisha chuo cha ualimu.
Safari yake haikuwa rahisi hadi kuwa na usajili wa chuo katika Kata ya
Kitendagulo Manispaa ya Bukoba kwa ajili ya kufundisha walimu wa daraja
la III A na kuwa alisimama imara kuhakikisha anaifikia ndoto yake ya
baadaye ya kuwa na kituo cha elimu kinachoandaa vijana katika fani
tofauti.
“Nilikutana na vikwazo vingi njiani hadi kufikia hatua
hii lakini ‘I was too strong’, ningeweza kutumia fedha yangu kwenye
mambo mengine, lakini nilijua Serikali pia inahitaji wadau katika elimu
kama ilivyo kwenye sekta nyingine,’ anasema Paschazia
Anasema
chuo hicho kilichoanzishwa miaka miwili iliyopita kimelenga zaidi kutoa
huduma kuliko kufanya biashara na kuwa anaamini ana uwezo wa kufanya
jambo kubwa zaidi, huku akiwa na mtazamo wa kuwa na kituo cha elimu
kitakachotoa kozi tofauti.
“Niliingia kwenye elimu lengo siyo
kuwa na chuo cha ualimu, nataka baadaye iwe’Education
Center’itakayofundisha fani nyingine pamoja na kuwaandaa vijana kwenye
masomo ya kilimo biashara,’’anasema.
Kwamba kwa umri wake wa
miaka 53 anaamini ana uzoefu uliomsukuma kutafakari na kuchukua hatua
kwa vitendo na huo ndiyo mwanzo wa jina la chuo cha (ERA) ambao ni
ufupisho wa ‘Experience, Reflection and Action’
Arejea nyumbani
Anasema alikuwa na sababu nyingi za kubaki nchini Sweden akifurahia
maisha kama walivyo Watanzania wengine waishio nje ya nchi, lakini
aliona ana deni la kurudi nyumbani kutoa mchango katika elimu.
“Nilikuwa na sababu nyingi za kutofikiria hata kurudi lakini suala la
elimu liliniumiza hasa kwa wanafunzi ambao hawakuandaliwa katika
mazingira mazuri kielimu ukilinganisha na wanaofundishwa shule binafsi
kwa gharama,’’ anasema.
Anasema suala la wazawa wa Mkoa wa Kagera
kuwekeza katika maeneo mengine na kutelekeza nyumbani ni miongoni mwa
mambo yanayoufanya mkoa kudumaa na kuporomoka kiuchumi. Hata alipofunga
safari ya kurejea nyumbani na kuwekeza katika elimu bado aliowacha
ughaibuni wanahoji sababu ya kuacha mazingira mazuri na maisha yasiyo na
karaha na kujitumbukiza kwenye mfumo wa kutafutana.
‘’Kwa
mazingira tuliyokuwa tunaishi, wengi wanaogopa kurudi wakilinganisha na
changamoto zisizo za lazima watakazokuta huku nyumbani, mimi
walinishangaa niliwaambia Tanzania ni nyumbani lazima niwekeze
huko,’’anasema Paschazia.
Hata hivyo, anasema Serikali na wadau
wanatakiwa kujenga mazingira rafiki yatakayowavutia wazawa walioko ndani
na nje ya nchi kuwekeza badala ya kuwekewa vikwazo vinavyokatisha
tamaa.
Katika hatua hii ndipo anashangaa maajabu ya nchi hii
kwamba ilikuwa lazima fomu zake zipitishwe na baraza la madiwani ili
akubaliwe kuwa mmiliki utaratibu aliosema unasababisha usumbufu usiokuwa
wa lazima.
“Sitaona vibaya kama Ofisa Elimu au jopo la wataalamu
wa elimu litakuwa na jukumu la kukupitisha kuwa mmiliki, lakini sheria
inawapa nguvu madiwani kusaini fomu ili ukubaliwe ni kikwazo na
usumbufu,’’anasema.
Mwanamke huyo mwenye fani ya uuguzi anasema
wengi wanakumbwa na woga katika masuala mbalimbali na wapo wanaokimbilia
majukwaa ya siasa badala ya kusimamia na kuendeleza mambo mazuri
waliyoanzisha. ‘’Mimi naamini mwanamke ana uwezo wa kufanya jambo kubwa
kumzidi hata mwanaume jambo muhimu ni kupaza sauti yako na kujiamini
kuwa unaweza ukiona umekwama kwenye plan A siyo kosa kwenda hata plan
D,’’ anasema Paschazia na kuongeza kuwa:
“Wanawake wengine
wanatafuta ‘status’ kupitia majukwaa ya siasa badala ya kupigania
mafanikio kupitia masuala mengine ya maendeleo kwenye jamii, wapo
wanaofanya mambo mengi, lakini hayajulikani kwa kuwa wamekimbilia kwenye
siasa.’’
Anasema wapo wanawake wanaojulikana kwenye siasa,
lakini hawajulikani kwenye mambo mengine makubwa waliyofanya kwenye
jamii, wengine wamekumbwa na uoga unaowapunguzia kujiamini kufanya mambo
makubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
1 comment:
Karibu sana Mama Paschazia, Bukoba na Kagera kwa pamoja zinatuhitaji sana. Hongera.
Post a Comment