Bukobawadau

RC ARUSHA AKUTANA NA KUFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA DINI

MKUU WA MKOA WA ARUSHA AFANYA MAZUNGUMZO NA VIONGOZI WA DINI

Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mheshimiwa Mrisho Gambo(katikati)akizungumza na Askofu wa Kanisa la Anglikan,Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,Stanley Hotay(kushoto)  alipomtembelea ofisini kwake na kufanya mazungumzo nae akiwa ameambata na Mbunge wa Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki(Eala)Mheshimiwa Angela Kizigha.
Askofu wa Kanisa la Anglikan,Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,Stanley Hotay(kushoto) akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mh.Mrisho Gambo.
Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mheshimiwa Mrisho Gambo akiagana na Askofu wa Kanisa la Anglikan Dayosisi ya Mount Kilimanjaro,Stanley Hotay(kulia)  baada ya mazungumzo yao.
Nteghenjwa Hosseah – Arusha


Mkuu wa mkoa wa Arusha,Mrisho Gambo ameendelea  na  ziara yake ya kujitambulisha kwa viongozi wa dini  ukiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kukutana na viongozi  baada ya kuteuliwa kushika  wadhifa huo hivi karibuni.


Mh.Gambo amekutana na  Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT)Dayosisi ya Kaskazini Kati,Mchungaji  Solomon Masangwa , Askofu wa  Kanisa la Evangelistic Assemblies of God(EAGT) mkoa wa Arusha,Leonard Mwizarubi  na Askofu  Stanley Hotay wa Kanisa la Anglikana , Dayosisi ya Mount  Kilimanjaro.


Katika mazungumzo na viongozi hao kwa nyakati tofauti mbali na kujitambulisha aliwahakikisha dhamira ya serikali kulinda na kuheshimu uhuru na haki ya kuabudu ambayo imekuwepo nchini kwa muda mrefu ikiwa ni njia ya kuwa na taifa la watu wenye hofu ya Mungu.


Alisema kutokana na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dr. John Joseph  Magufuli kutaka kuwainua wananchi wa chini kupitia mapato ya ndani  halmashauri zimetenga asilimia 10 kutoka kwenye mapato hayo kwa ajili ya  mikopo yenye riba nafuu kwa Wanawake na Vijana wajasiriamali  zitakazowawezesha kufanya  shughuli za uzalishaji mali.


Amewataka  wawajulishe waumini wa dini zote na serikali iko tayari  kupanga utaratibu wa maafisa maendeleo ya Jamii na Vijana kupita na kutoa  elimu kwa makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na madhehebu ya dini hili iwe inufaishe watu wote katika mkoa huu bila kujali itikadi za kidini wala kisiasa.


Askofu Stanley Hotay aliupongeza uongozi wa mkoa kuimarisha hali ya utulivu na kuomba vyombo vya ulinzi na usalama ambavyo Mkuu wa mkoa ndiye Mwenyekiti wake kukabiliana na changamoto za kiusalama na viashiria vya uvunjifu wa amani.



Aidha alishauri  kutokana na idadi ya watu wanaotumia usafiri wa anga kuongezeka kuna haja ya Serikali kufikiria uwezekano wa kupanua zaidi uwanja wa ndege wa Arusha uliopo Kisongo  ili uweze kukidhi mahitaji ya sasa badala ya kutegemea uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro(KIA) pekee.


Mh. Gambo amewahakikishia viongozi hao kuwa serikali itakua ikiwashirikisha mipango mbalimbali inayokusudia kuitekeleza ili  watoe mawazo yao katika kuiboresha na  kuifanya itekelezeke   kwa wepesi zaidi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau