Bukobawadau

WAZIRI LUKUVI ATATUA KERO ZA WANANCHI WA KAGERA KUHUSU ARDHI AWAPANGUSA MACHOZI WALIODHURUMIWA ARDHI ZAO MUDA MREFU

Mhe. Lukuvi (Kulia) Akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kijuu Vitabu vya Orodha ya Makampuni Yaliyosajiliwa katika Masuala ya Upimaji wa Ardhi
Mhe. Lukuvi (wa pili kutoka Kulia) Akiongea na Watendaji wa Serikali
Mhe. William Lukuvi Akiwasili Ofisini kwa mkuu wa Mkoa wa Kagera Tarehe 18.09.2016
Mhe. William Lukuvi Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Wandaji Mbalimbali wa Serikali Wakimsikiliza Mhe. William Lukuvi.


WAZIRI LUKUVI ATATUA KERO ZA WANANCHI WA KAGERA KUHUSU ARDHI AWAPANGUSA MACHOZI WALIODHURUMIWA ARDHI ZAO MUDA MREFU
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi awapangusa machozi wananchi wa Mkoa wa Kagera waliokuwa wamedhurumiwa ardhi zao na walio kuwa  na kero za ardhi za siku nyingi ambapo alisikiliza kero hizo kwa umakini na kuzipatia ufumbuzi wa papo kwa hapo na kutoa haki kwa waliostahili.
Akiwa Mkoani Kagera katika ziara yake ya siku mbili Mhe. Lukuvi aliitumia siku yake ya kwanza ya tarehe 19/8/2016 kusikiliza, kupokea na kutatua kero mbalimbali za muda mrefu na zilizoshindikana  kwa wananchi  kuhusu ardhi ambapo kero nyingi alizisuluhisha na kuzipatia ufumbuzi.
Aidha kwa wananchi waliokuwawamejipatia ardhi kwa njia ya udanganyifu au kwa kuwatapeli wananchi wenzao waliamuliwa kurejesha ardhi hizo kwa wamiliki halali wenye hati zinazoonyesha mmiliki halali ni nani pia Halmashauri ya Manispaa iliamuliwa kuwapatia viwanja wananchi ambao walichukuliwa viwanja vyao na kuhaidiwa kupatiwa viwanja vingine ifikapo mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti 2016.
Katika kutoa haki kwa wananchi Mhe. Waziri Lukuvi alifuta umiliki wa ardhi ya Bw. George Rogers ambye alikuwa Mtanzania lakini aliamua kuchukua uraia  wa nchi ya Uingereza ambaye alikuwa na mgogoro na wananchi wa kata ya Nyanga katika Manispaa ya Bukoba.
Bw. Rogers raia wa Uingereza alifutiwa umiliki wa ardhi aliyokuwa anaimiliki katika eneo la Kata ya Nyanga Manispaa ya Bukoba kitalu namba 1(b) kilicho kuwa na ekari zaidi ya 1800, pia alifutiwa umiliki wa eneo la Kibuye katika Manispaa ya Bukoba lenye vitalu 9 na kufutiwa pia umiliki wa ekari 60 alizokuwa anazimiliki katika eneo la Bugolora Wilayani Missenyi.
Akitangaza kufuta umiliki wa maeneo yote hayo Mhe. Lukuvi Alisema kuwa Bw. Rogers na Kampuni yake ya Rockshild Quality Food Products Ltd hawakufuata utaratibu wa umilikaji wa ardhi bali yeye na Kampuni yake walijipatia ardhi hiyo kwa njia za udanganyifu kutoka kwa wananchi.
Aidha Mhe. Lukuvi alisema kuwa raia wa nchi za Kigeni hawaruhusiwi kuingia mitaani na kuanza kujinunulia ardhi kwa wananchi bali wanatakiwa kupitia katika kituo cha uwekezaji (Tanzania Ivestment Center) ambao wanayo dhamana ya kuwapatia wawekezaji au raia wa nchi za nje sehemu au ardhi za kuwekeza mahala popote nchini.
Mbali na kutatua migogoro ya mwananchi mmoja mmoja Mhe. Lukuvi alisema kuwa migogoro mikubwa kama ya wafugaji  na wakulima, mgogoro wa wananchi wa Kakunyu Wilayani Missenyi na Ranchi za Taifa tayari unashughulikiwa na Wizara nne ambazo ni Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Katika hatua nyingine Mhe. Lukuvi alisema kuwa ameamua kugawa majukumu ya wizara yake katika kanda ambapo masuala yote yanayohusu ardhi hayaendi tena Dar es Saalam bali yanamaliziwa katika kanda hizo na Mkoa wa Kagera upo katika Kanda ya Ziwa ambayo ipo jijini Mwanza.
Mhe. Lukuvi kwenye ziara yake Mkoani Kagera alifuatana na Kamishna Msaidizi wa Ardhi Kanda ya Ziwa Bw. Joseph Shewiyo, Msajili Msaidizi wa Hati Kanda ya Ziwa Bi Magrgeareth Mziray, na Msajili Msaidizi wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya Kanda ya Ziwa Bi Dorothy Philip ambapo Wataalam hao wakishirikiana na Maafisa Ardhi wa Halmashauri za Wilaya walimsaidia Mhe. Waziri Lukuvi kupata ufafanuzi wa kero mbalimbali na kupata ufumbuzi wa keo hizo katika Mkutano na wananchi uliofanyika katika viwanja vya Halmashauri ya Bukoba.


MAAGIZO NA MAELEKEZO YA WAZIRI WILLIAM LUKUVI KWA WATENDAJI WA SERIKALI MKOANI KAGERA KUHUSU MIGOGORO YA ARDHI
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi akiwa Mkoani Kagera katika siku yake ya pili mara baada ya siku ya kwanza kuitumia kutatua migogoro ya wananchi kuhusu ardhi siku ya pili ya tarehe 19.08.2016 aliitumia kuaongea na watendaji  mbalimbali wa Serikali akiwa mkoani hapa. 
Eneo la kwanza aliloliongelea Mhe. Lukuvi ni kuhusu migogoro ya ardhi kwa wanachi  iliyo mingi ilisababishwa na Watendaji wa Serikali waliopewa dhamana ya kushughulikia suala la ardhi, ambapo aliwaonya Watendaji wote kuacha tabia hiyo mara moja. Agizo, aliwaagiza Makatibu Tawala wa Mikoa wote nchini kuwachukulia hatua za kinidhamu au kuwafukuza kazi  Watendaji hasa Maafisa Ardhi watakobainika kusababisha migogoro ya ardhi katika maeneo yao.
Katika Agizo hilo Mhe. Lukuvi alimpa Onyo kali Mthamini wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba Bw. Projestus Katabalo kuacha mara moja kufanya kazi kwa mazoea bila kufuata sheria, taratibu na kanuni za utekelezaji wa zoaezi la uthamini.
Eneo la pili, Mhe. Lukuvi alisema kuwa kupitia Wizara yake Serikali imepanga ndani ya miaka kumi kuwa itakuwa imepanga, imepima na kumilikisha ardhi yote ya Taifa la Tanzania. Agizo, Mhe. Lukuvi aliagiza Mikoa yote nchini kuanza kuweka mipango ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Aidha aliuagiza uongozi wa Mkoa wa Kagera kuhakikisha unatoa hati miliki elfu kumi za ardhi kwa mwaka huu wa fedha 2016/17ambapo lengo la kitaifa ni hati Laki nne.
Agizo la pili ni kuhusu kupima maeneo yote ya Serikali (Serikali za Mitaa na Serikali Kuu) pamoja na kubaini majengo yote ya Serikali ambapo yeye kama Waziri mwenye dhamana atatoa hati maalum yenye msamaha wa kodi ya kumiliki maeneo ya Serikali ili yaachwe bila kuingiliwa na wananchi.
Agizo la tatu, ni Maafisa Mipango Miji kuhakikisha wanaainisha maeneo yote yaliyoiva kuwa miji ili yapangwe, kupimwa na kumilikishwa kwa hati za muda mrefu badala ya hati za kimila. Agizo la nne ni maeneo yote ambayo wananchi walijenga miaka ya zamani na yapo katika miji (Makazi Holela) nyumba zisivunjwe bali wananchi Warasmishiwe makazi hayo kwa kuyapanga.
Eneo la Tatu aliloongelea Mhe. Lukuvi ni Kuhusu Migogoro Mikubwa  ambapo alisema kuwa katika migogoro hiyo mfano wakulima na wafugaji, alisema kuwa Serikali imeamua kuunda kamati ya Wizara nne ili kamati hiyo ipitie migogoro yote mikubwa  na kutoa ushauri kwa Mawaziri wa Wizara hizo husika ili kukomesha kabisa migogoro hiyo.
Wizara hizo nia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Kilimo, Uvuvi na Mifugo, TAMISEMI, na Wizara ya Maliasili na Utalii.
Angalizo mikoa yote iliagizwa kuacha ugawaji wa Kata na Vijiji wakati wa Uchaguzi Mkuu bila kuihusisha Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwani mipaka inayotolewa na Mikoa inashindikana kuonana na mipaka ambayohupimwa  ardhini na Wizara ya Ardhi. Ili kusuluhisha hilo aliagiza Wizara yake kupewa taarifa pale Mikoa inapotaka kugawa maeneo yake lakini kwa sababu za msingi bila shinikizo la wanasiasa.
Katika kuhitimisha Mhe. Lukuvi alisema kuwa Wizara yake inatengeneza sera ya Ardhi, Nyumba na Makazi ambaop aliagiza Maafisa Mipango Miji wote nchini katika Halmashauri, Miji, Majiji, na Manispaa kuhakikisha wanaitisha vikao vya wadau ili kuamua aina ya rangi zipakwe katika miji badala ya kila nyumba kupakwa rangi yake na lengo ni kuifanya miji ipendeze kwa kuwa na mpangilio wa upakaji wa rangi.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu alimshukuru Mhe. Lukuvi kwa kufanya ziara yake Mkoani Kagera na kutatua kero mbalimbali za wananchi ambapo alimuhaidi Mhe. Lukuvi  kuwa maelekezoa na maagizo yake yote yatafanyiwa kazi  na wahusika ili kuhakikisha migogoro ya ardhi inakomeshwa Mkoani Kagera.
Next Post Previous Post
Bukobawadau