Bukobawadau

UJENZI WA CHUO CHA KISASA CHA UFUNDI STADI VETA KAGERA MBIONI KUANZA MARA MOJA BURUGO HALMASHAURI YA WILAYA YA BUKOBA


Na:  Sylvester Raphael
Ujenzi wa Chuo cha kisasa cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kagera wakaribia kuanza katika eneo la Burugo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba nje kidogo ya Manispaa ya Bukoba ili kutoa Elimu au Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa vijana wengi wanaohitimu elimu ya Msingi na Sekondari kutoka ndani na nje ya mkoa.
Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) Kagera kinatarajiwa kujengwa kwa ufadhili wa Serikali ya China, aidha,  Serikali hiyo imetuma wataalam wa sekta mbalimbali za ujenzi na tayari wamewasili mkoani hapa kuanzia Septemba 7, 2016 ili kufanya upembuzi yakinifu wa gharama za ujenzi wa chuo katika eneo kitakapojengwa.
 Wataalamu hao wanane kutoka nchini China waliwasili mapema asubuhi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kumsalimia na kujitambulisha ambapo kati yao kuna Mhandisi wa masuala ya Maji, Ujenzi, na Umeme ambao kwa mujibu wa kiongozi wao watafanya upembuzi yakinifu wa gharama za ujenzi, katika eneo husika, mfano kuona eneo kama linafaa, upatikanaji wa vifaa, gharama za vifaa na masuala yote yanayohusu ujenzi.
Mara baada yakuwapokea ofisini kwake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu aliwaeleza kuwa Serikali ya Mkoa ipo tayari kutoa ushirikiano kwao ili ujenzi wa chuo hicho uanze mara moja . Pia liwakaribisha mkoani Kagera pamoja na kuja kufanya upembuzi yakinifu lakini watembelee mkoa na  kuona Kagera ilivyobarikiwa katika fursa mbalimali za utalii na kiuchumi.
Chuo cha Kisasa cha Mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Kagera kinatarajiwa kujengwa na kuwa chuo cha mfano wa vyuo vya ufundi nchini ambapo kitadahili wanafunzi wengi na kitakuwa na fani mbalimbali za ufundi stadi ambazo zitakuwa zinaendana na hali halisi ya sasa ya Sayansi na Technolojia .
Mkoa wa Kagera tangu mwaka1987 hadi sasa hauna chuo cha (Vocational Educational and Training Authority, VETA) cha ufundi  isipokuwa kuna Kituo cha mafunzo ya ufundi (Vocational Training Center) VTC Rwamishenye ambacho ni kimojawapo kati ya vituo 27 vinavyomilikiwa na VETA chini ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi nchini.
Kutokana na VTC kagera kutokuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi wengi aidha, kuwa kituo cha mafunzo kisichokuwa na wanafunzi wa kulala (bweni) na kupelekea wanafunzi ambao ni wa nje ya Manispaa ya Bukoba kukosa elimu ya ufundi na kuishia mitaani baada ya kumaliza elimu ya msingi na sekondari ndiyo sababu Serikali ya Tanzania iliamua kujenga chuo cha kisasa Kagera ili kupunguza tatizo hilo.
Ni baada ya Serikali ya Awamu ya Nne chini ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Jakaya Kikwete kuamua kujenga Chuo cha Kisasa cha Ufundi,  Rais Kikwete aliiomba nchi rafiki ya China kujenga chuo hicho na kupendekeza kijengwa mkoani Kagera.
Aidha Mhe. Rais Kikwete alitangza uamuzi wa Serikali ya China kukubali kujenga chuo hicho cha Ufundi Stadi Mkoani Kagera Wakati akiongea na wazee wa Mkoa wa Dodoma katika Ukumbi wa Kilimani tarehe 04/11/2014 na kuipongeza Serikali ya China kwa kukubali ombi lake kwa dhati.
Wananchi wa  Mkoa wa Kagera hatuna budi kuupokea mradi wa ujenzi wa chuo hicho kikubwa cha kisasa na kitakachotoa elimu ya ufundi wa kisasa unaoendana na sayansi na teknolojia , pia na kutoa ajira kwa wananchi wa mkoa wetu wakati wa ujenzi na mara baada ya kumalizika kujengwa kwa chuo hicho.


Next Post Previous Post
Bukobawadau