Bukobawadau

HOSPITALI YA RUBYA YAHITAJI FEDHA KUPANUA WODI YA KUJIFUNGULIA WAJAWAZITO

Picha ya Pamoja ya wafanyakazi wa Hospitali ya Rubya , wawakilishi wa shirika la Jhpiego na Askofu  msaidizi wa jimbo la Bukoba Methodius Kilaini baada ya kupokea tuzo na cheti kutoka shirika hilo.
 Mganga mkuu wa Hospitali ya Rubya Dr George Kasibante akionesha Cheti baada ya kukipokea kutoka shirika la Jhpiego chini ya mradi wa huduma ya mama na uhai wa mtoto Mkoani Kagera kwa kutimiza vigezo ya wizara ya afya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto
 SR Theonestina John Muuguzi mkuu wa Hospitali ya Rubya akionesha tuzo iliyotolewa kwa Hospitali hiyo kutoka shirika la Jhpiego mkoani kagera kutokana na utendaji bora wa kutoa huduma ya mama na mtoto

MULEBA:Na Shaaban Ndyamukama
Kiasi cha Sh 200 milioni zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa wodi  ya akina mama wanaojifungua katika Hospitali ya Rubya wilaya ya Muleba mkoani Kagera  ili kupunguza msongamano wa wajawazito katika Hospitali hiyo huku wengine wakijifungulia kwenye wodi za kulaza watoto wachanga.
Mganga mkuu wa Hospitali ya Rubya Dr George Kasibante amesema  hayo leo wakati akitoa taarifa ya utoaji huduma za mama na mtoto kwa shirika la Jhpiego   na kwamba wanaofika kujifungua Hospitalini hapo ni kati ya 300 hadi 360  kila mwezi badala ya120 na  baadhi yao wanalala wawili katika kitanda kimoja
Dr Kasibante alisema hayo katika kupokea tuzo ya utoaji bora wa huduma ya mama na mtoto iliyotolewa jana  na Shirika la Jhpiego mkoani Kagera na kwamba  kipindi cha miezi sita kati ya June hadi Desemba 2016 wamejifungua wanawake 2,057 na baadhi yao hupelekwa  wodi za watoto ili wasijifungulie chini
Alisema  Hospitali hiyo inapokea akina mama wajawazito kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Muleba na baadhi yao hukaa kati ya siku saba hadi  mwezi mmoja ili wapate huduma bora ya uzazi wakati wa kujifungua. 
Pia alisema wanawake wanofika kujifungua hufikishwa kwenye jengo la muda lililojengwa kwa miti na kuzungukiwa mabati ambapo hukumbwa na changamoto ya joto na msongamano ikiwa ni pampoja na kuhofia kuambukizana magonjwa.
“Wanawake hao baadhi hujifungua watoto njiti ambao uongozi wa Hospitali licha ya kuwa na upungufu wa wauguzi umejitahidi kuwatunza watoto hao na kuokoa maisha yao na kuendelea kuishi wakiwa na mama zao”.Alisema Dr Kasibante
Afisa Mipango wa Shirika la Jhipiego kupitia mradi wa Mama na uhai wa mtoto mkoani Kagera Bi Alphonciana Barongo amesema licha ya changamoto za Hospitali ya Rubya, shirika hilo linaipatia tuzo na cheti kwa ajili ya utoaji huduma bora za afya na kupunguza vifo vya mama  na watoto.
Alisema Shirika la Jhipiego kupitia mradi wa Mama na uhai wa mtoto mkoani Kagera  katika wilaya ya Muleba mradi huo unahudumia Hospitali tatu za Rubya Kagondo na Ndolage, vituo vya afya vitano na zahanati saba na kwamba Hospitali ya Rubya imefikisha vigezo vya tuzo kwa kufikisha asilimia 85
“Wizara ya Afya  imekuwa ikitumia vigezo vya Tathimini kila kituo chenye mradi wetu kwa kuangalia utoaji wa huduma na upungufu wa vifo vya mama na mtoto hivyo uongozi wa Hospitali uongeze bidii kuhudumia wananchi” Alisema Barongo
Hata hivyo Askofu msaidizi wa jimbo la Bukoba Methodius Kilaini ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya afya hospitalini hapo amesema wafanyakazi na watumishi wanatakiwa kufanya kazi na kulinda maadili yao na kwamba  wasiowajibika wataondolewa ili kuepuka kuchafua sifa ya Hospitali hiyo
Alisisitiza  watumishi kufanya kazi kwa kutanguliza uaminifu upendo na maadili mema katika kuhakikisha wanawafariji wanaokuwa na changamoto za afya na kutumia fursa za zinazotolewa na mashirika ama serikali kuwajibika ipasavyo.
Next Post Previous Post
Bukobawadau