Bukobawadau

SHIRIKA LA JHPIEGO LATOA TUZO ZA KAZI KWA WATUMISHI WA HOSPITALI WILAYANI NGARA

Kaimu mganga mkuu wa Hospitali ya Nyamiaga Dr Simon Kyamwenge akipokea cheti kama tuzo ya Hospitali baada ya kutimiza vigezo katika Mradi wa afya ya mama na mtoto wa MCSP wengine ni watumishi wenzake wakishangilia kwa tuzo hiyo 
 Picha zote na Shaaban Ndyamukama kutoka wilayani Ngara .
 Wauguzi ,Waganga pamoja na Madaktari wa hospitali za Rulenge na Nyamiaga wilayani Ngara mkoani Kagera wakiandamana kuelekea katika ukumbi kupokea tuzo ya utendaji kazi bora wa huduma ya mama na uhai wa mtoto ( MCSP ) kupitia shirika la Jhppiego mkoani Kagera
  Wauguzi ,Waganga pamoja na Madaktari wa hospitali za Rulenge na Nyamiaga wilayani Ngara mkoani Kagera wakiandamana kuelekea katika ukumbi kupokea tuzo ya utendaji kazi bora wa huduma ya mama na uhai wa mtoto ( MCSP ) kupitia shirika la Jhppiego mkoani Kagera
 Wauguzi,waganga na madaktari wakiwa katika Picha ya pamoja na mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya ngara Aidan Bahama (mwenye suti nyeusi ) na Afisa mipango wa MCSP chini ya shirika la Jhpiego mkoani kagera Alphoncina Barongo  jirani kulia mwa mkurugenzi 
Hospitali ya Nyamiaga na Rulenge katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera zimepokea tuzo kutoka shirika la Jhpiego baada ya kutekeleza mpango  wa huduma ya mama na uhai wa mtoto  na kutoa huduma bora kwa walengwa baada ya kutimiza vigezo vya wizara ya afya Maendeleo ya jamii jinsia wazee na watoto 
Afisa  mipango wa afya ya mama na uhai wa mtoto (MCSP)  kupitia shirika la Jhppiego mkoani Kagera Alphoncina Barongo,  ametoa tuzo na vyeti kwa hospitali hizo  katika wilaya ya Ngara ambapo  mpango huo unahudumia hospitali tatu za Rulenge, Nyamiaga na Murugwanza, vituo vya Afya vitatu  na zahanati 12
Alphoncina Barongo amesema mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa serikali kuu, halmashauri za wilaya pamoja na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ya Jhpiego ,JSI, Save the Children, lengo likiwa ni  kupunguza vifo na kutoa huduma bora ya afya ya uzazi na watoto wachanga chini ya miaka mitano
Hata hivyo  Barongo amesema mkakati wa kutoa tuzo katika hospitali vituo vya Afya na zahanati ni kwa kila wilaya ambapo katika mkoa wa kagera ni vituo vya Afya 12 hospitali za wilaya na baadhi ya zahanati  kuanzia Bukoba manispaa , Muleba , Biharamulo , Ngara , Karagwe , Bukoba vijijini na Misenyi
Kaimu mganga mkuu wa Hospitali  ya Nyamiaga Dr Simon Kyamwenge amesema pamoja na kupewa tuzo hiyo na cheti bado Hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya wagonjwa hasa wanawake wajawazito ambao hujifungulia sakafuni kwa kukosa vitanda pamoja na changamoto ya kifedha ya ruzuku toka serikalini 
Amesema Hospitaliya hiyo inakabiliwa na changamoto  za utoaji huduma za afya kwa wananchi ikiwa ni pamoja na uhaba wa  fedha za ruzuku ya  serikali ( OC)  na kutegemea mapato ya mfuko wa bima ya Afya ya Taifa NHIF pia fedha za papo kwa papo zitokanazo mfuko wa afya jamii CHF
Dr Kyamwenge amesema hospitali hiyo pia   inakabiliwa na uhaba wa vyumba vya mama  na watoto  (wodi) wakati wa kupata huduma ya kujifungua ambapo chumba kilichopo kina uwezo wa vitanda vitatu vya kujifungulia badala ya sita, kuna chumba  cha upasuaji chenye vitanda vinane badala ya vitanda 24
Ameongeza kuwa  hospitali  haina chumba cha kuhudumia watoto wachanga ambao   huchanganywa na watoto njiti kwa kulazimika kulala na mama zao kwenye vyumba vyenye msongamano wa wagonjwa, na kwamba ili kukidhi mahitaji hayo zaidi ya shilingi milioni 400 zinahitajika kujenga vyumba hivyo.
Pamoja na hayo mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya ngara Aidan Bahama ametoa wito kwa watumishi wa hospitali hizo kufanya kazi kwa kuzingatia taratibu kanuni na sheria za utumishi ikiwa ni pamoja na kulinda maadili yanayokubalika kijamii  huku wakitoa lugha rafiki ya kuwawezesha wagonjwa kupata matumaini ya kupona licha ya kuhitaji dawa na huduma nyinginezo
Next Post Previous Post
Bukobawadau