Bukobawadau

“SHIRIKI KUTOKOMEZA MALARIA KABISA KWA MANUFAA YA JAMII”

 Zoezi la Upuliziaji wa dawa ya Ukoko Majumbani Lazinduliwa Rasmi Mkoani Kagera

Na Sylvestera Raphael
Hiyo ni kaulimbiu ya uzinduzi wa zoezi la upuliziaji wa dawa ya ukoko majumbani kwa ajili ya kuua mbu waenezao malaria katika Mkoa wa Kagera kwa mwaka 2017 zoezi lililozinduliwa leo tarehe 23 Januari, 2017 katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi eneo la Kyaka na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum M. Kijuu.

Akizindua zoezi hilo Mkuu wa Mkoa alilishukuru shirika la TBT Associates kwa kuendendelea na juhudi za kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili kupunguza tatizo la ugonjwa wa Malaria katika mkoa wa Kagera kwa muda wa miaka kumi sasa tangu mwaka 2007.

Aidha, Mhe. Kijuu alisema kuwa Kimkoa, kiwango cha maambukizi ya malaria kilikuwa 42% mwaka 2007. Baada ya utekelezaji yakinifu wa afua mbalimbali za kupambana na ugonjwa wa malaria ikiwemo, matumizi sahihi ya  vyandarua, unyunyiziaji wa dawa ya ukoko majumbani, kupima na kutoa tiba sahihi, pamoja na usafi wa mazingira kwa ajili kupunguza mazalia ya mbu, kiwango cha maambukizi kilishuka na kufikia 9% mwaka 2011.

Mwaka 2016, takribani wagonjwa 446,285 waliugua malaria. Asilimia 24.5% ya wagonjwa waliohudhulia katika vituo vya kutolea huduma za Afya katika Mkoa walikutwa na Malaria. Kwa Wilaya ya Missenyi wagonjwa wanaougua malaria wamepungua kwa asilimia 54% kwa mwaka 2016, kwa watoto chini ya miaka 5 wagonjwa wamepungua kwa asilimia 64% na kwa watu wazima asilimia 45%. Hii imechangiwa kwa kiasi kikubwa na upuliziaji wa dawa ya ukoko uliofanyika mwaka 2016. Alisistiza Mkuu wa Mkoa.

Aidha Mkuu wa Mkoa wa Kagera alitoa wito kwa wananchi wa Halmashauri za Wilaya za Bukoba (Vijini) Ngara na Missenyi kutoa ushirikiano kwa maafisa wanaohusika na zoezi hilo ili kila nyumba iliyopangiwa kunyuziwa dawa ya ukoko unyunyiziwe bila kipingamizi chochote ili kufanikisha lengo lililokusudiwa la kutokomeza ugonjwa wa Malaria.

Dk. Magesa Mratibu wa Mradi wa TBT Associate alisema kuwa zoezi la upuliziaji wa dawa ya ukoko mjumbani kwa mwaka 2017 inaanza rasmi tarehe 25.01.2017 kwa Halmashauri za Wilaya tatu Bukoba Ngara na Miseenyi na litadumu kwa siku 24 na litahitimishwa tarehe 21 Februari, 2017. Aidha, nyumba 163,299 zinatarajiwa kupuliziwa dawa hiyo na kikosi cha wapuliziaji 743.

Zoezi la upuliziaji wa dawa ya ukoko majumbani litavihusisha vyombo vya Ulinzi na Usalama ili kuhakikisha linafanikiwa vizuri kutokana na baadhi ya wananchi kuwa na mitazamo tofauti au imani potofu juu ya dawa ya ukoko na kupelekea kuwahamsisha wananchi kutotoa ushirikiano katika majumba yao yapuliziwe dawa hiyo.

Wito kwa wananchi wa Halmashuri za Wilaya za Bukoba, Ngara na Missenyi ni kutoa ushirikiano ili kila nyumba iweze kupuliziwa dawa ya ukoko ili kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa malaria unaoenezwa na mbu. Kama zoezi hilo litafanikiwa kwa kiwango kikubwa ugonjwa wa malaria utatokomezwa na kuwaacha wananchi kufanya kazi zao bila madahara yoyote ya mwili yanayosababishwa na ugonjwa wa malaria
Next Post Previous Post
Bukobawadau