Bukobawadau

UFAFANUZI WA ACACIA DHIDI YA TUHUMA ZA USAFIRISHAJI WA MAKINIKIA YA DHAHABU/SHABA

Buzwagi Mining site.
Wakuu napenda kuwapa habari hiyo juu ya makinikia ya dhahabu/shaba.

===============
 Zimepita wiki tatu (3), tangu kutangazwa kwa zuio la ghafla la ushafirishaji wa makinikia ya dhahabu/shaba lililotangazwa tarehe 2 Machi. Tangu kutangazwa kwa zuio hilo kumekua na upotoshwaji mkubwa wa taarifa kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Hadi sasa, Acacia haikutoa tamko lolote hadharani, sababu tumekua tukielekeza jitihada katika kutafuta muafaka na Serikali juu ya nini kifanyike. Lakini, kutokana na kiwango kikubwa cha taarifa potofu na zisizo sahihi zenye uvumi mwingi ambao unaweza kutuletea taswira mbaya kwa kampuni, kwa wafanyakazi wetu na pia kwa Tanzania kwa ujumla, tumeamua kuweka wazi hali halisi juu ya hoja mbalimbali.

Acacia inapinga vikali kuhusika na madai yaliyotolewa mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya ukaguzi bandarini – Dar es Salaam kwamba sisi tulikua tukifanya njama za kutorosha makontena yenye makinikia ya dhahabu/shaba nje ya nchi licha ya katazo lililotangazwa na Serikali. Ukweli ni kwamba si Acacia wala wateja wetu walijaribu kusafirisha makinikia haya nje ya nchi.

Kabla ya kutangazwa kwa zuio hilo, makontena, 256 ambayo sasa yamehifadhiwa ZamCargo (zamani ikijulikana kama Mofed - ambaye ni wakala wa usafirishaji wa forodha Customs Freight Services, CFS) yalikuwa tayari yamesafirishwa kutoka migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, na makontena mengine 21 yaliyokutwa katika bandari ya Dar es Salaam yakiwa tayari yameidhinishwa na idara ya forodha ya Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) na yalikua tayari kusafirishwa. Zoezi hili huwa linajumuisha TRA pamoja na Wizara ya Nishati na Madini (MEM) ambao kwa pamoja wanahusika katika mchakato wa kusafirisha mikinikia nje ya nchi kwa utaratibu maalum.

Acacia imekuwa ikisafirisha makinikia nje ya nchi kutoka mgodi wa Bulyanhulu tangu mwaka 2001 na kutoka mgodi wa Buzwagi tangu mwaka 2010 huku ikiweka bayana mapato yote yanayohusiana na makinikia ya dhahabu/Shaba na kuwasilisha Serikalini. Mapato haya pia yamekua yakitolewa kama mrahaba na malipo mengine kama kodi ya mapato kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Sheria za Tanzania zinaruhusu migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi kuuza nje ya nchi makinikia ya dhahabu/Shaba, sambamba na kusafirisha makinikia ndani ya makontena. Migodi hii imekua makini kukidhi vigezo vyote vya kisheria na matakwa ya vibali vya usafirishaji (Export Permits).

Tunapenda umma ufahamu kua kila kitu tunachokifanya kinathibitishwa na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA). Kila kontena la makinikia linalosafirishwa linachukuliwa sampuli chini ya uangalizi wa idara zote za usimamizi ambazo ni TMAA na Kampuni ya huduma za maabara (SGS) ili kwamba Acacia na Serikali ziweze kukadiria wingi wa madini ya dhahabu, shaba na fedha yaliyomo. Matokeo ya sampuli hizi hupelekwa TMAA, TRA, Acacia na kampuni zenye mitambo maalum ya kuyeyusha na kuchenjua makinikia (Smelters) ili kubaini mrahaba wa awali ambao Serikali italipwa kabla ya kusafirisha makinikia.

Ni pale tu ambapo upimwaji wa sampuli umekamilika, na mrahaba umeshalipwa kwa Serikali, ndipo makontenta yanafungwa kwa lakiri maalum za TMAA, MEM na TRA, na makinikia yanaweza kusafirishwa kutoka migodini. Kisha makontena husafirishwa wa magari ya kubebea mizigo hadi kituo cha forodha cha Isaka ambako nyaraka za mwisho za kusafirisha nje ya nchi hutolewa na MEM pamoja na TRA, na makontena kuidhinishwa kwa safari ya kwenda bandari ya Dar es Salaam.

Baada nyaraka zote kukaguliwa na kuhakikishwa na maafisa wa forodha, kila kontena hukaguliwa kwa kutumia mtambo maalumu wa kieletroniki (Scanner) ili kuthibitisha kua ndani yake hakuna kitu kingine chochote isipokua makinikia ya dhahabu/Shaba tu. Baada ya hapo makontena huhifadhiwa chini ya ulinzi wa maafisa wa forodha mpaka hatua za mwisho za upakiaji wa makontena kwenye meli tayari kwa kusafirisha nje ya nchi.

Acacia iko tayari kushirikiana na Serikali kutafiti uwezekano wa Tanzania kua na kiwanda cha uchenjuaji ambacho kitatoa ajira na kuleta maendeleo kwenye sekta hii. Maendeleo ya teknolojia yanaweza kutoa muelekeo stahili juu ya uwezekano huu.

Hadi hivi sasa, migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi imeendelea na uzalishaji kama kawaida hata baada ya zuio la Serikali na makinikia haya yamehifadhiwa katika maeneo maalumu migodini. Lakini hali hii haiwezi kua ya kudumu kutokana na umuhimu wa kukusanya mapato yatokanayo na biashara ya makinikia kwa migodi hii miwili.

Acacia inaunga mkono kikamilifu jitihada za bila kuchoka za Mh. Rais Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali yake kuwekeza katika maendeleo ya nchi kupitia elimu, ajira na viwanda. Acacia ni mwajiri mkubwa nchini Tanzania na sasa tumetoa ajira za moja kwa moja za zaidi ya wafanyakazi 5,000 pamoja na wakandarasi na ajira zingine 55,000 katika uchumi, zinazofaidisha familia na jamii kwa ujumla. Kati ya waajiriwa wote wa Acacia, zaidi ya asilimia 96 ni Watanzania. Migodi yetu inasaidia kuendeleza wazawa kupitia idara yetu ya ugavi ili kuwapatia fursa endelevu za kibiashara.

Tunapenda kuendelea kuwakaribisha maafisa wa serikali kuja kutembelea migodi yetu ili waweze kufahamu mchakato mzima wa kuzalisha madini, kukusanya sampuli na kusafirisha makinikia ya dhahabu/shaba nje ya nchi.


Next Post Previous Post
Bukobawadau